Ufugaji wa samaki na faida zake

Ufugaji wa samaki na faida zake

Na Habiba Mohammed

 

Ebwana mambo vipi watu wangu wa nguvu? It’s another Friday kwenye jarida la Mwananchi Scoop. Katika segement ya biashara leo tunakuletea  ujanja wa kujifunza fursa mbalimbali ili kutengeneza mkwanja na hapa tunazungumzia biashara ya ufugaji wa samaki na faida zake.

 

Kama inavyofahamika Tanzania tumebarikiwa bahari, mito, maziwa na mabwawa yanayotupatia kitoweo hichi cha samaki ila changamoto kubwa iliyopo ni uchache wa upatikanaji wa samaki kwa idadi ya watu waliopo. Leo tutapeana madini namna ya kufuga samaki nyumbani  na kuchukua nafasi katika soko la samaki. Ungana nasi kujifunza zaidi.

 

MBINU MUHIMU WAKATI WA UZALISHAJI WA SAMAKI

 • Mfugaji anatakiwa awe na shauku na dhamira ya kweli ya ufugaji.
 • Kufanya tathmini ya rasilimali alizonazo kwa ajili ya mradi wa ufugaji wa samaki.
 • Chanzo endelevu cha mtaji kwa ajili ya mradi.
 • Hulka ya uvumilivu na kuthubutu.
 • Tathmini ya soko la bidhaa za samaki.
 • kujipatia maarifa ya msingi ya ufugaji wa samaki

 

 

MTAJI WA KUANZA BIASHARA YA UFUGAJI SAMAKI

 • Vifaranga vya samaki ni Tsh500. Sasa wewe utaamua uanze na wangapi kama ni 10 au 15 au zaidi.
 • Bwawa na eneo la kufugia Samaki. Hapa kwenye bwawa utaangalia wingi wa samaki ambao unataka kuanza nao. Watu wengi wanaofuga hutumia bwawa la urefu 20m, upana 15m na kina 1.5m.
 • Chakula cha samaki kinategemea na wingi wa samaki wako ila hupendelea kula nyama ya kusaga nk.

 

 

SIFA ZA ENEO LA KUFUGIA SAMAKI

 • Eneo la kufugia samaki linatakiwa liwe na maji ya kutosha kwa mwaka mzima.
 • Eneo la kufugia samaki linatakiwa liwe na udongo unaoweza kutuamisha maji.
 • Eneo zuri la kufugia samaki ni kuwa eneo lisiwe na historia ya mafuriko, kwa kuwa mafuriko yakitokea samaki waliokuwa bwawani wataondoka na maji na bwawa litafunikwa na udongo.
 • Eneo zuri la kufugia samaki ni lile linalofikika kwa urahisi.
 • Eneo la kufugia samaki pia linatakiwa kuwa ni eneo lenye amani na utulivu na watu wenye kuelewana.
 • Kuwa na soko la bidhaa.
 • Kuwa na umiliki wa ardhi wa uhakika.

 

UTENGENEZAJI WA BWAWA LA SAMAKI

 Zipo namna mbalimbali za utengenezaji wa bwawa la samaki, kulingana na aina ya bwawa lenyewe, hali ya uchumi, uwingi wa samaki watakaofugwa pamoja na aina ya samaki watakaofugwa. Zifuatazo ni aina za mabwawa ya kufugia samaki.

 

1.Bwawa la kuchimba udongo bila kujengea "Earthen Pond”

 1. Bwawa la kuchimba udongo na kujengea kwa matofali, simenti na zege.

 

UANDAAJI NA UPANDIKIZAJI WA VIFARANGA AU MBEGU ZA SAMAKI KATIKA BWAWA LAKO

Kabla ya kuvisafirisha vifaranga kutoka kwenye bwawa wanaloishi ni vyema vikatolewa na kuwekwa kwenye vibwawa vidogo vidogo kwa muda wa kati ya saa 24 hadi 72 (kutegemeana na umbali wa safari) bila chakula.

