Vitu vinavyoweza kuharibu ngozi yako

Vitu vinavyoweza kuharibu ngozi yako

Habari za siku msomaji wa fashion naamini kuwa u mzima wa afya tele na unaendelea na majukumu yako mbalimbali ya kulijenga taifa.

Leo tunakutana tena ili kuelezana na kujuzana mambo mbalimbali  ya urembo, mitindo na mavazi ambayo uwenda unayajua lakini mimi nakujuza tu zaidi.

Basi leo nakujuza juu ya vitu vinavyoweza kuharibu ngozi yako na ukajikuta ujiamini mbele za watu.

Kama tunavyofahamu kuwa ngozi ni kitu ambacho kikitunzwa vizuri huonyesha unadhifu wa mtu wa jinsi na rika lolote awe mwanaume, mwanamke, kijana, mtoto au mzee.

Unapoijali na kuitunza ngozi yako ndivyo unavyo ipa ngozi yako muonekano mzuri na wa kuvutia machoni pa watu wanaokuzunguka, usipoitunza huwezi kuwa na muonekano mzuri.

Kuna baadhi ya watu wanaamini wanaotakiwa kutunza ngozi ni wanawake tu, mimi leo  nakujuza kuwa jambo hilo si kweli kwa sababu hata mwanaume mtanashati lazima aitunze ngozi yake ili kuonyesha umaridadi na unadhifu wake.

Ngozi isiyo na matunzo mazuri huondoa mvuto wa mtu kwa sababu unaweza ukawa na chunusi, harara, upele hata mikunjo ya usoni ambayo itaondoa mvuto na umahiri wako.

Vipo vitu mbalimbali vinavyoharibu ngozi ya mtu na kuifanya kutokuwa nzuri na ya kuvutia.

Baadhi ya vitu hivyo ni, kutokunywa maji ya kutosha kwa siku, ili uwe na ngozi nzuri inayovutia unatakiwa kunywa maji mengi ili kuwezesha uchafu kutoka kwa njia ya mkojo lakini pia kuyeyusha mafuta yanayoweza kusababisha chunusi.

Pia ngozi inaweza kuharibiwa na matumzi ya losheni zenye kemikali nyingi, wako watu wengi wanaotumia losheni hizo ambazo huharibu ngozi zao kwa kubadilisha rangi, kuleta makunyanzi, chunusi na hata vidonda wakati mwingine.

Kitu kingine ni kutopata lishe bora hii pia inaweza kusababisha ngozi yao iharibike kwa kuwa mwili unakosa vitamin na virutubisho vinavyoweza kufanya kazi ya kuainisha ngozi yako na kuiweka katika hali nzuri.

Kiwango kikubwa cha homoni mbalimbali, ujauzito na matumizi ya dawa za kuzuia mimba pia huweza kuharibu ngozi yako kwani vitu hivi husababisha mabadiliko ndani ya mwili wa binadamu.

Msongo wa mawazo uliyokithiri ndio pia unaweza kuharibu ngozi yako, mtu anapokuwa na msongo wa mawazo uliyokithiri husababisha awe na huzuni muda wote hivyo ngozi ya mwili wake kusinyaa, lakini pia msongo wa mawazo husababisha mabadiliko ya homoni ambapo homoni uongezeka kwa wingi na nyingine upungua.

Uchafu pia una sehemu kubwa katika kuharibu ngozi, wapo baadhi ya watu hawapendi kusafisha miili yao, unapokuwa unapaka mafuta au losheni na vipodozi mbalimbali halafu unalala bila kuoga vitundu vya kutolea uchafu kwa njia ya jasho huziba hivyo husababisha kutokea kwa chunusi, upele au harara.

Upakaji wa vipodozi usoni (makeup) bila kufuata utaratibu na kanuni pia uchangia kuharibu ngozi yako. Kina dada wengi hupenda kujipaka vipodozi usoni pasipokujua kama vinafaa kwa ngozi zao au la.

Wadada wengi upaka na kulala na makeup bila kutoa ana kutoa kwa njia isiyofaa, hali hii pia uinyima ngozi uwezo wa kupumua na kutoa uchafu hivyo kufanya ibaribike.

Hivyo basi ni muhimu kila mtu yaani mwanamke mwanaume kutunza ngozi yake ili kuondoa mikunjo, chunusi, harara iliyoko usoni hata miwasho iliyopo katika mwili.

Waweza kutunza ngozi yako isiharibike na kuonekana nadhifu kwa kunywa maji mengi (kuanzia lita tatu kwa siku), kula matunda na lishe bora, fanya mazoezi kwa wingi, safisha ngozi yako kwa maji mengi na sabuni.

Epuka matumizi ya losheni zenye kemikali, epuka matumizi ya vipodozi mara kwa mara, matumizi ya dawa bila kupata ushauri kwa daktari.

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post