Wimbo wa Oscar marufuku kwenye vyombo vya usafiri

Wimbo wa Oscar marufuku kwenye vyombo vya usafiri

Mtangazaji na msanii mpya wa Hiphop nchini, Oscar Oscar leo Mei 22, 2025, ameitikia wito katika ofisi za Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) ambapo aliitwaa baada ya kuachia wimbo wake wa kwanza 'Niombeeni' huku akipewa mwongozo maeneo ambayo utasisikia.

Basata imetoa mwongozo kwamba wimbo huo utapigwa kwenye kumbi za starehe, katiks vyombo vya habari utapigwa kuanzia saa sita usiku. Pia hautapigwa kwenye vyombo vya usifiri wa umma, kwenye matamasha kama kuna watoto.
Baada ya kikao na baraza hilo, Oscar Oscar amezungumza na wanahabari na kusema kwake ni furaha kuitwa Basata kwani huwezi kuwa msanii mkubwa nchini kama hujawahi kuitwa Basata.


"Hauwezi ukawa msanii mkubwa bila kuitwa Basata, Kwasababu Basata kwenye sanaa ndio nyumbani. Kwa bahati mbaya watu wanamtazamo kwamba ukiitwa Basata umeitwa kwenye mambo magumu tu.

"Lakini hapa kuna vitu vingi sana vya kujifunza na elimu ya bure ambapo huku mtaani unaweza kuilipia kwa hiyo kama haujawahi kuitwa Basata bado hujawa msanii maana yake hauna mabaya, hauna mazuri sasa upo kwenye sanaa unafanya kitu gani," amesema Oscar Oscar.

Amesema Baada ya kuitwa Basata ameanza usajili na kutambulika rasmi kama msanii wa muziki nchini.

"Nimetambulika rasmi sasa kama msanii na nimekuwa nikizungumza kuwa mimi siyo Underground, mimi ni msanii mpya Superstar. Kwa hiyo nimeitwa nyumbani na kuanzia sasa chochote kile ambacho nitakifanya ni lazima kipitie kwenye miongozo ya Basata, kuja hapa ni kama nimekuja kuongeza ‘hasira’ ya kufanya zaidi," mesema Oscar Oscar.

Hata hivyo, amekanusha madai ya watu wanaosema wimbo huo umeandikwa na msanii Baba Levo, akisema hawezi kumuandikia.

"Babalevo hajaandika wimbo huo, niambie kuna msanii gani mpya nchini ndani ya siku moja akatazamwa zaidi ya mara laki moja kwenye YouTube. Ndani ya masaa 24 hii ni rekodi ambao imewekwa na mzee wa Kariuwa ambaye anasikika kwa mara ya kwanza na mgongoni kwake hakuna lebo," amesema Oscar Oscar.

Amesema wimbo ‘Niombeeni’ ni wa kutubu kwa mwanadamu yeyote ambaye ametenda makosa katika jamii au kwa Mungu wake na hakuwa na dhumuni la kwenda kinyume na maadili ya kitanzania.

"Huu ni wimbo wa toba kwa mwanadamu ambaye amefanya makosa mengi ambayo hayapendezi katika jamii hayampendezi pia mwenyezi Mungu na wimbo umekusudia kumpa nafasi mtu ambaye amepotoka katika jamii kwa kutenda dhambi sana bado ipo fursa ya kwenda kutubu ndio maana ukisiliza kwenye kiitikio wamefajwa viongozi mbalimbali wa dini," amesema Oscar.

Katibu Mtendaji Mkuu wa Basata, Kedmon Mpana amemkaribisha Oscar katika sanaa ya muziki na kumpa mwongozo wa maadili ya sanaa hiyo.

"Nikukaribishe kwenye sanaa lakini pia nadhani wimbo wako watu hawajaupokea kama ulivyoutunga. Wimbo wako mpaka ufike kwenye kiitikio ndio mtu anaelewa ujumbe, lakini unapoanza unaanza na maneno ambayo hayajazoeleka, nadhani ufuate ushauri watu huanza vipi, tunakukaribisha kwenye sanaa piga kazi lakini hakikisha usajili wako umekamilika," amesema Mapana.

Hata hivyo, Basata wametoa mwongozo namna ya wimbo huo utakavyopigwa sehemu mbalimbali kwa kuzingatia umri kuanzia miaka 18 na kuendelea.

"Wimbo umewekewa umri wa watu kuusikiliza ambao ni kuanzia miaka 18 na kuendelea na tumeshamwambia Oscar Oscar, wimbo huo utapigwa kwenye kumbi za starehe, kwenye vyombo vya habari utapigwa kuanzia saa sita usiku. Hautapigwa kwenye vyombo vya usifiri wa umma, kwenye matamasha kama kuna watoto," amesema Mapana.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags