Utamjuaje mwanaume anayetaka kukuchezea

Utamjuaje mwanaume anayetaka kukuchezea

Wakati watu wawili mwanamke na mwanaume wanapokuwa kwenye kilele cha mapenzi, ni rahisi sana kila mmoja kuchunga kauli zake na kuongea yale ambayo yatamvutia mpenzi wake ili kila mmoja awe na mvuto kwa mwenzake na hivyo kuwa karibu zaidi. Hata hivyo watu wengi (hususan wanawake) wanashindwa kung’amua kwamba, katika mapenzi kila mmoja ana lake moyoni, na ni vigumu kujua mwenzako anawaza nini juu yako.

Katika mahusiano mara nyingi wanawake ndio huumizwa kwa sababu wakati mwingine mwanaume anapomtaka mwanamke humpa matarajio makubwa kuhusu hatima yao ili kumvuta, lakini kumbe analo lake moyoni na hapo ndipo mwanamke hujikuta akijitolea kwa hali na mali, akijua kwamba mwenzake amempenda na wataoana wakati kumbe mwenzie wala hana mpango huo.

Ni vyema kama mwanamke akiamua kujiingiza kwenye uhusiano, basi awe na uhusiano na mwanaume ambaye anaonekana dhahiri kuwa ni muoaji na si wa kumchezea tu na kuingia mitini. Unaweza kujiuliza kuwa utamjuaje mwanaume muoaji na yule ambaye si muoaji bali wa kukuchezea tu.

Hapa chini nitaeleza baadhi ya mambo muhimu yatakayomuwezesha mwanamke kujua kama mwanaume aliye nae ni muoaji au anamchezea tu:

  1. Katika mazungumzo yenu ya kawaida jaribu kuzungumzia kuhusu maisha ya ndoa ili kuangalia kama yeye anayachukulia vipi.

Wanawake wengi hukwepa kuzungumzia maisha ya ndoa na wapenzi wao kwa kuhofia kwamba wataonekana wanajipigia debe ili waolewe, lakini hili ni jambo muhimu sana kulijadili.

Kwa nini?

Kwa sababu ni muhimu kwa wapenzi waliopendana na kuaminiana kukaa na kujadili kuhusu matarajio ya kila mmoja ili kujua kama wako kwenye mustakabali mmoja au la. Kwa kujadili kuhusu jambo hilo kutawawezesha kujiwekea malengo ya namna ya kufikia matarajio yao.

Iwapo mwanaume ataonekana kutovutiwa na mazungumzo hayo, basi hapo mwanamke ajue kwamba anachezewa na kama akiendelea na uhusiano huo, basi ajue kwamba, amekubali kuchezewa. 

  1. Katu usijiaminishe kwamba kila mwanaume utakayekutana naye na kukutongoza na kukuahidi kukuoa kuwa huenda akawa ndiye mtarajiwa.

Wanawake wengi wamekuwa na hamu kubwa ya kutaka kuolewa na wanayatamani sana maisha ya ndoa. Wanaamini kwamba kila mwanaume atakayemualika kuwa na mtoko naye hususan wa chakula cha mchana au usiku ndiye mtarajiwa.

Lakini jambo ambalo wanawake wengi hawalijui ni kwamba si kila mwanaume anayevutiwa na yeye ni muoaji. Ni kujidanganya tu, si wote wenye nia thabiti ya kutaka kuoa. Kwao jambo la muhimu ni kutaka kuonja na kuacha. 

  1. Ni vyema ukaangalia matendo yake zaidi kuliko maneno yake.

Hii ni muhimu sana. Mwanaume anaweza kukwambia kwamba wewe ndiye chaguo lake atakayekuoa na anaweza hata kukupeleka kwa Sonara au duka la kuuza pete za uchumba za dhahabu na kukununulia pete ya uchumba ya gharama, lakini kama hataanza kuchukua hatua muhimu za kukutambulisha kwao kwa ajili ya kupata baraka za wazazi wake au kujitambulisha kwenu kwa ajili ya kupata Baraka za wazazi wako, basi ujue kwamba hayo ni maneno matupu na katu hayavunji mfupa.

 Hapo ujue kwamba huna chako bali unachezewa na iwapo utaendelea na uhusiano huo, basi umekubali kuchezewa.

  1. Kama mwanaume akiwa mkweli na kukueleza kwamba anakupenda lakini hana mpango wa kuoa hivi karibuni, usilazimishe kujenga uhusiano naye kwa nia ya kutaka kumshawishi ili akuoe.

Kama kuna mambo ambayo mnaendana na umevutiwa kuwa naye karibu, si vibaya kujenga naye urafiki wa kawaida usiohusisha mapenzi. Lakini ni vyema kuwa makini kwani wakati mwingine urafiki wa kawaida na mwanaume unaweza kukufikisha mahali ambapo hukutarajia.

  1. Tengeneza aina ya maisha yatakayokutambulisha jinsi ulivyo na matarajio yako, pamoja na msimamo wako kuhusu mahusiano.

 Hiyo itakufanya kujenga uzingativu kwenye matarajio yako na haitakuwa rahisi kwako kwenda kinyume na malengo uliyojiwekea hasa pale atakapojitokeza mwanaume atakayetaka kujenga mahusiano na wewe.

Ni vyema wanawake wakijua kwamba, ni rahisi kuingia katika mitego ya wanaume wakware.

Kama hutaki kujiingiza kwenye uhusiano utakaokuumiza na kukusababishia maumivu makali moyoni, basi ni vyema kujua aina ya uhusiano ulionao na huyo mpenzi wako. Usikubali kuchezewa!






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Shaban Kaluse

A Sales and Marketing in the hospitality Industry and also a freelance journalist, writing about love and relationships and educative articles which aims for youths, every Tuesday on Mwananchi Scoop.


Latest Post