Tugeuze mitandao ya kijamii kuwa fursa

Tugeuze mitandao ya kijamii kuwa fursa

Ni ukweli uliyowazi kuwa dunia kwa sasa inakwenda kasi, na teknolojia inazidi kuimarika watu wanahabarika kupitia mitandao ya kijamii.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara zinazofanya vizuri katika matumizi ya mitandao ya kijamii. Na hii inachagizwa na ongezeko la watumiaji wa simu janja na huduma ya mtandao (intaneti) nchini.

Taarifa ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inasema watumiaji wa intaneti mpaka kufikia Juni 2021 walikuwa milioni 29 sawa na asilimia 49 ya Watanzania.

Mitandao hii si tu majukwaa ya kimawasiliano, bali ni fursa katika ulimwengu wa leo ya kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla endapo itatumika vizuri.

Licha ya kuwa na idadi kubwa ya watumiaji wa huduma za intaneti na simu janja, lakini matumizi ya mitandao ya kijamii yameendelea kuwa kitendawili kwa Watanzania wengi.

Wapo ambao wamekuwa wakiitumia mitandao hiyo kwa namna sahihi ambayo imekuwa ikiwanufaisha kama vile kibiashara, kikazi na kielimu na wale ambao wamekuwa wakiitumia ndivyo sivyo.

Katika miaka ya hivi karibuni, kumeshuhudiwa kukithiri kwa matukio ya upotoshwaji wa taarifa, wizi mitandaoni, usambazaji wa maudhui yasiyo na maadili (picha na video za utupu na lugha za matusi) na udhalilishaji yanayofanywa mitandaoni.

 

 

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na utoaji wa elimu ya matumizi sahihi ya kidijitali (DA4TI), Peter Mmbando wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo vijana katika masuala ya usalama wa kidigitali alisema katika karne ya sasa ipo haja vijana kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo katika mitandao ya kijamii kuliko kuitumia vibaya.

“Tunachotaka kufanya sisi ni kuwaelimisha vijana kufanya matumizi yenye tija katika mitandao, leo tupo hapa kuwaeleza vijana kuwa wanaweza kupata kazi kwa kuandika makala mbalimbali na kutengeneza video nzuri zinazohusiana na mazingira na kupinga unyanyasaji na kisha kuweka katika mtandao,” alisema

Hata hivyo alifafanua kuwa biashara za kimtandao zinakosa uaminifu kwa kiasi kikubwa kutokana na baadhi ya watu kuitumia kutapeli watu kwa kutangaza biashara bandia na kuwaibia.

Aliongeza kuwa ili kupunguza utapeli katika mitandao shirika lao limeamua kutoa elimu kwa kundi hilo la vijana juu ya namna ya kuepukana na wizi mtandaoni.

“Tumeanza na vijana hawa tutaendelea kwenda shule mbalimbali na kuwaeleza kwamba wanaweza kutumia mtandao kwa kusoma, kutafuta kazi na kuelimisha jamii hasa kuwa na maadili, pia wanatakiwa kujua siyo kila kitu wanaweza kuweka mitandaoni bali unapaswa kuchuja na kujiridhisha kabla ya kuweka habari mitandaoni,” alisema

Ni kweli mitandao ina umuhimu mkubwa ingawa ina haribiwa na watu wachache wasiojua umuhimu wake.

Kutokana na vitendo hivyo, vijana nchini wanashauriwa kuacha tabia ya kutumia vibaya mitandao ya kijamii na mifumo ya kidijitali badala yake wanahimizwa kuitumia kutafuta fursa mbalimbali za mafunzo na biashara ili kujikwamua kiuchumi.

Tuelewe kuwa wapo baadhi ya watu wamekuwa wakifanya utapeli na kusambaza picha zisizofaa katika mitandao wanashindwa kutambua kuwa zipo fursa mbalimbali za kibaishara ambazo zikitumika zinaweza kumuongezea mtu kipato.

Tunaweza kutumia mitandao kwa kutangaza biashara na bidhaa mbalimbali na kupata wateja wa kutosha watakaonunua hatimaye muuzaji kupata fedha za kujikwamua.

Tuache kabisa kupoteza muda kufatilia masuala ya udaku na mambo mabaya katika mitandao tuamke sasa kwa kuitumia vizuri kwani baadhi ya matajiri wakubwa dunia unaowajua wamefika hapo walipo kwa kuitumia mitandao vizuri.

Kijana mwenzangu amka sasa na achana na matumizi mabaya kwenye mitandao bali itumie kwa malengo ya kunufaika.

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags