Na Mark Lewis
Inafaa kutambua ni siku zipi za mwezi mwanamke anaweza kushika mimba, pia kutambua kipindi ambacho mwili wa mwanamke uko tayari kushika mimba (Ovulation Period).
Ovulation ni wakati ambao yai lililokua hutoka katika mirija ya ovari katika kizazi cha mwanamke. Katika wakati huu uwezo wako wa kushika mimba ni mkubwa. Kwa kawaida mwanamke huwa na mayai kadhaa katika ovari zake kwa wakati maalumu wa mwezi, ambapo yai kubwa kuliko yote huondoka na kueleka katika tumbo la uzazi kupitia mirija ya ovari.
Ovulation haifuati mpangilio maalumu kati ya ovari katika kila mwezi na haijulikani ni ovari gani itatoa yai kila mwezi. Wakati yai linapotoka huwa na uwezo wa kurutubishwa au kukutana na mbegu ya kiume na kuanza kutengeneza mtoto kwa muda wa masaa 12 hadi 24, kabla halijapoteza uwezo wake.
Iwapo yai litafanikiwa kurutubishwa na mbegu ya kiume kwa wakati maalumu na kujikita katika fuko la uzazi basi matokeo yake ni mimba. Na iwapo halitorutubisha yai hilo pamoja na kuta za kizazi huharibika na kutoka nje ya mwili kama damu ya hedhi.
Utangulizi huo hapo juu utatusaidia kuelewa umuhimu wa kujua idadi ya siku zetu za mzunguko wa mwezi (Menstrual Cycle) na umuhimu wake katika kushika mimba na hata katika magonjwa ya wanawake.
Ili kuelewa vyema siku hizo inatubidi tujue kitu kinachoitwa kalenda ya ovulation au kalenda ya kubeba mimba na pia tujue mzunguko wetu wa hedhi una siku ngapi. Mzunguko wa mwezi ni siku ya kwanza unayopata damu yako ya hedhi hadi siku kabla ya kupata tena hedhi nyingine.
Wataalamu wanatuambia kuwa ili kujua mzunguko huo vyema inatubidi tuchunguze hedhi yetu kwa miezi isiyopungua 6. Lakini kama una haraka na huwezi kuchunguza kwa miezi 6 chunguza kwa miezi mitatu.
Unaweza kufanya hivyo kwa kutumia kalenda ya kawaida na kwa kuziwekea mduara kwa kalamu siku zako za mwezi, yaani siku ya kwanza ya kupata damu ya hedhi hadi siku ya mwisho kabla ya hedhi inayofuata.
Mzunguko wako wa mwezi ni siku ya kwanza ya hedhi hadi siku ya kabla ya kuanza hedhi nyingine. Kwa mfano iwapo umepata siku zako tarehe 02 Julai na ukapata tena siku zako tarehe 29 Julai, mzunguko wako ni wa siku 28.
Kwa kawaida mzunguko wa siku 28 ndio mzunguko wa kawaida kwa wanawake wengi. Lakini kuna baadhi ya wanawake huwa na mzunguko wa chini ya siku 28 na wengine huwa na mzunguko wa hadi siku 35.
Ni vipi utazijua siku zako za ovulation
Wakati wa ovulation katika mzunguko wa mwezi huainishwa na luteal phase, katika mzunguko wako. Unaweza kujua muda wa ovulation katika mzunguko wako wa mwezi kwa kutoa idadi ya siku za luteal phase.
Katika kuhesabu huko utapata mzunguko mfupi na mrefu. Chukua mzunguko mfupi wa mwezi na hesabu idadi ya siku katika mzunguko huo. Toa 18 katika mzunguko huo na utapata idadi fulani.
Halafu anza kuhesabu siku yako ya kwanza ya mzunguko wa hedhi katika mwezi unaofuata kwenda mbele hadi kufikia namba ulioyopata, hivyo utaweza kupata siku ambayo una uwezekano mkubwa wa kubeba mimba.
Kwa mfano mzunguko wako mfupi ni siku 29, unatoa 18 katika 29 na unapata 11. Iwapo siku yako ya kuanza hedhi mwezi ujao ni Julai 3, ongeza siku 11 kuanzia siku hiyo. Hivyo siku ambayo una uwezekano mkubwa wa kubeba mimba itakuwa Julai 14.
Halafu chunguza idadi ya siku za mzunguko wako mrefu wa hedhi. Toa siku 11 kutoka katika idadi ya siku za mzunguko huo na utapata namba fulani.
Halafu tena anza kuhesabu katika mzunguko wako ujao wa hedhi kwenda mbele hadi kufikia siku ambayo una uwezekano wa kupata mimba.
Kwa mfano iwapo mzunguko wako mrefu ni siku 31, toa 11 katika mzunguko huo na utapata 20. Iwapo hedhi yako ijayo inaanza tarehe 3 Julai, ongeza siku 20 kuanzia siku hiyo na tarehe 23 Julai itakuwa siku yako ambayo una uwezekano mkubwa wa kubeba mimba.
Kwa utaratibu huo utakuwa umepata kipindi cha kati ya Julai 14 hadi Julai 23 ambacho ni siku ambazo una uwezekano mkubwa wa kubeba mimba.
Ovulation huweza kubadilika kidogo katika mzunguko wako wa hedhi kwa sababu ovulation huweza kucheleweshwa na sababu mbalimbali kama vile wasiwasi au fikra nyingi, ugonjwa, lishe au kufanya mazoezi.
Vipi kipindi cha ovulation kinaainisha siku za kubeba mimba?
Kipindi cha kubeba mimba huanza siku 4 hadi 5 kabla ya ovulation, na humalizika masaa 24 hadi 48 baada ya hapo hii ni kwa sababu muda wa ovulation huweza kuchelewa au kuwahi kutokana na sababu mbalimbali.
