Dj Travella: Singeli Haihitaji Kingereza Kimataifa

Dj Travella: Singeli Haihitaji Kingereza Kimataifa

Msanii wa muziki wa Singeli ambaye pia ni Dj wa kimataifa, Dj Travella ameweka wazi kuwa lugha ya kiswahili kwenye muziki huo kwa mashabiki wa nje ya Tanzania sio tatizo.

Travella amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 14, 2025, kwenye uzinduzi wa tamasha la Singeli Vibes, litakalofanyika Mei 15,2025, Tip Top jijini Dar es Salaam.

"Naweza nikasema kikubwa wanachohitaji ni muziki wa Singeli. Kwasababu kila Dj ana mtindo wake na vionjo vyake kwa hiyo kingereza sio kisingizio kwamba usipojua huwezi kufanya shoo," amesema Dj Traveller.

Amesema kwa muda aliofanya shoo nchi za nje amegundua muziki wa Singeli unapendwa kuliko aina nyingine ya muziki kutokea nchini.

"Singeli ni muziki wa tofauti na unapendwa sana hata wakisikiliza wanakuwa na moyo wa kusikiliza tena na kukuita tena kwenye shoo, tofauti na nyimbo nyingine za kibongo.

"Singeli huko imeshakuwa kubwa, kibongo bongo wanaweza kuwa wanaichulia poa lakini singeli kule imeshakuwa kubwa. Mimi na miaka karibia minne nasafiri kufanya show sijawahi kumaliza mwezi nimekaa Bongo, shoo ni nyingi za Singeli huko," amesema Travella.

Kwa upande wake meneja wa wasanii wa Singeli kimataifa, Manager Abbas amesema kwa sasa Singeli ipo katika nafasi nzuri kutokana na matamasha mengi kuwahitaji wasanii wa muziki huo.

"Kwasasa muziki wa Singeli tulipofikia tupo hatua nzuri na tumepata matamasha mengi ya kushiriki kwa ajili ya kuwakiliaha muziki wetu, huu pendwa kuna wasanii tofauti tofauti wamesafiri ni mashahidi na hii yote inatafsiri muziki wetu huu ni pendwa na mzuri,"amesema

Amesema kwa kutambua mchango wa muziki huo wameamua kuja na tukio kubwa la Singeli Vibes huku wakishirikiana na waandaaji wa matasha makubwa ya muziki kimataifa Boiler Room ili kuwatangaza wasanii wa muziki huo.

"Tunafanya shoo ya muziki wa Singeli lakini tumekaribisha washirika wetu ambao tunafanya nao kazi za nje ya nchi, lengo ni kuwatangaza wasanii wa Singeli," amesema Abbas






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags