Albamu ya kwanza ya Tems kuachiwa mwaka huu

Albamu ya kwanza ya Tems kuachiwa mwaka huu

Baada ya kushiriki kuandika nyimbo za mastaa wakubwa duniani kama Beyonce na Rihanna, hatimaye Temilade Openiyin ‘Tems’ kutokea nchini Nigeria ametangaza kuwa mwaka huu ataachia albamu yake ya kwanza.

Tems (28) alivuma zaidi Afrika kufuatia kushirikishwa na Wizkid katika wimbo, Essence (2020), uliochaguliwa kuwania Grammy na kushinda BET 2022 kama Wimbo Bora wa Kushirikiana, huku Tems akishinda kama Msanii Bora wa Kimataifa.

Katika mahojiano yake na Billboard yaliyochapishwa mapema wiki hii, Tems amesema ana uhakika kwa asilimia 1,000 kuwa albamu hiyo itatoka mwaka huu ingawa hafikirii sana kuhusu matokeo yake ya kimauzo sokoni.

Hata hivyo, Tems aliyeshinda Grammy 2023 kupitia kolabo yake na Future, Wait For U (2022), bado hajataja jina na albamu hiyo, tarehe ambayo itatoka pamoja na orodha ya nyimbo zake na wasanii walioshirikishwa.

Utakumbuka hadi sasa Tems ameachia EP mbili, For Broken Ears (2020) na If Orange Was a Place (2021), EP yake ya kwanza ndiyo ina wimbo wake maarufu ‘Free Mind’ ambao ulishika nafasi ya kwanza chati za Billboard U.S. Afrobeats Songs na Bubbling Under Hot 100.

Vilevile Tems alizungumzia wimbo wake mpya, Not An Angel (2023) na kusema unahusu kujua thamani yako na kusonga mbele maishani bila kujali chochote kile kinachokuzuia kufanya hivyo.

Tems anayefanya vizuri na wimbo wake, Me & U (2023) alimshukuru Future kwa kumpa shavu katika kazi yake, pia alimshukuru na Drake kwa kumshirikisha katika wimbo wake ‘Fountains’ kutoka katika albamu yake ya sita, Certified Lover Boy (2021).

“Sina hakika kama nitawahi kufahamu athari zozote za hadithi yangu, lakini inatia moyo kujua kwamba nimewatia moyo wengine kwa sababu nami nimetiwa moyo na watu wengine pia. Inanitia moyo kwa hatua hiyo,” alisema Tems.

Tems anatazamiwa kutumbuiza katika tamasha la Coachella 2024 nchini Marekani hapo Aprili pamoja na wakali wengine wa Hip Hop na R&B kama Jhene Aiko, Blxst, Victoria Monet na Tinashe.

Ikumbukwe Tems alizaliwa Juni 11, 1995 huko Lagos, Nigeria, muda mfupi baadaye familia yake ilihamia Uingereza maana Baba yake ni raia wa huko, akiwa na umri wa miaka mitano wazazi wake waliachana kwa talaka, hivyo akareja Nigeria na Mama yake.

Alijiunga na Chuo cha Dowen huko Monash Afrika Kusini, alipopata Shahada ya Uchumi, akiongea na Hot 97 mwaka 2021, Tems alisema jamii anayotoka ni lazima kwenda shule ili kupata kazi itakayokupa malipo makubwa ila aliacha kazi ya ofisini kisa muziki.

Tems alianza kuimba akiwa na umri wa miaka 13, alipojiunga na kwaya na kujifunza kupiga piano, alivutiwa na wasanii kama Aaliyah, Destiny’s Child na Lil Wayne, huku akiutengeneza mwenyewe wimbo wake wa kwanza, Mr. Rebel (2018)






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags