Kwa miaka ya nyuma kidogo nguo za Boubou zilikuwa zikitumika kuvaliwa hasa katika sehemu za misiba na sehemu za heshima, lakini kwa takribani mwaka mzima sasa nguo hizo zinazoshonwa na vitambaa vya lesi zimerudi tena mjini huku baadhi ya watu wakizivaa zaidi katika sehemu za sherehe.
Historia ya vazi la Boubou
Boubou ni vazi la Kiafrika linalovaliwa na wanaume na wanawake katika maeneo mengi ya Afrika Magharibi, na sehemu za Afrika ya Kati. Boubou kwa ujumla linajumuisha vipande viwili ambavyo ni shuminzi (gauni lenye mikoni mifupi) na gauni jingine kubwa la juu ambalo linakuwa la lesi.
Historia ya mavazi ya Boubou inarudi tena baada ya kupita kwa karne nyingi huku chimbuko lake likiwa ni kutoka katika mataifa kama Nigeria, Senegal, Ghana, na Mali. Hapo awali, boubou lilivaliwa na familia za kifalme na waheshimiwa, likiwa ishara ya hadhi, utajiri, na nguvu.
Kutokana na mavazi hayo kupendelewa zaidi na kuwapatia watu muonekano wenye hadhi zaidi kwa sasa linatajwa kuteka sekta ya mitindo na soko la biashara la kimataifa.
Vazi hili hutengenezwa na kitambaa cha ‘Lace Kaftan’ ni aina ya kitambaa chenye muundo wazi na wa kupendeza, kitambaa hicho kimekuwepo kwa karne nyingi na hapo awali kilitengenezwa kwa mikono kwa kutumia nyuzi za aina mbalimbali, lakini siku hizi hutengenezwa kwa kutumia mashine.
Uzuri wa kitambaa hiki kinachotengeneza nguo za Boubou haupo tu kwenye kutengeneza mavazi hasa magauni lakini pia vinaweza kutumika kwa matumizi mbalimbali kama vile mapambo ya nyumbani na katika sehemu zenye mzunguka mwingi wa watu.
Mara nyingi vitambaa hivi hutengenezwa kwa kutumia nyuzi za aina tofauti kama vile pamba, hariri, polyester, na nailoni. Mtindo huu wa vazi hilo umerudi upya ukiwa na rangi tofauti tofauti ukiachilia na ule wa zamani ambao ulikuwa na rangi mbili ambazo ni nyeupe na nyeusi lakini kwa sasa unaweza kupata katika rangi ya bluu, njano, nyekundu, zambarau, kijani, maruni na nyinginezo.
Leave a Reply