Taarab katika ubora wake haikuhitaji promo na kelele nyingi kwenye vyombo vya habari. Taarab ilijiuza kwa sababu ina njia zake ambazo ni za kipekee sana. Ni muziki wenye dunia yake ya muziki.
Kuna mtandao wa taarabu usioingiliana na jamii ya muziki mwingine. Na zaidi ni muziki ambao hauhitaji kutoa wimbo mpya ili kuvutia mashabiki. Maisha ya kila siku ya mashabiki ndiyo hufanya shoo zao ziwe na uhai.
Yaani kama kuna mwanamke kaiba bwana wa mtu. Mwenye bwana hakosi wimbo ambao utakuwa kama kijembe kwa huyo mwizi wake. Ndivyo ilivyo na kwa mwizi wake pia hakosi wimbo wa kijembe kwa aliyemuibia.
Taarabu ndiyo muziki ambao aliyetenda na mtendwa wote hawakosi wimbo wa ujumbe wake. Na kama ni majirani ndipo hapo mtaani kelele zitakuwa nyingi za muziki wa vijembe. Kama siyo majirani basi watakutana kwenye shoo zao.
Kama ni Lango la Jiji ama Max Bar Ilala. Kama siyo Travertine Mapipa. Basi ni DDC Kondoa. Hayo ndiyo maeneo yenye mashabiki wa muziki huu. Wataenda na wapambe wao kurushana roho. Ukumbi utajaa kambi mbili zenye fujo.
Kambi hii watatoa pesa waimbiwe wimbo wa ‘Kinyago cha Mpapule’ wa Mwanahawa Alii. Na kambi ile kule pia wataweka pesa waimbie ‘Paka Mapepe’ kama siyo ‘Yatakushinda’. Zote hizo siyo nyimbo mpya ila ujumbe unawahusu.
Hii ndiyo iliyofanya taarabu isihitaji sana promo. Bali maisha ya uswahilini kwetu ndiyo yaliyofanya mashabiki waende katika kumbi za taarabu. Kupigana masingi na vijembe na kuchambana kwa mtindo wa kuvimbiana ukumbini.
Wimbo ukianza tu, shabiki atainuka toka nyuma ya ukumbi. Kashikilia noti ya elfu 10 akiizungusha hewani kwa vidole viwili. Akiwatambia wale wa kambi ya pili kwamba hilo linawahuu. Nao watalipiza kwa wimbo unaofuata.
Hii ilifanya bendi ziendelee kusimama imara bila presha ya promo. Utaratibu ni kwa mashabiki wanaotuza kuweka pesa katika kapu lililo mbele kando ya msanii anayeimba. Maana yake ni pesa ya wasanii wote walioshiriki kwa siku hiyo.
Ndiyo maisha ya Mwanahawa Alii. Miaka yote akiishi Unguja. Atalipiwa nauli ya boti kutoka Unguja kuja Dar. Atalipiwa na hoteli kila mwisho wa wiki. Angeshiriki na wenzake katika shoo kisha Jumanne angerudi zake Zenji.
Pamoja na taarabu kuwa na mashabiki ‘loyo’. Kuna shida ambayo hiyo ndiyo inafanya wasanii wengi wa taarabu kuwa na maisha tofauti na majina yao. Maisha ya shida hivi. Maisha yasiyoakisi ukubwa wa majina yao.
Kwanza bendi ya taarabu inahitaji watu wengi ili ikamilike. Ndiyo muziki ambao una waimbaji zaidi ya watano kwa bendi moja. Hii inafanya hata mgawanyo wa mapato kuwa mkubwa. Na ndiyo sababu ya pesa za kutuzwa msanii zinawekwa kwenye kapu moja.
Lakini pia taarabu nyimbo zake ni ndefu sana. Hii hufanya muziki huu kukosa nafasi katika vituo vya radio na runinga. Kwa sababu kwenye hizi radio na runinga muda ni mali. Ukiwa na wimbo mrefu sana unakosa kuchezwa. Na hii ipo hata kwa dansi.
Sasa kukosa nafasi katika ‘platifomu’ kuna mapato wanayakosa wasanii kama mirabaha na matangazo ya biashara kwa msanii husika. Na hii ni hata kwenye shoo za mchanganyiko watu wa taarabu hawana nafasi.
Mfano shoo kubwa zenye mchanganyiko wa wasanii, bendi za taarabu hazipewi nafasi. Siyo kwamba hakuna mashabiki wake bali ni suala la muda. Nyimbo zao zinachukua nafasi kubwa kiasi kwamba ni vigumu kupokezana jukwaani kwa wakati.
Pia bendi za taarabu ni vigumu kupata shoo za nje ya mji ama nje ya nchi. Sababu ikiwa ni lile nyomi la wasanii wa bendi na gharama kuwa kubwa. Matokeo yake shoo nyingi hufanyia maeneo yale yale ya siku zote. Kupeleka bendi ya taarabu nje ya nchi ni gharama kubwa.
Na sasa imefika wakati, wanamuziki na wasanii wa taarabu hawajui wafanye nini. Wasimame upande gani, wafanye aina gani ya muziki. Maana ni zege la dansi, singeli, mnanda na Bongo Fleva.
Wameshindwa kukishawishi kizazi cha sasa kuupenda muziki wao wa taarabu. Wasanii wengi ni walewale, mashabiki walewale. Hakuna uzao mpya kwa wao na mashabiki wao. Na hili ni tatizo kuu kwa muziki huu.
Pamoja na ubora wa sauti na vyombo, lakini shida kubwa ipo kwenye muziki wa taarabu linapokuja suala la kujiuza kwa kizazi cha sasa. Hawataki kwenda na dunia ya sasa bado wanaishi katika mtazamo wa kale sana.
Video za nyimbo zao hazina tofauti na video za ‘besidei’. Ubora na mazingira yake ni ya dunia ya kale. Aliyekufa miaka ya 2000, akifufuka na kukutana na video ya muziki wa taarabu ya 2024. Ataamini dunia bado ipo mwaka 2000.
Kwa dunia ya sasa na aina ya ‘shuting’ wanazofanya ni vigumu sana watoto wa dunia ya Mbosso na Konde Boy na Amapiano yao kuwaelewa. Taarabu inapaswa kwenda na wakati ama kwenda na maji.
Pesa ipo mitandaoni. Taarabu inataka wimbo mrefu. Sasa ni kuchagua kufuata misingi ya taarabu ama kufuata misingi ya pesa. Maana misingi ya pesa ipo katika ‘digital platform’. Huko ndiko iliko pesa siyo kwa Wadosi Kariakoo kama zama zile.
Mbaya zaidi hakuna kizazi kipya cha wasanii wapya. Ni walewale wengine wanaokoka kumrudia Mungu, baadaye tena wanaamua kuirudia pesa ilipo. Lakini uzao mpya wa wasanii hakuna na uzao mpya wa mashabiki hakuna.
Tunaona Bongo Fleva ilivyojitafuta. Kutoka kuonekana muziki wa kihuni mpaka sasa wasanii wake kuwa karibu na Ikulu kuliko mawaziri. Kwa nini kwa taarabu iwe vigumu? Ni lazima wasanii wa taarabu wabadili mtazamo.
Hakuna Mwanahawa mpya, wala Sabaha mpya. Simuoni Khadija Yusuf mpya wala Leila Khatibu wa kizazi kipya. Aliyetakiwa kuwa Khadija Kopa wa dunia hii ya sasa amekuwa Lady Jaydee wa kizazi kipya. Namuongelea Zuchu.
Tunaona kutoka Diamond, Konde Boy, Rayvvany mpaka D-Voice. Lakini kwa watu wa taarabu tunamuona Mzee Yusuf na Mzee Yusuf wa Mzee Yusuf. Mzee Yusuf anaondoka kisha anarudi Mzee Yusuf tena. Hakuna matoleo mapya.
Matokeo yake wasanii wa taarabu wanaishi kwa nguvu ya mashabiki wa miaka ileile. Kwa mtindo uleule wa zamani. Wakati Mondi anakula pesa za You Tube, Mzee Yusuf anawaza pesa za viingilio vya Lango la Jiji.
Dunia ya sasa inataka nyimbo fupifupi. Iwe radio, iwe shoo, iwe digital platform, ama runinga. Kwa sababu muda ni pesa. Nyimbo za mfumo wa Fanco Lwambo Makaidi hauna nafasi. Watu wanataka vitu rahisi na vifupi. Radio na runinga wanataka nyimbo fupi ili wapate muda wa matangazo. Digital platform wanataka nyimbo fupi ili watu wamudu kutazama na mabando yao. Kwenye shoo wanataka nyimbo fupi ili isichoshe watu.
Hali hii inaenda tofauti na utamaduni wa muziki wa taarabu. Bahati mbaya wakati taarabu imeganda palepale dunia ipo spidi kali sana ikihama. Ni wakati wa ama kwenda na dunia upate pesa. Ama kwenda na utamaduni ubaki na njaa zako.scriptions
Leave a Reply