Olipa Assa, Mwananchi
Dar es Salaam. Msanii wa Bongo Fleva wa miondoko ya R$B, Ben Pol anatarajia kuachia wimbo aliofanya na DJ Don Diablo kutoka Ulaya.
Mwaka 2016 Diablo alichukua nafasi ya 15 ya heshima katika orodha ya Jarida la DJs 100 Bora 2024. Akiwa katika Top 100 ya DJs ya DJMag.com na kafanya kazi na wanamuziki mbalimbali wakubwa duniani. Hivyo kushirikiana wimbo na Pol inamsaidia kumtangaza zaidi duniani.
Akizungumza na Mwananchi Pol amesema kwa mara ya kwanza walikutana na Diablo Zanzibar katika Taasisi ya World Resource International(inayohusu mambo ya mazingira).
"Nilirekodi Tanzania ila DJ Diablo alitengeneza muziki na kuumalizia. Video ipo tayari hivi karibuni tutauachia. Ukiacha huo zipo nyimbo nyingine nilizozifanya, naamini mashabiki wangu watazifurahia ," amesema Pol ambaye nje na muziki anajishughulisha na kilimo cha mazao.
Mbali na hilo amesema kati ya albamu anazozisikiliza mara kwa mara ni ya Darassa 'Slave Becomes A King', na kinachomvutia kila wimbo una utofauti, jambo linaloonyesha ubunifu wa msanii huyo.
"Katika albamu hiyo Darasa amefanya kazi kubwa, kila wimbo unatamani kuusikiliza kwa nafasi, zina ujumbe unaofundisha maisha hasa kwa mtu ambaye anatamani kufika mbali kimaisha," amesema na kuongeza;
"Kuna wimbo mwingine ninaoupenda unaitwa 'Nimetumwa Pesa' umeimbwa na Billnass, Darasa na mimi mwenyewe ambapo nimeimba kiitikio, umetukutanisha watu wenye historia sawa za kutokea maisha ya chini hadi kutegemewa na zetu ."
Kwa wasanii wa kike amesema anapenda kuusikiliza wimbo wa Alele ulioimbwa na Ruby ambao umeonyesha ufundi wa sauti na kipaji kikubwa alichonacho.
"Wimbo huo kauimba kwa hisia kubwa, umeonyesha kipaji chake ni wimbo ambao sijawahi kuuchoka," amesema Ben ambaye amewahi kutamba na nyimbo mbalimbali kama Moyo Mashine,Maneno,Nikikupata, Im in Love na nyigine nyingi.

Leave a Reply