Simulizi: Sehemu ya tatu (3) Kwa Udi na Uvumba...!

Simulizi: Sehemu ya tatu (3) Kwa Udi na Uvumba...!

Sehemu o3

Daladala la Mwananyamala lilipofika Hilda alipanda, Panja naye hakubaki nyuma, akajitoma garini. Bado alikuwa ni mwanamume wa ‘kutesa.’ Alipoingia ndani ya daladala hilo alikuwa na shilingi laki moja na vikorokoro vichache mfukoni, achilia mbali milioni moja na kidogo zilizobaki nyumbani, hizo zikiwa ni masalia ya zile milioni tatu.

Akabahatika kuketi siti moja na Hilda, roho yake ikasuuzika. Hata hivyo kwa jinsi mazingira yalivyokuwa ndani ya daladala hilo, Panja hakuweza kuiweka bayana dhamira yake kwa Hilda. Alichoambulia ni jina na kituo atakachoteremkia.

“Na mimi nateremkia hapohapo Kinondoni,” Panja alimwambia.

“Naishi Mtaa wa Sekenke.”

“Mie niko Mtaa wa Togo,” Hilda alisema.

Walifahamiana zaidi baada ya kuteremka. Na usiku wa siku hiyo ukawazalishia uhusiano wa mapenzi wakiwa pamoja nyumbani kwa Panja.

Siku ya pili walirudia.

Ya tatu wakanogewa.

Hatimaye Hilda akawa ‘mke.’ Na akilini mwa Panja, kati ya wanawake wote waliowahi kumchojolea nguo, ni huyu Hilda aliyemtoa jasho!

**********  

MIEZI miwili ilipita, sasa Hilda akiiona dunia tamu kuliko kile kipindi alipokuwa akiishi peke yake. Ni kipi alichokosa? Kama ni pesa, lilikuwa ni kosa la jinai ndani mwao kukosekana   shilingi laki mbili, tatu au zaidi ya hizo. Jinsi zilivyopatikana, hakujua. Kwa jumla hakujua bwana wake alikuwa akifanya kazi gani iliyomwingizia pesa. Na ilipotokea akahoji japo kwa mbali, hakupata majibu sahihi. “Napata tenda ya kuendesha daladala…” au “nafanya kazi kwenye benki moja ya nje…” au “Niko bandarini…” na kadhalika na kadhalika.

Hata hivyo, Hilda hakujali kupewa majibu tofauti, alijali kupata kile ambacho mwili wake kiliuhitaji. Ndiyo, alijali kuufaidi mwili wa Panja ambao kama si kumkanda basi ulimkaanga pindi kitanda kilipowalaki sanjari na pesa lukuki za matumizi, ambazo Panja alimpa.

Ndipo ikaja siku ambayo Panja alimwambia Hilda kuwa alitarajia kwenda Morogoro.

 “Morogoro?” Hilda alihoji kwa mshangao. “Kufanya nini Morogoro?”

“Kuna kazi kidogo. Nitarudi kesho au keshokutwa. Lakini hiyo itatokea kama mipango yangu itasababisha nishindwe kurudi leo hii.”

Hilda, kama kawaida yake, hakujali. Si mara moja au mbili ameshalala peke yake hadi alfajiri arudipo Panja. Siku nyingine alijikuta akipitisha saa arobaini na nane bila ya kumwona. Taarifa hii ilikuwa haitofautiani na taarifa nyingine nyingi alizokwishampa.

Alichofanya ni kumdhibiti kitandani kwa takriban nusu saa, akimuaga kwa namna waliyoizoea, shahidi wa kuagana huko wakiwa ni mijusi wadogo wawili waliokuwa darini. Na Hilda aliamini kuwa kama ilivyokuwa katika safari zote zilizopita, Panja angerejea na pesa, tena pesa nyingi.

 ************  

NI baada ya nusu siku ndipo Panja alirejea. Na hakurudi hata na sarafu moja, zaidi ni uso wake ndio uliobeba hasira kali iliyodhihirika hata machoni mwa Hilda ambaye alizoea kuuona uso huo ukiwa umechangamka. 

Usiku mambo yalizidi kuwa mabaya kwa Hilda. Hakuipata huduma aliyozoea kupewa na Panja. Akajaribu kutumia zile mbinu zake zote, mikono ikitalii kila sehemu na ulimi ukiteleza kila palipostahili kwa namna aliyoamini kuwa ingeyaamsha ‘mashetani’ ya Panja ambayo siku hiyo yalilala usingizi mzito.

Haikusaidia!

Mtoto wa kike akashangaa, na ndipo alipoamua kumtupia lile swali: “Una nini leo?”

Alikuwa na sababu ya kumuuliza hivyo. Kwa kawaida, muda kama huo, usiku kama huo, Panja huwa akimsumbua, akihitaji kwa mara nyingine, na Hilda apende asipende, angemtimizia matakwa yake.

Lakini usiku huu hakuwa yule Panja wa siku zote, Panja ambaye hakuwahi kudai kuwa ana uchovu uliosababishwa na mahangaiko ya mchana kutwa.

 Huyu alikuwa ni Panja mwingine, Panja ambaye hakuonesha kufurahishwa na chochote kati ya aliyofanyiwa na huyu mpenziwe. Na kutokana na uchungu uliomjaa moyoni, aliamua kulitoa lile lililomsonga na kumfanya aonekane kiumbe wa ajabu kwa Hilda.

 “Sikia Hilda,” alitamka kwa sauti ya chini. “Kama kuna safari ambayo ilikuwa mbaya kwangu basi ni hii ya leo.”

 Hilda alishtuka. “Hii ya Morogoro?” alimuuliza.

 “Hiyohiyo.”

“Ilikuwa mbaya ki-vipi?”

 “Sikurudi na pesa.”

 “Hukurudi na pesa?” mshangao ulidhihirika katika sauti ya Hilda. “Hilo ndio limekunyong’onyesha ivo? Siku hazifanani, mpenzi. Kuna siku mtu unapata pesa na kuna siku ambazo mambo yanakuwa kama ivo tena.”

 “Usemavyo si uongo, lakini hayo siyo ya kutokea kwa upande wangu.”

 “Ki-vipi?”

 “Uelewe maana ya kukwambia kuwa sikurudi na pesa,” Panja alisema kwa msisitizo mkali japo sauti yake ilikuwa ya chini. Akaongeza: “Siyo kwamba pesa sikupata. Nimezipata, lakini sikurudi nazo. Mpaka hapo tuko pamoja?”

 Hilda hakuwa mwepesi wa kuelewa. Maneno hayo ya Panja bado yalimwacha njiapanda. Akashusha pumzi ndefu kabla hajauliza, “Una maana kipi kilichotokea hadi ukapata pesa na hukuja nazo? Umeporwa na majambazi?”

 Ilimbidi Panja atumie juhudi za ziada na kufanikiwa kukizuia kicheko kilichomjia kufuatia swali hilo la Hilda. Moyoni akamsikitikia kwa kutoijua sababu ya yeye kutorudi na pesa, na zaidi, kwa kuishi na mtu asiyekubalika katika jamii iliyostaarabika.

 Jambazi!

 Alimtazama kwa sekunde chache kisha, kwa sauti ndogo, akasema, “Tulia. Najua, kuna jambo ambalo hulijui, na sasa ni vizuri ukilijua.”

 “Ni nini? Mbona sikuelewi?” sauti ya Hilda ilikuwa ya mchanganyiko wa woga na mshangao.

 “Ni vizuri ukiifahamu kazi yangu,” Panja alisema kwa unyonge.

 “Kazi yako?” Hilda alimdaka.

 “Tulia. Mbona una papara?”

 

Hilda akanywea.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags