Na Michael Anderson
Ni kipindi cha mwanzo wa mwaka. Hiki ni kipindi ambacho watu wengi wanaweka malengo ya mwaka mpya. Ni kipindi ambacho watu wanatathimini malengo yao ya mwaka uliopita na kujipanga kwa kuweka malengo ya mwaka mwingine mpya.
Rafiki yangu kama umekuwa na tabia ya kuweka malengo ya mwaka mzima nakupongeza sana. Hiyo ni hatua kubwa umepiga. Lakini kama umekuwa huweki malengo ya mwaka, nakushauri na kukushawishi uanze kuweka malengo kila mwaka, hata kama utashindwa kuyafikia yote, nakuhakikishia utapiga hatua kubwa mno kwenye safari yako ya mafanikio.
Huwezi kufikia ndoto yako bila kuwa na malengo. Kama kweli ulikuwa hauna tabia ya kuweka malengo na unataka kufikia ndoto yako kubwa, anza kuweka malengo kwa ajili ya mwaka ujao.
Kuna sifa nne za malengo ambazo watu wengi wanapoweka malengo hawazifuati, na hii imekuwa ni moja ya chanzo kikubwa cha kutofikia malengo tunayojiwekea. Leo naomba nikushirikishe sifa hizi nne za malengo ambazo tunatakiwa kuzizingatia kipindi tunaweka malengo.
ZINGATIA HAYA KUWEKA MALENGO YAKO VIZURI
1.Malengo lazima yawe makubwa (Goals must be big)
Watu wengi wanapoweka malengo wanajihurumia, kwa hiyo wanaweka malengo madogo ambayo hayatawasumbua kuyafikia. Wanaweka malengo ambayo hayawapi hamasa kwenda hatua ya ziada hata kidogo.
2.Malengo lazima yawe ya muda mrefu (Goals must be long-range)
Malengo yanatakiwa yawe ya muda mrefu, angalau mwaka mmoja. Unapoweka malengo ya muda mfupi, changamoto zinapokuja kuna uwezekano mkubwa wa kukata tamaa. Matatizo ya kifamilia, magonjwa, ajali, au tatizo lolote ambalo huwezi kulitatua kwa kipindi kifupi, linapokuja ni rahisi sana kukata tamaa na kuachana na malengo yako kama ni ya muda mfupi.
3.Malengo lazima yawe maalumu au mahususi (Goals must be specific)
Epuka kuweka malengo ya kiujumla tu. Malengo yako lazima yawe maalumu. Kwa mfano; unapoweka lengo la kujenga nyumba nzuri, hakikisha unajua unataka nyumba ya vyumba vingapi, urefu gani, rangi gani, ukubwa gani, aina gani, mahali gani n.k.
Malengo kama; kutengeneza pesa nyingi, kuwa na kazi yenye mshahara mkubwa, kuwa mke au mme bora, kuwa mwanafunzi bora, kuwa mtu bora, ni malengo ambayo yako kiujumla sana.
4.Malengo lazima yafanywe kila siku (Goals must be daily)
Mafanikio ni muunganiko wa vitu vidogovidogo vinavyofanywa kila siku. Kuna methali moja inasema haba na haba hujaza kibaba. Malengo yako lazima yawe ya kila siku. Isipite siku bila kufanya chochote kwa ajili ya malengo, hata kama ni kitu kidogo. Mambo mazuri na makubwa hayaji ghafla, ni muunganiko wa vitu vidogovidogo utakavyofanya kila siku.
CHUKUA HII !
Tafakari njema rafiki yangu. Nikutakie sikukuu njema kwa wewe ambaye unasherehekea leo. Tufurahi kwa amani. MWAKA 2025 UKAWE WA MAFANIKIO MENGI SANA KWAKO
HAKUNA LISILOWEZEKANA KAMA UKIAMINI. HATA WEWE UNAWEZA. KUNA UWEZO MKUBWA NDANI YAKO.
Leave a Reply