Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza Suella Braverman amesema watu wanaoingia Uingereza kupitia njia zisizo halali wasiruhusiwe kuomba hifadhi nchini humo.
Braverman ameapa kuendelea na mpango wenye utata wa kuwapeleka nchini Rwanda watu wanaoomba hifadhi. Hata hivyo amesema kutokana na changamoto za kisheria kuhusu sera hiyo hakuna mtu atakayepelekwa Rwanda mwaka huu.
Kulingana na mpango huo uliosainiwa mwezi Aprili, Uingereza inapanga kuwapeleka Rwanda baadhi ya wahamiaji wanaowasili nchini humo kwa kutumia boti ndogo ambako mchakato wa maombi yao ya hifadhi utashughulikiwa.
Akizungumza jana kwenye mkutano wa mwaka wa chama tawala cha Kihafidhi, Braverman amesema wale watakaopatiwa hifadhi watabaki kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki, kuliko kurejea Uingereza.
Aidha makundi ya kutetea haki za biaadamu yamesema mpango huo hauwezekani na ni unyama kuwapeleka watu maelfu ya maili mbali kwenye nchi wasiyotaka kuishi.
Chanzo DW
Leave a Reply