Wasanii wajitokeza kumuaga Gardner

Wasanii wajitokeza kumuaga Gardner

Wasanii mbalimbali wamejitokeza katika viwanja vya Leaders Club leo Aprili 22,2024, kumuaga marehemu Gardner Habash aliyekuwa mtangazaji wa Clouds Media katika kipindi cha Jahazi.

Gardner alifariki Aprili 20,2024 katika Hospitali ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alipokuwa anapatiwa matibabu.

Baada ya mwili huo kuagwa utapelekwa uwanja wa ndege kwa safari ya kuelekea kijijini kwao Wilayani Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika kesho Aprili 23,2024.

Wasanii ambao wamejitokeza ni pamoja na Temba, Monalisa, Joh Makini, Barnaba, Chege, Madee, Ferooz na wengineo. Aidha wasanii hao wamejumuika katika tukio hilo kutokana na mtangazaji huyo kuinua baadhi ya vipaji vya wasanii wa Bongo Fleva nchini.

Aliyekuwa mke wa Gardner Habash, Lady Jaydee amezungumza mchache msibani hapo na kuwashukuru waliofika kumsindikiza Gardner kwenye safari yake ya mwisho.

“Sijui hata kitu cha kuzungumza, nianzie wapi kwa sababu sikuwa nimejipanga na wala sikuwa nimetegemea kama tutakuwa hapa kumuaga mpendwa wetu, lakini nishukuru tu kwa wote waliofika kushiriki na tuendelee kumuombea apumzike kwa amani”. Amesema

Kwa upande wake mwigizaji Stive Nyerere, amesema kuwa msiba wa Gardner ni tafakari kwa watu wengine.

“Msiba huu siyo wenu nyinyi pekee, ni msiba wa Watanzania wote wakati tunajitafakari katika msiba huu wa Gardner G Habash, jitafakari na wewe kama unaweza kuzikwa na watu kama hawa, Gardner alitengeneza maisha yake, hakuwa mkubwa sana wala mdogo sanalakini alikuwa kimbilio la watu na ndiyo maana wamejitokeza kutoka kila mahali na hii ndiyo maana ya kuishi na watu vizuri, jitafakari wewe uliyopo je ukidondoka sisi tutakuja”.  Steve Nyerere.

Aidha aliwaomba wasanii na mastaa kuishi vizuri na watu pamoja na kujenga mahusiano mema na watu ili pindi upatapo matatizo waweze kukimbiliwa.

Hata hivyo Joh Makini amesema ni ngumu kueleza mafanikio ya muziki wa Bongo Fleva bila ya kumtaja Gardner.

“Gardner hakuweza kujielezea mwenyewe bila kuuelezea mapenzi yake kwenye muziki wa Bongo Fleva, hivyo basi leo hii hatuwezi kuelezea mafanikio ya kiwanda hichi cha muziki wa Bongo Fleva bila kutaja jina la Captain Gardner G Habash, Mwenyezi Mungu ampumzishe mahala pema peponi”. Amesema Joh Makini

Ikumbukwe kuwa Gardner ndiye mtangazaji aliyefufua na kunyanyua kipaji cha mwanamuziki Chege Chigunda, baada ya kuusimamia wimbo wa msanii huyo uliyemfanya ajulikane uitwao ‘Twenzetu’.
.
.
..
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags