Whats good, whats good wanangu wa faida, Kama kawaida haina kupoa wala kuboa. Kwenye segment yetu ya UniCorner, tunakusogezea story zinahusu maisha ya vyuoni ili kuweza kujifunza na kuelimika mawili matatu ama nini.
Kila mwanachuo anayehitimu anakuwa na ndoto ya kupata kazi tu mara baada ya kumaliza elimu yake ya juu na kama tunavyojua wanafunzi wengi wa vyuoni wanasoma kwa kutegemea mkopo kutoka serikalini hiyo inasababisha wanavyuo wengi kuwaza kupata kazi mapema ili kuweza kulipa mkopo.
Licha ya kuwaza kupata kazi mapema baada ya kuhitimu, vilevile wanafunzi wamejawa na fikra au mtazamo wa kupata matokeo mazuri ambayo yatamsaidia kupata kazi kwa haraka zaidi.
Katika soko la ajira inakuwa tofauti na mtazamo wa wanavyuo ulivyo kwani soko la ajira limekuwa na wahitaji wengi kuliko nafasi zenyewe za kazi, hii inatokana na makampuni mengi kuhitaji watu ambao wazoefu katika ujuzi flani kwa zaidi ya miaka kadhaa na wahitaji wa ajira wengi hawana huo ujuzi.
Pia waajiri wa ajira mbalimbali wanahitaji mfanyakazi ambaye ana ujuzi zaidi ya kitu alichosomea, mfano ujuzi wa kuzungumza lugha zaidi ya moja, matumizi ya kompyuta ili kupunguza gharama za kuajiri watu wengi katika kampuni na hivyo kupelekea soko la ajira kuwa gumu kwa wanafunzi wanaohitimu.
Vilevile asilimia kubwa ya watafutaji wa ajira hawako na uwezo wa taaluma sawa na walichosomea, hii inatokana na wahitimu wengi kuamini alama zao za juu kwenye matokeo (GPA) zikiwa nzuri wanaweza kupata kazi sehemu yoyote ilihali kuwasilisha taaluma yake kwa vitendo hawezi na hali hiyo husababisha kukosa nafasi katika soko la ajira.
Aidha maendeleo na ukuaji wa sayansi na teknolojia inachangia pia kukosekana kwa ajira hususani kwa wahitimu wa mara ya kwanza kuingia kwenye ajira kwani kampuni nyingi zinakuwa kwa kasi kutokana na ukuaji wa teknolojia hivyo kupelekea matumizi makubwa ya mashine katika kazi zao kama mbadala wa kuajiri watu.
Baadhi ya viongozi pia wametoa sababu za kuwa na ajira chache kwa wahitimu ambapo wamesema tatizo la ajira nchini linatokana na mfumo wa elimu kupitwa na wakati hivyo kuna hatua zinafanywa kuleta mabadiliko katika mfumo wa elimu ili kuwawezesha vijana kujiajiri au kuajiriwa.
Mfumo uliopo hauwafundishi wahitimu ujuzi wala stadi zozote za kujitegemea kimaisha, badala yake umelenga kumuwezesha mwanafunzi kutoka ngazi moja kwenda ngazi inayofuata; Mfano mwanafunzi akimaliza darasa la saba akiwa na miaka 13, mfumo utakuwa umemfanya amalize akiwa na maarifa ya historia au jiografia na akimaliza sekondari mambo ni yale yale pia.
Mwanafunzi anamaliza shule bila ya kuwa na maarifa, ujuzi wala stadi za maisha, hivyo akikwama katika ngazi moja ni ngumu kusimama katika hatua nyingine ya maisha ya kuweza kujitegemea au kujiajiri.
Mfumo uliopo sasa nchini Tanzania unaanza kutoa ujuzi mpaka mtu afike chuo kikuu au vyuo vya ufundi. Na hivyo kupelekea wengi kumaliza chuo bila ajira wala uwezo.
Pia tumechukua jitihada mbalimbali za kuboresha mitaala ya elimu ili mitaala inayotolewa iendane na mahitaji ya wakati huu na kuwezesha vijana kupata ajira.
Oooooooh! Haya haya anza kuchakalika sasa mjini hakuna kazi huku hahaha! Jokes so chakufanya ni kupambana kabla hujatoka katika kuta za chuo. Hatuna cha ziada Zaidi ya tukutane tena next week katika segment yetu pendwaaa!!!.
Leave a Reply