Usiyoyajua kuhusu Queen Darleen na Diamond

Usiyoyajua kuhusu Queen Darleen na Diamond

Mwimbaji wa Bongo Fleva, Queen Darleen kwa kipindi cha takribani miaka 20 akiwa ndani ya tasnia hiyo, ana makubwa aliyoyafanya katika muziki wake kwa kiasi chake akitengeneza nyimbo kadhaa kubwa na kushinda tuzo.

Huyu alianza muziki mwanzoni mwa mwaka 2000 baada ya kusikika katika wimbo ‘Historia ya Kweli’ wake Dully Sykes, na alifanya kazi na G Records na kwa sasa yupo WCB Wasafi licha ya kutoachia kazi kwa muda mrefu. Fahamu zaidi.

Sauti ya msichana katika wimbo wa Inspector Haroun ‘Mtoto wa Geti Kali’ ni ya Darleen, na aliyewakutanisha ni Dully Sykes pande za Ghorofani Kariakoo. Inspector alikuwa na mazoea ya kwenda huko ili kukutana na DJ G Lover (Guru) wa G Records.

Wakati huo Darleen alikuwa bado binti mdogo ambaye alipenda muziki, hivyo wakaenda kuomba ruhusu kwa mama yake ili aweze kushiriki katika wimbo huo, walikubaliwa na huo ndiyo ukawa mwanzo wa safari yake katika muziki.

Baadaye Darleen alipata nafasi ya kusainiwa G Records, lebo iliyofanya kazi na wasanii kama Dully Sykes, Abby Skills, Pasha na Alikiba ambaye wameshirikiana katika nyimbo kadhaa ikiwemo, Najua Nakupenda (2006) na Ndio Yule (2009).

Tuzo ya kwanza kwa Queen Darleen kushinda katika muziki ni kutokea Tuzo za Muziki Tanzania (TMA), alishinda kipengele cha Wimbo Bora wa Ragga & Dancehall kupitia wimbo wake, Maneno Maneno (2012).

Kabla ya Diamond hajatoka, Darleen alimwambia asiseme popote wao ni ndugu maana atabaniwa na baadhi ya redio kitu kilichomtokea yeye akiwa G Records. Walitunza siri hiyo hadi kwenye show ya ‘Diamond Are Forever’ Machi 2012 walipoifichua.

Awali Diamond alikuwa hatoi wimbo hadi amsikilizishe Darleen na kumshauri, huyu alikuwa karibu naye tangu anaanza muziki na kipindi video ya pili ya Diamond ‘Mbagala’ inashutiwa Darleen alikuwepo location.

Darleen alikuwa ni mfanyakazi pale WCB Wasafi na alikuwa akilipwa mshahara kama wafanyakazi wengine, ila kazi yake ilikuwa ni upande wa muziki tu kama kusimamia zile behind the scene ndipo baadaye mwaka 2016 akasainiwa kama msanii.


Huyu ndiye alitakiwa kuwa msanii wa kwanza kusainiwa WCB Wasafi ila kutokana ni undugu na Diamond ikaonekana haitaleta mvuto wa kibiashara, hivyo Darleen akangoja watambulishwe Harmonize, Rayvanny na Rich Mavoko ndipo yeye.

Na hadi sasa Darleen hajatoa albamu wala EP chini ya WCB Wasafi alipodumu kwa miaka nane ila Lava Lava, Mbosso, Zuchu na D Voice ambao wamemkuta tayari wamefanya hivyo huku yeye akiwa kimya mwaka wa nne sasa.

Queen Darleen hajawahi kumshirikisha Diamond katika wimbo wake, hivyo hivyo Diamond hajafanya hivyo licha ya kuishi pamoja tangu wakiwa wadogo. Wawili hao wamekutana tu katika nyimbo mbili za WCB Wasafi, Zilipendwa (2017) na Quarantine (2020).






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags