Ilikuwa ni siku ya Jumamosi, na ndio nilikuwa nimetoka Benki kuchukua mshahara wangu wa kwanza baada ya kusota kwa takriban mwaka mmoja bila ajira. Kwa mwaka huo mmoja niliokuwa nje ya ajira baada ya kupigwa kile kinachoitwa Ridandansi, nilikuwa nimepigika kweli kweli kwa msoto. Nilikuwa nimekomba akaunti yangu yote kwani kwa mahesabu yangu ya haraka haraka, nilikuwa nina mahitaji mengi pale nyumbani ya kutekeleza achilia mbali madeni niliyokopa kwa marafiki zangu na kwenye duka la Mangi jirani na ninapoishi.
Ama kweli ibilisi ni ibilisi tu, nikiwa ndani ya dala dala nilimkumbuka mwanamke mmoja niliyekutana naye juma lililopita wakati nikitokea Morogoro Kikazi, huyu mwanamke alikuwa ameumbika hasa, alikuwa maji ya kunde na amejaaliwa kweli kuwa na kalio kubwa kama mtungi na kiuno kama cha nyigu. Nilikuwa nimekaa naye siti moja na alionekana kuwa mcheshi sana kwangu. Tuliongea mambo mengi sana na alinijulisha kwamba anaye mchumba lakini kuna mgogoro huko kwa wakwe zake watarajiwa, kwani hawakutaka kijana wao amuoe kwa sababu ya tofauti za kidini. Yule kijana ni Mkristo mlokole na huyu dada ni Mwislamu. Na mimi sikulaza damu kama kawaida yangu nikajikuta namtupia nyavu zangu, na bila kusita yule mwanamke alinasa sawia.
Alinitajia jina lake kuwa anaitwa Saniah na anaishi Mbezi ya Kimara na wazazi wake lakini anafanya kazi kwenye taasisi moja ya UN. Lakini hakunitajia taasisi hiyo. Tulikubaliana tukutane juma lijalo, na nilipanga iwe hivyo kwa sababu nilijuwa kuwa kipindi hicho nitakuwa nimepokea mshahara. Alinidadisi kama ninafanyia wapi na mie kwa kutaka ujiko nilimpiga fix kwamba mimi ni consultant wa kuchunguza vyura wa kule Kihansi kwa ushirikiano na Serikali ya Marekani na nilimdanganya kwamba wiki ijayo nitasafiri kwenda nchini humo kuwasilisha ripoti yangu. Kumbe mimi ni fundi mchundo ambaye niko choka mbaya.
Ni wiki hiyo nilipopata mshahara Wangu ndipo nikamkumbuka mwanamke yule. Nilimpigia simu na baada ya kusalimiana nilimuomba tuonane kama tuliyoahidiana, alinijulisha kwamba mchumba wake anatarajia kurudi siku ile kutokea nchini Rwanda alikoenda kikazi hivyo asingeweza kuungana na mimi. Nilijitaidi kumshawishi amdanganye huyo mchumba wake kuwa ana dharura na asingeweza kuonana naye lakini akakataa akidai kwamba walikubaliana ampokee. Ilibidi nikubaliane naye. Lakini muda mfupi baadae alinipigia simu na kunijuza kwamba mchumba wake ameahirisha safari na atarudi siku inayofuata, alinitaka tukutane kwenye Hoteli moja maarufu ya nyota tano iliyoko katikati ya jiji hili la Dar. Nilipanda daladala na kugeuza kuelekea mjini kwani mwanaume tamaa ya ngono ilinitawala na nilikuwa nimepania kweli kumfaidi mwanamke Yule aliyeumbika hasa.
Niliwahi kufika kabla yake na haukupita muda mrefu na yeye akafika, lakini kabla ya kukaa aliniomba nimpe shilingi elfu ishirini akamlipe dereva taxi aliyemleta. Nilimpa zile hela akaenda kumlipa dereva taxi kisha akarudi na kuungana na mimi. Alinikuta nikiwa nakunywa Bia yangu, lakini na yeye akaagiza Gordons Gin na soda aina ya Tonic Water na barafu. Mie pale nilipokaa nilianza kupiga mahesabu ya gharama za vile vinywaji........maana bei za hotel za nyota tano ni pasua kichwakweli.
Haukupita muda yule mwanamke akaniambia, “Vipi honey hatuli, mwenzio nina njaa,” Mh, mie pale mapigo ya moyo yakaanza kwenda kasi, nikajua leo nimelivaa Gubeli, lakini kwa tamaa yangu ya ngono , nikajisemea moyoni, “ngoja tukale kisha niondoke naye akanilipe alivyokula.” Tuliingia kwenye mghahawa wa ile Hoteli na tulipoletewa Menu, jasho lilinitoka, bei ya vyakula ilikuwa iko juu kweli. Lakini nilijipa moyo kwani nilikuwa na mshahara wangu mfukoni.
Tulitoa oda ya vyakula vyetu , na wakati tunasubiri vyakula vije mwenzangu akaagiza chupa ya mvinyo, ambayo bei yake ilikuwa si kidogo... Mweh! Mie nikajua leo nimepatikana. Ingawa alikuwa akiongea na mimi kwa bashasha, lakini akili yangu ilikuwa mbali kweli nilikuwa nawaza nitamwambia nini mke wangu. Nitamwambia mshahara nimeupeleka wapi? Nadhani alihisi hali niliyokuwa nayo. “Honey you seems to be uncomfortable, what is wrong?” aliniuliza. Kwa kujifaragua nilimwambia ninawaza kama ripoti yangu itakubaliwa na serikali ya Marekani kwani ni mradi mkubwa sana ambao una thamani ya mamilioni ya dola. Lakini moyoni nilikuwa naumia kweli kwa gharama anazonipa.
Haukupita muda chakula chetu kililetwa na baada ya kula kabla bili haijaletwa simu yake iliita na alionekana kushtuka, aliipokea na nilisikia sauti ya kiume upande wa pili, aliniomba radhi na kusogea pembani, nadhani ili nisisikie anaongea nini na huyo mwanaume. Nilitulia pale kwenye kiti, nikimsubiri arudi ili tuondoke nikajivinjari naye kabla ya kurudi nyumbani kwangu.
Alirudi na kunibusu shavuni na kuchukua mkoba wake kisha akaniambia mchumba wake amekuja na amemwambia wakutane nyumbani, nilipomuuliza, mbona aliniambia kuwa ameahirisha safari na asingekuja siku hiyo. Akanijibu kuwa mpenzi wake amezoea kum-surprise. Aliniomba radhi na kuniahidi kukutana na mimi siku inayofuata, akaniambia atanijulisha kwa simu tukutane wapi, hata hivyo aliniomba nimpe tena elfu ishirini ya taxi, ili amuwahi mchumba wake, nilizitoa zile hela huku roho ikiniuma. Aliondoka na kuniachia msala wa bili ya kulipa. Nilijikuta nikitoka pale Hotelini nikiwa nimebakiwa na shilingi elfu arobaini tu mfukoni. Nilitembea kuelekea kituoni huku nikiwa na mawazo kichwani. Nashukuru nilifika nyumbani salama, maana kwa jinsi nilivyokuwa na mawazo, nadhani ningegongwa na gari au boda boda.
Nilifika nyumbani na kujitupa kitandani. Nilimwambia mke wangu sijisikii vizuri na sitakula kwani nahitaji kupumzika.
Niliamka asubuhi nikiwa bado na lindi la mawazo kichwani. Nitamwambia mke wangu mshahara umekwenda wapi, yale madeni ninayodaiwa, nitawaambia nini wanaonidai? Niliwaza. Nilisimama dirishani nikichungulia nje, wanangu walikuwa walikuwa wakicheza na wenzao kwa furaha huko nje lakini walikuwa wamevaa viguo vilivyowaacha makalio yao yote nje kwa kuchakaa...
Niliwahurumia wanangu, na nilijikuta nikibubujikwa na machozi kwa majuto......Ama kweli majuto ni mjukuu...............
Leave a Reply