Asha Baraka: Jaydee, Nandy, Zuchu Endeleeni Kuzalisha

Asha Baraka: Jaydee, Nandy, Zuchu Endeleeni Kuzalisha

Mkongwe wa muziki wa dansi na mwenyekiti wa bendi ya Twanga Pepeta, Asha Baraka 'Iron Lady' ametoa wito kwa wasanii wa Bongo Fleva wakiwemo Lady Jaydee, Nandy na Zuchu kusaidia katika kuinua vipaji vya wasanii wapya wa kike ili watimiza ndoto zao.

Asha Baraka ametoa wito huo kwa wasanii hao leo Jumatano, Agosti 6, 2025, kwenye mkutano na waandishi wa habari akielekea kusherehekea miaka 30 ya muziki wake Agosti 28, 2025 The Superdome, Masaki, Dar es Salaam.

Amesema ni muhimu kwa wasanii hao wa Bongo Fleva kuzalisha wasanii wengine wa kike kupitia wao bila kukata tamaa, kama yeye alivyofanya kupitia bendi ya Twanga Pepeta.

"Mfano Lady Jay amefanya miaka 25 ya muziki wake inabidi amkuze Lady Jaydee mwingine atokee, kuna Zuchu japo ni mdogo inabidi amkuze Zuchu mwingine. Nandy naona juzi alijaribu kumsaini msanii wakike kwahiyo anatakiwa aendelee na sio kukata tamaa kuna kuwa na changamoto tuu ndogo ndogo kama mimi nilivyo muinua Luiza Mbutu kwahiyo Luiza anatakiwa kumuinua mwanamke mwingine na tayari kuna msichana ndani ya Twanga Pepeta anaitwa Fatuma," amesema

Asha amesema lengo kubwa la kusherehekea miaka 30 ya muziki wake ni kutaka kuwainua wanawake wengine wasiogope kufanya muziki.

"Lengo kubwa ni kutaka kuwainua wanawake wasiogope kufanya hizi shughuli za muziki. Tunataka tuwe na wanawake wengi, wanawake wakue na wawavute wengi kwenye changamoto za kimaisha kwasababu kila nyumba kuna mwanamke, sasa sisi tupo kwenye muziki lazima tuwasaidie wanamuziki," amesema Asha Baraka.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags