Yajue madhaifu matano (5) yanayodidimiza mahusiano

Yajue madhaifu matano (5) yanayodidimiza mahusiano

Mara nyingi uwapo katika mahusiano ya kimapenzi elewa na tambua ya kwamba kama hautakuwa makini haijalishi unampenda mpenzi wako kiasi gani ipo siku yatakufa.

Siombei jambo hilo litokee ila nakwambia ukweli ya kwamba kama hautakuwa makini na mahusiano yako ni lazima mahusiano hayo yatakufa, nasema hivyo nikiwa na ushahidi wa kutosha kwa sababu wanaojenga na kubomoa mahusiano ya kimapenzi ni wapenzi wenyewe.

Na upo usemi usemao ajengaye hubomoa pia, Hata katika vitabu vya dini vinasema ya kwamba mwanamke mjinga huibomoa ndoa yake kwa mikono yake mwenyewe, si mwanamke bali hata mwanaume naye huibomoa ndoa au mahusiano yake kwa mikono yake mwenyewe.

Ili kudhihirisha ukweli wa maneno hayo leo katika Makala mwanasaikolojia Neema Mwamkina akizungumza na MwananchiScoop ametuletea madhaifu matano yanayoweza kudidimiza mahusiano.

Neema alisema moja ya madhaifu hayo ni mchangango mkubwa kuhusu maana ya mahusiano, mapenzi na ndoa.

Alisema kunaweza kuwepo ndoa, lakini yasiwepo mahusiano wala mapenzi, anafafanua kwa kusema inaweza kuonekana kama inachanganya kidogo, lakini ndio ukweli wenyewe. 

“Ndoa ni namna tuu ambayo wawili walio kwenye mahusiano wanaamua kuwataarifu rasmi watu wengine kuwa wao wapo rasmi katika mahusiano.Ndoa ni kiapo mbele ya watu wengine , na ni namna ya kutaka kumuhakikishia mwenza wako kuwa endapo kiapo hicho kitatokea kuvunjika, basi unakubali rasmi kuwajibika kwa mujibu wa taratibu zilizopo za ndoa husika.

“Ikiwemo kukubali kuitwa kwenye mabaraza ya usuluhishi, kugawana mali, n.k. Na kwa upande wa kiroho, inabeba maana zaidi kuwa unaweka kiapo kwa Mungu wako kuwa utalinda mahusiano yako na huyo unayemchagua,” alisema Neema.

Hivyo basi, Neema alisema ndoa haijengi mahusiano wala mapenzi bali kiuhalisi inabidi kwanza yawepo mahusiano na mapenzi kisha ndio kiapo kifanyike, kwani kinyume cha hivyo ni kuwa unakula kiapo ‘feki’.

“Ndio maana basi, ni muhimu kwa wapenzi kutambua kweli kama wanahitajiana, kuwa kwenye mahusiano na kutafakari kwa uhuru kama kweli wanataka kuweka kiapo rasmi cha kuwa pamoja.

Kutumia ndoa kama kinga ya kuhakikisha mahusiano yako yanadumu ni maamuzi magumu ambayo pengine yanaweza yasilete faida hapo baadae,” alisema Neema.

Alisema madhaifu ya pili yanayodidimiza mahusiano ni kuyumbishwa ana matarajio yasiyo halisi.

Anafafanua kuwa kabla hata ya kuingia katika mahusiano na hatimaye ndoa watu wengi huwa na matarajio binafsi ya kimaisha.

“Matarajio haya yanajumuisha vile tunavyotaka sie wenyewe kuwa hapo baadae, pamoja na matarajio ya vile tunavyotaka wenza wetu wawe.

“Hata hivyo katika hali halisi tunajikuta sisi wenyewe hatuwezi kujibadilisha au kujiweka kwa usahihi vile tunavyotamani kuwa (kwa sababu kwa kila tunachojaribu kufanya kuwa bora, tunajikuta bado tuna madhaifu mawili matatu),” alisema Neema

Alisema pamoja na ukweli huu, baadhi ya watu wanajikuta wapo kwenye matarajio ya kuwafanya wenza wao wawe watu wa aina fulani.

Anaendelea kusema kwakuwa kiasili binadamu ni kiumbe huru, wanajikuta wenza wao nao wapo ‘busy’ kutimiza ndoto za vile wanavyotamani kuwa iwe kimavazi, aina ya marafiki, utafutaji wa kazi, kujiendeleza kimasomo, aina ya mali za kununua, hata kufikiria tofauti aina ya maisha wanayotaka muishi.

“Matokeo yake ukinzani huu wa matarajio ni mkanganyiko wa mgongano wa mawazo kati ya wawili nyie, na mwanzo wa vita ya chini kwa chini ya nguvu ya maamuzi katika mahusiano yenu,” alisema.