Pia kwa sababu mbegu ya kiume huwa na uhai kwa siku 4 hadi 5 na yai huweza kuishi kwa masaa 24 hadi 48 baada ya kuingia katika tumbo la uzazi. Hivyo kwa kujua siku hizo humsaidia mwanamke kufahamu kipindi chake cha ovulation kimewadia na hivyo kuweza kukukutana na mumewe au mwenza wake wakati huo ili aweze kubeba mimba. Pia kujua kipindi hiki na masuala mengineyo kama hali ya joto la mwili ilivyo wakati wa ovulation huweza kutumika kama njia ya kuzuia mimba. Yaani kutojamiiana katika kipindi hiki huweza kumzuia mtu asipate mimba.
Kwa kuwa kipindi cha ovulation hakina tarehe maalum na ni siku kadhaa, zipo baadhi ya alama za mwili zinazosaidia kutambua ni wakati gani ovulation imewadia.
Ni alama gani za mwili wako zitakufahamisha ovulation imewadia?
Alama hizo za ovulation si ngumu kuzitambua, iwapo utafahamu unatafuta alama gani. Kuna baadhi ya alama za mwili zinazokutahadharisha kwamba ovulation iko njiani, hivyo kuweza kukusaidia kupanga vyema muda wa kujamiiana kwa ajili ya kupata mimba.
Alama nyinginezo zinakufahamisha kwamba ovulation imewadia au imeshapita. Ingawa alama hizo ziko nyingi na zifuatazo ni baadhi ya alama.
- Mabadiliko ya joto lako la Mwili
Tunaweza kusema kuwa Joto lako la mwili ndio alama maarufu inayotumiwa na wanawake wengi ili kufahamisha kwamba ovulation imewadia pale wanapotaka kubeba mimba.
Hii ni kwa sababu joto lako la mwili huongezeka kwa kiasi kidogo na huendelea kuongezeka baada ya ovulation. Ongezeko hilo la joto husababishwa na homoni ya progesterone, ambayo huongezeka sana punde baada ya ovulation. Kwa kujipima joto lako la mwili na kuandika chati ya mabadiliko hayo unaweza kufahamu ongezeko hilo la joto lako la mwili.
Ingawa njia hii haianishi moja kwa moja kuwa ovulation imewadia, lakini joto la mwili huongezeka kidogo kabla yakipindi hicho na huongezeka kwa kwa degree 0.4 hadi 0.6 baada tu ya kumalizika ovulation. Kuongezeka joto kwa kiasi kikubwa baada ya ovulation huendelea hadi siku utakayopata siku zako ambapo hupungua na mzunguko wako wa mwezi huanza tena.
- Mabadiliko ya majimaji ya ukeni
Wakati ovulation inakaribia, majimaji ya ukeni hubadilika pia kwa kiasi na hali. Ikiwa hakuna ovulation majimaji ya ukeni huwa yanayonata au kama ute au hukosekana kabisa.
Wakati ovulation inakaribia majimaji ya ukeni huongezeka na huwa katika hali ya kuwa na rangi nyeupe kama ya yai bichi. Iwapo utapima kwa vidole vyako huvutika kwa inchi au zaidi kati ya vidole vyako. Njia hii huhesabiwa kuwa yenye uhakika zaidi.
- Ongezeko la matamanio
Inaonekana kuwa maumbile nayo hutusaidia kujua ni siku gani tunaweza kubeba mimba! Wataalamu wameonyesha kwamba wanawake wanapokuwa katika siku zenye uwezekano mkubwa wa kupata mimba, matamanio yao ya huongezeka. Hizo ni siku chache kabla ya kujiri ovulation, ambapo ndio wakati unaofaa wa kujamiiana iwapo unataka kubeba mimba.
- Mabadiliko ya Ukeni:
Kama ambavyo majimaji ya ukeni yanavyobadilika wakati wa Ovulation, uke nao hubadilika wakati wa kukaribia Ovulation. Wakati huo uke husogea mbele, huwa laini na hufunguka zaidi.
- Maumivu kidogo katika matiti:
Baadhi ya wanawake wakati wanapokaribia ovulation au baada ya hapo matiti yao huwa na maumivu kidogo. Suala hili huhusiana na mabadiliko ya homini mwili ambazo hujitayarisha kwa ajili ya mimba.
Hata hivyo njia hii sio yenye kutegemewa sana kwani maumivu ya matiti huweza kusababishwa na masuala mengine. Pia maumivu ya matiti hutokea kabla ya hedhi au baada ya kutumia baadhi ya dawa za kusaidia uzazi.
Alama nyinginezo
Baadhi ya wanawake huhisi maumivu kidogo ya tumbo. Maumivu hayo kwa kawaida hutokea upande ule yai linapotoka yaani upande wa ovulation. Maumivu hayo hutokana na mwendo wa yai wakati linapopenya kwenye mirija. Maumivu hayo si ya kuendelea na wala si makubwa na huisha haraka.
Kuna baadhi ya alama kama vile baadhi ya wanawake huhisi kichefuchefu, gesi tumboni, kukojoa mara kwa mara na maumivu wakati wa kujamiina, hali ambayo haitokei kwa watu wengi.
Pia kuna baadhi ya vifaa ambavyo huweza kukusaidia kujua wakati wako wa ovuation umewada, vifaa hivyo hujulikana kama ‘’Ovulation Kit”
Iwapo hutoona alama zozote za Ovulation au iwapo siku zako za mwezi hazina mpangilio maalum, ni bora umuone daktari ambaye atakupa msaada wa haraka au kugundua tatizo ulilo nalo.
Leave a Reply