Nancy Sumari Miss Tanzania 2005, hadi sasa ndiye mrembo mwenye historia yenye msisimko zaidi tangu kuanzishwa kwa Miss Tanzania, hii ni baada ya kufanikiwa kutwaa taji la Miss World Africa (Continental Queen of Africa) 2005 na ndiye Mtanzania pekee aliyefanya hivyo.
Nancy ambaye 2017 alitajwa katika orodha ya vijana 100 wenye nguvu ya ushawishi Afrika, anatoa mafunzo ya matumizi ya vifaa vya kidijitali kwa watoto kupitia taasisi yake ya Jenga Hub, pia ameandika vitabu vinavyowahusu kama Haki, Nyota Yako n.k.
Baada ya Nancy kutamba alifuata Wema Sepetu 2006. Ndiye anatajwa kuwa mrembo maarufu zaidi katika historia ya Miss Tanzania, baada ya kukabidhi taji, Wema alienda Malaysia aliposomea biashara ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Limkokwing na aliporejea nchini akajitosa katika uigizaji.
Filamu yake ya kwanza kucheza ni A Point of No Return (2007) akiwa na Marehemu Steven Kanumba, kisha zikafuata nyingine kama Family Tears (2008), Red Valentine (2009) na White Maria (2010).
Wema aliyeshiriki Miss World huko Warsal, Poland, ukiachana na mambo mengi umaarufu wake umekuzwa na uigizaji akishinda tuzo kama Sinema Zetu International Film Festival Award (SZIFF), Hollywood And African Prestigious Awards (HAPAWARDS) n.k

Leave a Reply