Anafunguka kwa kusema madhaifu mengine, kuweza kumbadili tabia mwenza wako.

“Mojawapo ya jambo ambalo hufanywa na wengi walio katika mahusiano ni kuwa na ‘tamaa’ ya kutaka kumbadili tabia fulani mwenza wake.

“Hata hivyo ‘tamaa’ hii ni sehemu ya yale tunayoyaita matarajio yasiyo halisi, kwani tabia ya mtu hujengwa na mambo mengi sana, ikijumuisha aina ya makuzi, aina ya mfumo wa imani mtu anaouamini, aina ya marafiki alio nao, uwezo wake wa kujiamini katika kubadili tabia kwani wengine wameshakata tamaa kuwa hawawezi kukata tamaa, na zaidi sana, mabadiliko ya tabia huhitaji mfumo endelevu na wenye kusoma vema asili ya tabia ili kuweza kuirekebisha,” alisema.

Hata hivyo alisema watu wengi kwenye mahusiano, hutegemea ‘mapenzi’au vitisho tuu kama vile ‘nitakuacha mie ’, kama sababu ya kumfanya mtu abadilike kitabia.

“Udhaifu wetu katika kutambua asili ya tabia ya mtu husika na mbinu za kisayansi za kubadili tabia hufanya zoezi la kubadilishana tabia kuwa gumu na pengine lisilowezakana,” alisema

Mbali na hayo, Neema alisema kuvumilia ndio kuonyesha upendo na ndio kudumisha mahusiano.

Alisema hiyo ni aina nyingine ya matarajio ambayo sio halisi kwani kiukweli kila mtu analo jukumu la kufanya bidii kuwa mtu mwema, hivyo hauhitaji kubeba ‘uzembe’ wa mwingine kwa kisingizio tu cha kuwa unaonyesha upendo hususani pale ambapo ni kwa uzembe au kutokujali kwake mwenza husika amefanya jambo fulani.

“Kwa jinsi kasumba hii ilivyo enea sio ajabu kukuta mtu akifanya mambo mabaya kwa mwenza wake kwa makusudi ili tuu eti apime kama kweli mwenza wake ni mvumilivu.

“Kumbuka hapa hatumaanishi kuwa kusamehe ni kosa, hapana, kusameheana ni muhimu, lakini sio kwamba ni muhimu tu katika mapenzi. Kusameheana ni jambo la asili, na tunapaswa kusameheana kwa mambo mengi nje hata ya mahusiano,” alisema na kuongeza 

“Tunachosema ni kuwa kuna kasumba ya baadhi yetu kuona kuwa wanayo ‘haki’ ya msingi ya kukosea eti tuu kwakuwa mwenza wake analazimika kusamehe ili kuonyesha kweli anao upendo wa dhati,” alisema.

Alisema kasumba hiyo ya kutarajia aina ya pekee ya kusamehewa na kuvumiliwa kwa kisingizio cha kuwa upo kwenye mapenzi na mwenza wako, hurudisha nyuma maendeleo ya mahusiano.

“Tambua kuwa mwenzi wako nae ni binadamu na kumbuka anayo matarajio mengine ya maisha, isitoshe na yeye anahitaji upendo na kujaliwa na wewe, hivyo kutarajia kwako kusamehewa na kuvumiliwa kuna mnyima haki mwenza wako. Hatimaye kutegema kwako kusamehewa kila wakati, kunamfanya mwenza wako atilie mashaka upendo wako kwake,” alisema

Mwisho Neema alisema Uaminifu, Upendo na Kudumu kwa mahusiano ni miongoni mwa madhaifu ya kudidimiza mahusiano kama hazitafuatwa.

Alisema pamoja na ukweli kuwa mwenza wako anatarajia utakuwa muanifu kwake, elewa kuwa kuwa mwaminifu pekee katika mahusiano yako sio tiketi ya kudumu kwa mahusiano yenu.

Anaeleza kwakuwa watu wanaingia kwenye mahusiano sio tu kwa kuwa wanataka kuwa na mtu mmoja muaminifu bali wana mahitaji mengine wanayohitaji.

“Zungumza na mwenza wako, fanya utafiti wako binafsi kuhusu mpenzi wako ujue mambo mengine anayohitaji toka kwako. Pia msikilize anapokutaka urekebishe mambo kadhaa au ufanye mambo fulani.

“Inapendeza pale unapomfanyia mtu mambo yanayompendezesha kwa kuwa hivyo ndivyo anavyotaka, sio kwakuwa tuu wewe unadhani kufanya hivyo kutampendezesha mhusika,” alisema

 

.

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags