Licha ya Rayvanny kushirikiana na aliyekuwa bosi wake kimuziki, Diamond Platnumz katika nyimbo 10, hakuna hata moja iliyofikia rekodi aliyoipata katika nyimbo mbili tu alizomshirikisha Zuchu aliyetoka kimuziki miaka minne iliyopita.
Staa huyo wa Next Level Music (NLM) aliyekulia WCB Wasafi yake Diamond, nyimbo mbili alizotoa na Zuchu hadi sasa ni Number One (2020) na I Miss You (2022) huku zote zikipata mapokezi mazuri kutoka mashabiki wao.
Utakumbuka Rayvanny na Diamond wameshatoa nyimbo kama Salome (2016), Iyena (2018), Mwanza (2018), Tetema (2019), Timua Vumbi (2019), Amaboko (2020), Woza (2020), Nitongoze (2022), Yaya (2023) na Nesa Nesa (2024).
Na kati hizo 10, nyimbo nane za mwisho ni zake Rayvanny akimshirikisha Diamond, huku mbili ya mwanzo ni za Diamond akimpa shavu Rayvanny aliyetoka kimuziki na kibao chake, Kwetu (2016) kilichotengenezwa na Laizer.
Hata hivyo, utitiri wa nyimbo hizo kuna eneo umezidiwa na zile chache ambazo Rayvanny alishirikiana na Zuchu, mziwanda wa Malkia wa Taarab nchini, Khadija Kopa aliyeanza kazi ya sanaa mwaka 1990 katika kikundi cha Culture Musical Club, Zanzibar.
Jumatano ya wiki hii video ya wimbo wa Rayvanny, Number One (2020) akiwa na Zuchu imefikia rekodi ya kutazamwa (views) zaidi ya mara milioni 100 katika mtandao wa YouTube ikiwa ni video ya kwanza ya Rayvanny kufanya hivyo.
Video hiyo imefanya vizuri ndani ya muda mfupi na kuzipiku Mwanza (2018) na Tetema (2019) ambazo Rayvanny alimshirikisha Diamond na sasa zikiwa nafasi ya pili na tatu kwa Rayvanny zikiwa zimetazamwa zaidi ya mara milioni 87, na 70.
Kwa matokeo hayo, Rayvanny anaungana na Diamond, Harmonize, Zuchu na Jux ambao wana video zilizofikia namba hizo YouTube, mtandao wa kucheza video ulioanzishwa Februari 14, 2005, huko San Mateo, California nchini Marekani.
Hadi sasa Diamond ndiye msanii pekee Tanzania na Afrika Mashariki mwenye video nyingi zilizotazamwa zaidi ya mara milioni 100 YouTube, anazo tano ambazo ni Yope Remix (2019), Inama (2019), Waah! (2020), Jeje (2020 na Nana (2015).
Huku hao wengine wakiwa na moja moja, video ya Harmonize iliyofanya hivyo ni Kwangwaru (2018), Zuchu ni Sukari (2021) na Jux ni Enjoy (2023), wimbo ulioshinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2023.
Ikumbukwe Rayvanny alifanikiwa kutoa video ya wimbo wake, I Miss You (2022) akiwa tayari amejiondoa WCB Wasafi, ingawa video hiyo ilikuja kwa kuchelewa sana bado imefanya vizuri hadi sasa ikiwa imetazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 33.
Pengine video hiyo ilichelewa kutokana na utaratibu wa Zuchu au WCB Wasafi, unaonekena kumzuia msanii huyo kufanya video za wasanii wa nje ya lebo hiyo waliyomshirikisha katika nyimbo zao.
Mathalani nyimbo za Jux (Nidhibiti), Darassa (Romeo) na Whozu (Attention) ambazo Zuchu kashirikishwa, hakuna hata moja ambayo video yake rasmi imetoka ila zile anazoshirikishwa na wenzake wa WCB Wasafi ndizo video zake zimekuwa zikitoka.
Na ukiachana na Rayvanny, msanii mwingine aliyeshirikiana mara nyingi zaidi na Zuchu ni Diamond, wawili hao wametoa pamoja nyimbo tano ambazo ni Cheche (2020), Litawachoma (2020), Mtasubiri (2022), Raha (2024) na Wale Wale (2024).
Ikumbukwe Rayvanny alijiunga na WCB Wasafi mwaka 2015 akitokea Tip Top Connection alipojiunga tangu 2012 kupitia Babu Tale ila akaishia kurekodi wimbo mmoja tu (Upo Mwenyewe) ambao haukufanya vizuri.
Aprili 2016 ndipo aliachia wimbo wake kwanza (Kwetu) chini ya WCB Wasafi ambao video yake ilishika namba sita kati ya video 15 zilitazamwa zaidi YouTube Tanzania kwa mwaka huo, huku Salome ya Diamond ambayo kashirikishwa ikiongoza.
Baada ya kufanya vizuri na wimbo wake wa pili, Natafuta Kiki (2016) alichaguliwa kuwania tuzo za Africa Entertainment Awards, USA (AEAUSA) kama Best New Artist na Best New Talent, pia aliwania MTV MAMA 2016 kama Best Breakthrough Act.
Mwaka 2017 alishinda tuzo kubwa duniani, BET huko Marekani na hadi sasa ameshinda nyingine kama Zikomo (Zambia) 2022, Afrimma (Marekani) 2022, EAEA (Kenya) 2022, DIAFA (Dubai) 2022 na TMA (Tanzania) 2022 & 2023.
Chini ya WCB Wasafi aliachia EP tatu, Flowers (2020), New Chui (2021) na Flowers II (2022), pamoja na albamu moja, Sound From Africa (2021), na baada ya kujiondoa hapo akatoa EP moja, Unplugged Session (2022) na albamu moja, The Big One (2024).
Ukubwa wa muziki wake ilimuwezesha kuandika rekodi kama msanii wa kwanza Afrika kutumbuiza katika hafla ya utoaji wa tuzo za MTV Europe Music Awards (EMAs) huko Hungary mwaka 2021.
Tetesi za kuondoka WCB Wasafi zilishika kasi baada ya kutoshirikishwa kwenye EP ya Diamond, First of All (2022) iliyotoka ikiwa na nyimbo 10 ambazo ni wasanii wawili tu wa lebo hiyo walipewa shavu ambao ni Mbosso na Zuchu.
Na sasa Rayvanny anamiliki lebo yake, Next Level Music (NLM) aliyoianzisha Aprili 2021 akiwa bado WCB Wasafi, Septemba 2021 ndipo NLM ilimtambulisha msanii wa kwanza, Mac Voice aliyefanya vizuri na EP yake, My Voice (2022).
Leave a Reply