Vidonge vya P2, kichocheo kwa wasichana kupata saratani ya matiti

Vidonge vya P2, kichocheo kwa wasichana kupata saratani ya matiti

Wasichana na wanawake wengi kwa sasa wamekuwa wakitumia vidonge vya kuzuia mimba maarufu kama P2 bila kufuata utaratibu wala maelekezo kutoka kwa daktari.

Leo hii katika makala ya afya tunaangazia madhara ya matumizi holela ya muda mrefu ya dawa hiyo ya kuzuia mimba na kwa wanawake na wasichana.

Kandali Samweli ni daktari Mbobezi wa Tafiti za Saratani Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Saratani kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) anaeleza bayana juu ya madhara ya vidonge hivyo kama zitatumiwa na mtu kwa muda mrefu,

Daktari Samwel amewasihi wasichana kujiepusha na matumizi holela ya muda mrefu, pasipo kuzingatia ushauri wa daktari na kwa wingi kupita kiasi kwa vidonge vya dharura vya kuzuia mimba maarufu P2, kwani ni tabia hatarishi inayoonekana kuchangia kupata saratani hiyo.

“Pale Ocean Road miaka ya hivi karibuni tunagundua hadi wasichana wenye umri kati ya miaka 20 hadi 25 wana saratani ya matiti, wapo wanaoeleza wametumia dawa hizo bila ushauri wa daktari, kwa wingi na kwa muda mrefu.

“Tafiti mbalimbali zilizofanyika duniani zinaonesha watu wanaotumia kiholela, kwa wingi vichocheo hivyo wapo kwenye uwezekano mkubwa kuishia kupata saratani hiyo,” anasema Dk. Samwel na kuongeza

“Hivyo, tunapata hizo taarifa, tunatilia maanani na tunaendelea kutoa elimu sahihi ili mbeleni tusije tukapata shida, hii inatufumbua macho na huu ni wito kwa kwa upande wa tafiti tuangalie shida hii ipo kwa kiwango gani kwenye jamii.

“Sisi tunaona tu kama wahudumu watu wanatoa hizi shuhuda, lakini hatuwezi kujua kwa kiwango gani pengine tatizo ni kubwa zaidi, hili linaweza kuletewa majibu na tafiti za kisayansi zaidi,” anasema.

Anasema kimsingi dawa hizo zinapaswa kutumiwa pale tu dharura inapotokea ndiyo maana zinaitwa ‘emergency contraceptive’, zimewekwa kwa ajili ya dharura na dharura kutokea labda ni mara moja.

“Kwa mfano kwa mtu ambaye anaweza kujamiiana pasipo kutarajia kile kitendo labda amebakwa na sisi wataalamu tunatarajia kitendo hicho si cha mara kwa mara,” anasema.

Hata hivyo Dk. Samweli anasisitiza kuwa dawa hizo za P2 ni kichocheo cha wanawake kupata saratani hiyo ya matiti.

“Hizi dawa ni kichocheo kikubwa sana cha hii saratani na ndio maana tunawasisitizia vijana kutozitumia kabisa bila kupata ushauri kutoka kwa daktari,” anasema

Aidha anasema njia za uzazi wa mpango zina kiwango cha homoni ambazo zinakuwa zimepimwa kwa wakati huo, lakini kumbe jamii wanafanya kuwa matumizi ya mara kwa mara, kwa wingi bila ushauri wa wataalamu, wanameza kama karanga.

Anasema pamoja na hilo, vipo visababishi vingine vinavyoweza kuchangia mwanamke kupata saratani ya matiti ikiwamo kuchelewa kuzaa, kutokuzingatia kunyonyesha ipasavyo, kurithi kwenye familia na sababu nyinginezo.

Kaimu Meneja Rasilimali Watu Veta- ICT Kipawa, Upendo Abraham amemshukuru wataalamu wa ORCI kutoa elimu hiyo ambayo imewaelimisha wanafunzi kuhusu saratani.

“Kwa sababu asilimia moja ya wanaopata saratani hii ni wanaume na asilimia 99 ni wanawake, tuna vijana vyuoni mwetu tuliona wakielimishwa kuhusu visababishi vya saratani hii, elimu hii itawasaidia na wale watakaokutwa na tatizo watapata matibabu kwa wakati.

“Wanafunzi 124 na watumishi 24 wakiwamo wanaume wameonesha utayari wa kuchunguzwa, hapa chuo wanafunzi wetu wengi ni wanaume kwa asilimia 75,” amesema.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post