Wakati wa kupandikiza mfugaji anatakiwa akifika asivimwage vifaranga kwenye bwawa bali anatakiwa kuyaruhusu maji yaliyobeba vifaranga yabadilishane ujoto na maji yatakayopokea vifaranga. Hapa mfugaji anatakiwa kuliweka kontena au chombo alichobebea vifaranga kielee kwenye maji anayotaka kufugia kwa muda wa dakika kati ya 30 hadi 35, baada ya hapo chombo kilicho na vifaranga kifunguliwe na kiinamishwe ili maji hayo yaweze kukutana na yale yaliyoandaliwa kwa ajili ya kufugia na hapo ataruhusu vifaranga kuingia wenyewe kwenye

bwawa husika.

Iwapo utafika na kuvimwaga vifaranga kwenye bwawa jipya bila kufuata utaratibu huo wa kitaalamu basi tofauti ya ujoto wa maji kati ya chombo kilichosafirishiwa vifaranga na bwawa unaweza kusababisha vifaranga wote kufa kwa muda mfupi, kitaalamu wanasema kuwa vifo vya vifaranga hivyo vinasababishwa na mshituko wa joto.

Jambo lingine la kuzingatia ni kuwa uandaaji na usafirishaji wa vifaranga ni vizuri ukafanywa muda ambao hali ya hewa inakuwa na ubaridi. Muda unaopendekezwa zaidi na wataalamu ni asubuhi au jioni kwa sababu muda huo samaki wanakuwa na uwezo wa kuhimili misukosuko ya safari tofauti na hali ya hewa inapokuwa ya joto.

 

ULISHAJI NA UTUNZAJI WA SAMAKI BWAWANI

 • Samaki wapewe chakula angalau mara 2 kwa siku (saa 3-4 asubuhi na 9-10 jioni) /hewa ya kutosha.
 • Kuwapa vyakula tofauti kutegemeana na silka ya aina ya samaki unaowafuga.
 • Kuna samaki wanaofaidika na vyakula vya nyama nyama kama vile kambale na sangara (hawa hawali pumba) na kuna samaki wengine kama sato wanakula vyakula mchanganyiko wa nyama na mboga mboga na wapo wengine wanaokula vyakula vyenye asili ya mimea tu “carps.”

TABIA ZA ULAJI WA SAMAKI

 • Samaki wanaokula nyama, (sangara na kambale)
 • Samaki wanaokula mimea ‘carps’
 • Samaki wanaokula vyakula mchanganyiko (nyama na mimea) kama perege, sato na mwatiko (samaki wa maji chumvi)

MUONGOZO WA MAHITAJI YA VIINI LISHE VYA SAMAKI Wanga 20-25%

Mafuta 10-15%

Vitamin 1-2%

Madini 1-2%

Protini 18-45% na maji

Pia fahamike kuwa wakati tunazungumzia viwango vya maji vinavyohitajika kwa wanyama wengine wafugwao, hitaji la maji kwa samaki ni ubora wa maji anayofugiwa na sio wingi wake.

TARATIBU ZA ULISHAJI WA SAMAKI

Umri (Wiki)         Uzito (gm)      Kiasi cha chakula kwa siku(gm)

1-2                          5-20                    1gm

2-3                        20-50                    2gm

3-5                        50-110                   3gm

5-7                       110-200                  4gm

7 mpaka mavuno 200gm na zaidi     5gm

MASOKO YA SAMAKI

 • Soko la awali, hili ni soko la moja kwa moja kutoka kwa muuzaji ambaye ni mfugaji kwenda kwa mlaji,
 • Soko la kati, katika soko hili kwa kawaida kunakuwa na mtu wa kati ambaye ananunua samaki kwa mfugaji kwa lengo la kwenda kuwauzia walaji.
 • Soko la kimataifa, hili ni soko linalofanyika nje ya nchi (baina ya nchi moja na nchi nyingine)

FAIDA YA UFUGAJI WA SAMAKI

 • Kupata kitoweo
 • Kujiajiri na kuajiri watu
 • Kuwa na soko endelevu bila kizuizi cha hali ya hewa kwa mfano kiangazi na masika

Tuambie mtu wangu? Je ungependa kujaribu biashara hii? Tukutane wiki ijayo kwa tips zingine za biashara.


Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Detricia Pamba

A Digital Journalist, Content Creation Executive at Mwananchi Communications Ltd and Chief Editor of Mwananchi Scoop. I'm also writes stories around Technology, every Wednesday on Mwananchi Scoop. My other famous segments on Mwananchi Scoop include LISTI and WHO’S HOT.


Latest Post