Unafahamu nini kuhusu tezi dume

Unafahamu nini kuhusu tezi dume

Na Mark Lewis

Tezi dume ni kiungo kidogo na ni sehemu moja ya uzazi wa wanaume. Hupatikana chini ya kibofu na mbele ya mwanzo cha njia itoayo mkojo hupitia ndani ya tezi dume.Tezi dume ndiyo hutoa maji yabebayo mbegu (manii) ya mwanaume.

Tezi dume kupanuka

Kupanuka kwa tezi dume ni tatizo la kawaida ambalo halisababishwi na ugonjwa wa saratani(kansa). Huwa ni jambo la kawaida kwa karibu kila mwanaume mzee. Miaka inavyoenda,ndivyo tezi dume huzidi kuwa kubwa; na hufinya njia ya mkojo na kuziba mkojo.Hivyo mkojo hutoka polepole .

Dalili za kupanuka kwa tezi dume

Dalili huonekana baada ya umri wa kuanzia miaka hamsini. Dalili huanza polepole na kuzidi jinsi miaka inavyoongezeka.Dalili hizi ni kama zifuatazo:

  • Kukojoa mara nyingi hasa nyakati za usiku. Hii ni dalili ya mapema sana.
  • Kulazimika, mara nyingi hasa nyakati za usiku, kutumia nguvu kuanzisha mkojo kutoka. Hata pale mgonjwa anahisi kibofu kimejaa. Hii ni dalili ya mapema sana.
  • Mkojo kutiririka polepole, hukatikakatika na hutumia nguvu kutoka.
  • Mkojo kushindwa kutoka hata wakati mtu anapohisi kukojoa.
  • Mkojo kuendelea kutoka kidogokidogo baada ya kukojoa, matone ya mkojo huendelea kutoka hata baada ya kukojoa hivyo nguo za ndani hulowa.
  • Kibofu hakiishi mkojo.

Matatizo ya tezi dume iliyotanuka

Tezi dume ikitanuka sana huleta matatizo mengi kwa wagonjwa wengine hali hii isipotibiwa. Matatizo hayo ni kama yafuatayo:

  • Mkojo kukosa kutoka kabisa
  • Wagonjwa wenye tatizo hili lazima wawekewe katheta ili kumimina mkojo.
  • Madhara kwenye kibofu na figo.
  • Kwa sababu ya kibofu kuwa na mkojo wakati wote, ukuta na misuli yake hupanuka na mwishowe hudhoofika hivi kwamba haiwezi kuzuia mkojo.
  • Kwa sababu ya kibofu kujaa mkojo hurudi kwenye figo na mwishowe huharibu figo.
  • Maambukizi na mawe
  • Kwa sababu kibofu hakimimini mkojo wote kuna hatari kubwa ya maambukizi kwenye njia ya mkojo na kuwa na mawe kwenye kibofu.

Utambuzi wa kupanuka kwa tezi dume

Historia na dalili zikiashiria uwepo wa hali hii, basi uchunguzi ufuatao hufanywe.

Uchunguzi wa ukubwa wa tezi

Uchunguzi huu hufanywa kwa kuingiza kidole chenye glavu nyuma hadi kwenye tezi dume. Daktari huweza kujua ukubwa na hali yake. Iwapo mtu ana ugonjwa huu tezi dume ni kubwa kuliko kawaida, laini na gumu yote pamoja. Iwapo tezi lina vifundo basi inaweza kuwa na kansa (saratani).

Vipimo vya picha ya ultrasound na kiasi cha mkojo kwenye kibofu

Picha za ultrasound zinaweza kutathmini ukubwa wa tezi dume na kutambua shida zingine kama kudhoofika kwa tezi,kupanuka kwa njia ya mkojo na kibofu au usaha. Picha hizi pia hutumika kutathmini kiwango cha mkojo unaobaki baada ya kukojoa. Ikiwa kiasi cha mkojo ni chini ya mililita hamsini, basi inaonyesha mkojo wa kutosha unatoka , mililita mia moja hadi mbili au zaidi huonyesha kuna kasoro na basi uchunguzi hufanywe.

Uchunguzi wa maabara.

Uchunguzi huu hauwezi kusaidia katika kutambua ugonjwa wa tezi dume, bali hutumika kutambua matatizo yanayohusiana nao.Mkojo hupimwa ili kutambua maambukizo, na damu hupimwa ili kutathimini uwezo wa figo.

Prostate Specific Antigen (PSA)

 hiki ni kipimo muhimu sana cha damu cha kuchunguza saratani ya tezi dume.

MATIBABU YA TEZI DUME

Mambo yanayozingatiwa katika matibabu ya tezi dume ni pamoja na ukali wa dalili na jinsi shughuli za mgonjwa zinavyoathirika na dalili za ugonjwa huu. Lengo la matibabu huwa ni kupunguza makali ya dalili, kurahisisha maisha,kupunguza mkojo unaobaki kibofuni na pia kuzuia matatizo yanayokuja na ugonjwa huu.

A: Kubadilisha maisha na kungoja

Hii ndiyo njia inayopendekezwa kwa wanaume ambao wana dalili kidogo ambazo haziwasumbui. Hata hivyo,haimaanishi kukaa tu bila kufanya chochote.Wakati mgonjwa anangoja,anahitajika kubadili jinsi anavyoishi ili kupunguza dalili zilizopo,na pia kumwona daktari kila mara(walao mara moja kwa mwaka) ili kujua kama dalili zinapungua au zinazidi.

 

  • Badili mazoea ya kukojoa na kutumia vinywaji.
  • Kojoa mara kwa mara,usizuie mkojo,kojoa mara tu haja ijapo.
  • Kojoa kwa vipindi viwili, yaani kwanza kojoa kama kawaida, ngoja kidogo na ujaribu kukojoa tena papohapo,usijilazimishe kukojoa.
  • Usinywe pombe wala kahawa jioni.Hivi viwili hulegeza kibofu na kufanya figo kitengeneze mkojo na hivyo basi kukojoa zaidi usiku.
  • Usinywe maji mengi sana.Usizidi lita tatu kwa siku.Usinywe maji mengi mara moja bali unywe kidogo kidogo siku nzima/mchana wote.
  • Punguza vinywaji unapoenda kulala au unapoenda kwenye shughuli nje.
  • Usinunue dawa za homa dukani.Hizi huzidisha dalili na mkojo kutotoka.
  • Badilisha wakati unapokunywa dawa za kukojoza.
  • Jichunge na baridi, weka mwili wako na joto na fanya mazoezi. Kutokufanya mazoezi huzidisha dalili.
  • Fanya mazoezi ya mifupa ya nyonga ili ipate nguvu. Mifupa hii ndiyo hushikilia kibofu na kusaidia kufunga njia ya mkojo.Mazoezi haya ni kukaza na kuachilia misuli ya nyonga.
  • Jaribu kukojoa baada ya muda fulani siku yote.
  • Pata matibabu unapofunga choo.
  • Punguza mfadhaiko.Kufadhaika na wasiwasi husababisha kukojoa zaidi.
  1. Matibabu ya dawa

Dawa za kulegeza misuli,dawa za kupunguza tezi dume na matibabu ya mseto.

  1. Njia ya upasuaji

Upasuaji umegawanyika katika aina mbili kukatwa sehemu au kipande cha tezi dume au kuchomwa.

Kuchomwa yaweza kuwa kuchoma kwa mawimbi ya sitima. Kumomonyoa kwa sindano. Kuchoma kwa maji moto. Kuwekwa springi au koili. Kuchomwa kwa miale.

Je,mgonjwa wa tezi dume lililotanuka anafaa kumwona tena daktari lini?

  • Akishindwa kukojoa kabisa.
  • Kuwashwa au uchungu akikojoa, mkojo wenye harufu mbaya, homa na kuhisi baridi.
  • Damu kwenye mkojo.
  • Kushindwa kuzuia mkojo na nguo za ndani kulowa mkojo

Je, mtu mwenye tezi dume iliyotanuka anaweza kuwa na saratani pia?

Ndio. Dalili za magonjwa haya mawili hufanana.Kwa hiyo vipimo vya kawaida vilivyotajwa haviwezi kutambua ugonjwa wa saratani. Lazima vipimo maalum vya saratani vifanywe. Vipimo hivi ni kumpima mgonjwa nyuma kwa kidole, kipimo cha damu kuona kiwango cha PSA na kuchukua kipande cha tezi dume (prostate biopsy).

 

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags