Umuhimu wa matamasha ya sanaa kwa wanavyuo

Umuhimu wa matamasha ya sanaa kwa wanavyuo

Na Magreth Bavuma

Mambo niaje wanangu ni wiki nyingine tena niwakaribishe kwenye kona yetu pendwa ya wanavyuo “unicorner” chimbo moja tu ambalo wanavyuo tunakutanishwa kwa njia ya maandishi kujifunza kwa pamoja.

 Ni mara ngapi umewahi kusikia kuhusu matamasha ya wanavyuo na ukahudhuria? ukiachana na yale ambayo lengo lake kubwa ni kutafuta mshindi katika category fulani, jaribu kuvuta picha ya uwepo wa matamasha ya wanavyuo ambayo yatawakusanya wanavyuo wenye vipaji tofauti tofauti na kuwapa platform ya kuonyesha uwezo wao na sio kushindana kama ilivozoeleka.

Matamasha ya wanavyuo ni sehemu muhimu ya maisha ya chuo kikuu. Ni fursa kwa wanafunzi kuonesha vipaji vyao vya muziki, sanaa, na utendaji. Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na mwelekeo wa kuandaa matamasha ya wanavyuo kama mashindano. Hii inaweza kuwa na athari mbaya kwa wanafunzi, kwani inaweza kuwafanya wahisi shinikizo la kushindana na wengine, na inaweza kuwazuia kushiriki katika matamasha kwa sababu ya hofu ya kushindwa.

Sambamba na sababu za wengi wao kupenda kushiriki mashindano hayo licha ya ushindani kuwa mkubwa baadhi yao huwa na sababu mbalimbali zinazofanya wasishiriki mashindano baadhi ya wanavyuo wanatoa mawazo yao juu ya suala hili,

Mwanfunzi kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam Exaudi Matokeo anasema “baadhi ya wanavyuo hawapendi kushiriki mashindano ya sanaa kwa sababu wanaona ni kama wanapoteza muda”, akigusia tamasha la Sanaa blast la UDSM ambalo huwa kwa kawaida linafanyika muda ambao unaingiliana na baadhi ya vipindi darasani hivyo mtu anaona kuliko aache vipindi ni bora aipoteze fursa kama hiyo.

Anaongezea “wanachuo wengi wamekua na tabia ya kupuuzia baadhi ya mambo ambayo kwao haikua kipaumbele wakati wanafika chuo kwa mfano mtu amekuja zake chuo kusoma sheria au ustawi wa jamii, ndiyo anakipaji lakini anaona kama aaah mimi nisome nimalize niondoke chuo kwa upande mwingine pia mifumo ya uongozi wa baadhi ya vyuo inasababisha wanafunzi kutopenda kushiriki katika matamasha ya mashindano.

Anahitimisha “lakini pia kujuana ni kwingi sana bhana mtu unaweza ukajitoa ukasema uingie kwenye mashindano mwisho unaishia kutoka na mchoko tu, watu wanapiga simu moja nakwambia unashangaa imekuaje mimi mbona nipo hapa muda tu nimewekwa benchi, kwa hiyo bana mashindano ni mazuri ila ukianza kufikiria kujuana juana huko unaona ni heri ufanye zako mambo mengine tu.

Muhitimu wa chuo kikuu kishiriki cha Tumaini Dotto Malela anasema “wengine hawashiriki kwa sababu tu ya kutojiamini unakuta mtu anakipaji kabisa lakini anaona nikama ha-fit in kwenye mashindano.

 Anaongezea kwa kusema “wengine wanakua na fear of cost kwa sababu mashindano mengine yatamtaka mshiriki kuwekeza sana kwa mfano mashindano ya ubunifu wa mavazi na mengine mengi yanayo fanana na hayo”.

Matamasha ya wanavyuo yanatakiwa yapewe kipaumbele kwa utofauti na mfumo wa kimashindano ili kuwezesha wanafunzi kuonesha vipaji vyao, matamasha ya wanavyuo ni fursa nzuri kwa wanafunzi kuonesha vipaji vyao vya muziki, sanaa, na utendaji. Matamasha haya yatasaidia kuunda mtandao na watu wengine wenye vipaji sawa, na inaweza kusababisha fursa za kazi au masomo.

Vilevile kushiriki katika matamasha ya wanavyuo kunaweza kusaidia wanafunzi kuboresha kujiamini kwao, kwa kuwa watapata nafasi ya kukutana na wenzao wenye vipaji itasaidia kuwaongezea confidence, maarifa zaidi na ujuzi wa juu ya kile wanachokifanya.

Baadhi ya wanavyuo hawapendi kujihusisha na masuala ya kijamii na hii inatokana na makuzi na malezi waliyoyapata ambayo yanachangia wao kupendelea kuwa pekeyao mara nyingi, lakini kama kutakuwepo matamasha ya wanavyuo ni njia nzuri kwa wanafunzi kujihusisha na jamii ya chuo kikuu na kuwasaidia wao kuunda mahusiano mapya.

Ili kuhakikisha kwamba matamasha ya wanavyuo yana manufaa kwa wanafunzi, ni muhimu kuandaa matamasha haya kama fursa za kuonesha vipaji na siyo kama mashindano na inaweza kufanywa kwa njia zifuatazo

Kupunguza msisitizo kwenye kushinda, matamasha ya wanavyuo yanapaswa kuwa na msisitizo zaidi kwenye kuonesha vipaji na siyo kwenye kushinda. Hii inaweza kufanywa kwa kutotoa tuzo kwa mshindi mmoja, lakini badala yake kutoa tuzo kwa wanafunzi wote wanaoshiriki.

Kutengeneza mazingira rafiki kwa washiriki, matamasha ya wanavyuo yanapaswa kuwa na mazingira ya kirafiki ambayo yatafanya wanafunzi wote wawe comfortable kushiriki. Na inaweza kufanywa kwa kuhakikisha kuwa kuna msaada wa kutosha kwa wanafunzi wanaoshiriki, na kwa kutengeneza mazingira ya burudani na furaha.

Zaidi pia wanafunzi wanapaswa kuelimishwa kuhusu manufaa ya matamasha ya wanavyuo kama fursa za kuonesha vipaji na kujihusisha na jamii, inaweza kufanywa kupitia program za elimu na uhamasishaji.

Matamasha ya wanavyuo ni fursa muhimu kwa wanafunzi kuonyesha vipaji vyao na kujihusisha na jamii. Ni muhimu kuhakikisha kwamba matamasha haya yanapangwa kwa njia ambayo yanaangazia manufaa ya kuonyesha vipaji na siyo shinikizo la kushindana. Kwa kuchukua hatua hizi, tunaweza kuhakikisha kwamba matamasha ya wanavyuo yanabaki kuwa fursa muhimu kwa wanafunzi.

Kwa leo niseme shukrani sana kwa kuendelea kufuatilia kona yetu pendwa ya dunia ya wanavyuo “unicorner” kama una mawazo yoyote kuhusu Makala zetu usisite kunifikia moja kwa moja kupitia ukurasa wangu wa Instagram @mcmaggie19 until next time tchaaoooo!!!!!.
.
.
.
#MwananchiScop
#BurudikaNasi






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags