Waitara avitaka vyuo vya ufundi kwenda kujifunza NIT jinsi ya kujiendesha

Waitara avitaka vyuo vya ufundi kwenda kujifunza NIT jinsi ya kujiendesha

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara amevitaka vyuo vya ufundi nchini kwenda kujifunza jinsi ya kujiendesha katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).

Aidha Waitara amekipongeza chuo hicho kwa namna kilivyojipanga vema kutoa wataalamu bora katika sekta ya usafirishaji.

Waitara ameyasema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara katika chuo hicho kwa lengo la kuangalia na kujadili maendeleo ya NIT.

Amesema NIT kinapaswa kuwa chuo cha Serikali kwani kimejipanga vema katika kutoa elimu bora itakayozalisha wataalamu wataokwenda kusimamia miradi ya kisasa ya usafirishaji hapa nchini.

“Tangu nilipoteuliwa kushika nyadhifa hii nimetembelea taasisi nyingi za ujenzi na uchukuzi ambazo zipo 25 NIT ni sehemu yao, ila niseme tu chuo hiki kinafanya kazi kubwa na kimejipanga kwa kila kitu.

“Nilienda Kigoma Chuo cha Hali ya Hewa ila sikuelewa taarifa niliyopewa kwani nilijua nitakuta kitu kikubwa, vitu vya kisasa na watu wamejipanga hata hivyo ilikuwa ni tofauti, nimeenda Chuo cha Bandari na kwenyewe sikulidhishwa ila nimekuja hapa NIT nimeona namna mlivyojipanga sasa hiki ndicho chuo na kinapaswa kuwa cha serikali,” amesema

Amesema anakipongeza chuo hicho kwa kufanikisha ununuaji wa mitambo ya kisasa kwa juhudi zao binafsi na kuwataka kuendelea na hali hiyo.

“Chuo hiki hakijapata fedha kwa muda mrefu sana nadhani mwaka huu ndo kimepata Milioni 500 lakini kupitia mapato ya ndani kimeweza kukusanya Bilioni moja ni mara mbili ya fedha ambazo Serikali imetoa, na kiukweli tumetoa fedha baada ya kuona Mkuu wa Chuo na wenzake wanafanya kazi kubwa iliyotukuka,” amesema

Naye Mkuu wa Chuo cha NIT, Profesa Zacharia Mganilwa amesema chuo hicho kimejipanga kutoa wataalamu bora katika sekta ya usafiri wa Anga, barabara pamoja na reli ya kisasa.

“Tunajua kuwa Serikali inakarabati meli huko za kisasa na kununua zingine, tuna mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), inapanua bandari na kujenga barabara, tunaimani kupitia chuo chetu tutatoa watu waliobobea watakaoshindana katika masoko ya kimataifa pia,” amesema

Mganilwa amesema uwekezaji mkubwa unaofanya na Serikali katika sekta ya usafirishaji umefanya chuo hicho kuendelea na mipango madhubuti ya kuzalisha wataalamu mahili.

 

 

 

 

 

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags