Waafrika Walioshinda Grammy Kupitia Kazi Zao

Waafrika Walioshinda Grammy Kupitia Kazi Zao

Peter Akaro

Ni hivi karibuni zimetolewa tuzo za 67 za Grammy huko Marekani na kumshuhudia msanii wa Nigeria, Tems akishinda kipengele cha wasanii wa Afrika akiwa ni wa pili kufanya hivyo baada ya Tyla wa Afrika Kusini. 

 

Hata hivyo, wanamuziki wa Afrika wamekuwa wakishinda Grammy tangu miaka ya 1960 wakati Miriam Makeba wa Afrika Kusini aliposhinda akiwa ni msanii wa kwanza katika bara hilo. 

 

Na hii ni orodha ya wasanii wa Afrika walioshinda tuzo za Grammy kupitia kazi zao wenyewe na sio zile za kushirikishwa ambazo ndizo hasa zimewapa wengi tuzo hiyo yenye hadhi ya juu zaidi duniani upande wa muziki tangu mwaka 1959. 

 

  1. Miriam Makeba (Afrika Kusini) 1966

 

Alizaliwa Prospect, kitongoji kilichotengwa karibu na Johannesburg mwaka 1932, Makeba baada ya kucheza filamu, Come Back, Africa (1959) iliyopinga ubaguzi wa rangi alipata umaarufu na kusafiri hadi New York na London akiimba nyimbo za kitamaduni. 

 

Akiwa London alikutana na Harry Belafonte na kuanza kufanya muziki pamoja, huku akiendelea na harakati zake, alitoa albamu, An Evening with Belafonte/Makeba (1966) yenye nyimbo zilizoimbwa kwa Kizulu na Kiswahili, na ndio albamu iliyoshinda Grammy. 

 

  1. Sade Adu (Nigeria ) 1986

 

Helen Folasade Adu ni mzaliwa wa Nigeria ila mama anatokea Uingereza, alisomea mitindo huko London kabla ya kuwa mwimbaji wa bendi ya Sade, walitoa albamu yao ya pili, Promise (1985) na kufanya vizuri hadi kushika namba moja chati za Billboard 200. 

 

Kufanya vizuri kwa albamu hiyo kulipelekea Adu kushinda Grammy kama Msanii Bora Chipukizi 1986, huku kundi hilo lenye makazi yake Uingereza kwa kipindi chote likichaguliwa kuwania Grammy mara nane na kushinda mara tatu. 

 

  1. Ali Farka Toure (Mali) 1994   

 

Katika maisha yake ameshinda Grammy mbili za Albamu Bora ya Muziki Ulimwenguni, alishinda kupitia albamu ya ushirikiano,  Talking Timbuktu (1994) akiwa na Ry Cooder, akashinda tena kupitia albamu, In the Heart of the Moon (2005). 

 

Ali Farka Toure aliyelelewa katika mji wa Niafunke kwenye ukingo wa Sahara nchini Mali, kabla ya kifo chake mwaka 2006, alikuwa Meya wa Niafunke na alitumia fedha alizopata kwenye muziki kujenga barabara na miundombinu mingine. 

 

  1. Cesaria Evora (Cape Verde) 2004

 

Alikulia katika umaskini na akaanza kuimba akiwa mtoto katika mji wa Mindelo huko Cape Verde, aliimba bila viatu ili kuwaenzi maskini na baadaye Evora alianza kutumbuiza katika maeneo mbalimbali duniani. 

 

Evora alipotoa albamu, Voz d'Amor (2003) ilifanya vizuri na kushinda Grammy kama Albamu Bora ya Muziki wa Kisasa Duniani 2004, licha ya umaarufu mwanamama huyo alichagua kuendelea kuishi Cape Verde hadi alipofariki mwaka 2011 akiwa na miaka 70. 

 

  1. Youssou N’Dour (Senegal) 2005 

 

Huyu ni alizaliwa huko Dakar, Senegal, mwishoni mwa miaka ya 1970 alipata umaarufu kama mwimbaji mkuu wa bendi ya Etoile de Dakar ambayo ilianzisha muziki aina ya Mbalax kwa kuchanganya dansi ya Afro-Latin na midundo ya kitamaduni. 

 

Mwaka 2005 N’Dour  aliweka rekodi kama mshindi wa kwanza wa Grammy kutokea Senegal baada ya albamu yake, Egypt (2004) kushinda katika kipengele cha Albamu Bora ya Muziki wa Kisasa Duniani 2005. 

 

  1. Angelique Kidjo (Benin) 2008

 

Mwimbaji huyu ana asili ya Benin na Ufaransa, baada ya kutoroka Benin na kuelekea Paris mwaka 1983, alisainiwa na Island Records na kupata umaarufu kimataifa mapema miaka ya 1990 kupitia vibao vyake kama Batong na Agolo.

 

Ndiye msanii wa Afrika aliyeshinda Grammy nyingi zikiwa ni tano, 2008 alishinda kwa mara ya kwanza kupitia albamu, Djin Djin (2007), akashinda nyingine tatu za Albamu Bora na mara mwisho akashinda kupitia albamu, Mother Nature (2021). 

 

  1. RedOne (Morocco) 2010 

 

Alizaliwa katika jiji lenye milima la Tetouan kaskazini mwa Morocco,  RedOne akiwa na miaka 19 alihamia Sweden kujiendeleza kimuziki kama mtayarishaji na mafanikio yake makubwa yamepatikana alipoandaa EP ya Lady Gaga, The Fame Monster (2009).

 

Mwaka 2010 EP hiyo yenye nyimbo kali kama 'Just Dance' na 'Alejandro' ilichaguliwa kuwania vipengele sita vya Grammy na kushinda vitatu ikiwemo cha Albamu Bora ya Elektroniki ambacho ushindi huwenda kwa mtayarishaji wa kazi husika. 

 

  1. Tinariwen (Mali) 2012

 

Kundi la Tinariwen kutokea Mali ambalo lilianzishwa miaka ya 1980 limechaguliwa mara tatu kuwania Grammy, kupitia albamu yao ya tano, Tassili (2011) walishinda kama Albamu Bora ya Muziki Duniani 2012. 

 

Maisha yao ya muziki huko Sahara hayakuwa marahisi kwani yaliathiriwa na vita kati ya serikali na waasi  na kuwafanya kuwa watu wa kuhama kila mara, hata albamu hiyo imerekodiwa katika nchi mbalimbali kama Mali, Algeria na Libya.

 

  1. Burna Boy (Nigeria) 2021

 

Kabla ya Burna Boy, wasanii wa Nigeria kama Femi Kuti, King Sunny Ade, Babatunde Olatunji na WizKid walikuwa wameshinda Grammy ila kupitia kazi walizoshirikishwa na wasanii wengine. 

 

Hivyo Burna Boy ni msanii wa kwanza wa kiume wa Nigeria kushinda Grammy kupitia kazi yake mwenyewe, albamu yake ya tano, Twice as Tall (2020) alishinda Grammy kama Albamu Bora ya Muziki Duniani 2021. 

 

  1. Black Coffee (Afrika Kusini) 2022

 

Ni DJ na Mtayarishaji muziki Afrika Kusini, kupitia albamu yake ya sita, Subconsiously (2021) alishinda Grammy kama Albamu Bora ya Elektroniki 2022 akiwa mtu wa kwanza nchini humo kushinda kipengele hicho. 

 

Hata hivyo, kabla ya Black Coffee, Afrika Kusini ilibebwa katika Grammy zaidi na waimbaji kama Ladysmith Black Mambazo na Soweto Gospel Choir alioshinda kupitia kazi zao wenyewe. 

 

  1. Tyla (Afrika Kusini) 2024

 

Anatambulika kama mwanamuziki wa kwanza kushinda kipengele maalam kwa muziki wa Afrika, Best African Music Performance, ni kupitia wimbo wake, Water (2023) uliofika hadi namba saba chati ya Billboard Hot 100 na namba moja Billboard U.S Afrobeats Songs. 

 

Tyla ambaye washindani wake walikuwa ni Asake & Olamide (Amapiano), Ayra Starr (Rush), Burna Boy (City Boy Miracle) na Davido (Unvailable) wote kutokea Nigeria, baada ya Grammy 2024 alishinda tuzo nyingine kama MTV EMAs, BET, MTV VMAs, Billboard n.k. 

 

  1. Tems (Nigeria) 2025 

 

Awali alishinda Grammy 2023 kupitia wimbo alioshirikishwa na Future, Wait For U (2022) alioshinda kama Best Melodic Rap lakini 2025 Tems akashinda kwa kazi yake mwenyewe, Love Me Jeje (2024) katika kipengele cha Best African Music Performance. 

 

Tems ambaye ni msanii wa pili Afrika kushinda kipengele hicho, ushindi wake ulikuja kufuatia kuwazidi kete washindani wake ambao ni Asake & Wizkid (MMS), Burna Boy (Higher), Yemi Alade (Tomorrow) na Chris Brown ft. Davido & Lojay (Sensational).






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags