Serikali yaahidi kushirikiana na sekta binafsi kukamilisha miradi ya maji kwa wakati

Serikali yaahidi kushirikiana na sekta binafsi kukamilisha miradi ya maji kwa wakati

Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi amesema kuwa Serikali itashirikina na sekta binafsi katika kuhakikisha miradi ya maji inakamilika ndani ya muda uliopangwa ili kuondoa changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo hapa nchini.

Pia Mahundi ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha uwepo wa maji safi na salama kwa wote ili kufikia malengo ya Milenia ifikapo mwaka 2030.

Hayo ameyaeleza leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa wadau mbalimbali wa maji  na usafi wa mazingira uliolenga kujadili namna ya kuboresha huduma za utoaji maji safi na salama pamoja na usafi wa mazingira, mkutano ulioandaliwa na Shirika la WaterAid.

Mahundi anasema hali ya upatikanaji wa maji kwa sasa umefikia asilimia 72.3 kwa vijijini na asilimia 86 kwa mjini huku malengo ya Wizara ni kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi aliyoibainisha ikiwemo kushirikiana na sekta binafsi kwa lengo la kukamilika ndani ya muda uliopangwa.

“Kwa takwimu hizo bado wadau tuna kazi kubwa ya kufanya katika kufikia malengo ya Milenia hususani lengo namba sita la kuhakikisha kuwa maji safi na salama yanapatikana kwa watu wote ifikapo mwaka 2030.

“Katika lengo hili pia wadau kama WaterAid wana mchango mkubwa wa kuhakikisha adhma ya wizara inafanikiwa na tupo pamoja nao,”anasema.

Amesema kwa sasa Serikali inajielekeza kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa yenye vyanzo vya maji vya uhakika na itakayohudumia idadi kubwa ya wananchi.

Pia kuongeza nguvu katika utunzaji wa vyanzo vya maji na kufanya juhudi kubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

“Pamoja na hayo vilevile tunalenga kuongeza msukumo katika utekelezaji wa majitaka na usafi wa mazingira mjini na vijijini na kuongeza uwajibikaji kwa watumishi wote walio chini ya Wizara ili kutoa huduma bora kwa gharama nafuu,”anasema.

Aidha, anaema Shirika la WaterAid limekuwa likishirikiana na serikali katika kuongeza upatikanji wa huduma za maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi (WASH).

“Serikali inatambua mchango mkubwa wa shirika hili na asasi zingine za kiraia ambazo tumekuwa tukishirikiana nazo katika sekta ya maji. Kuna msemo ukitaka kwenda haraka nenda peke yako lakini ukitaka kwenda mbali nenda na wenzaki serikali inataka kwenda mbali hivyoimechagua kwenda na wenzetu kama WaterAid ili tuweze kufikia adhima yetu,”anasema Mahundi. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la WaterAid, Anna Mzinga anasema wataendelea kutoa ushirikiano kwa serikali na wananchi ikiwemo wale makundi maalumu ili kupata huduma stahiki zenye tija endelevu za huduma za maji safi na mazingira.

“Shirika lina maono ya kuhakikisha watu wote wanapata huduma ya maji safi ya uhakika, vyoo bora na usafi binafsi wenye viwango na uhifadhi wa mazingira hususani katika vyanzo vya maji,”anasema.

Mzinga anasema hadi sasa wamefanikiwa kuwafikia wananchi zaidi ya milioni nane wanaoishi maeneo ya mjini, pembezoni mwa miji na vijijini.

Anasema malengo ya mkutano huo ni kushirikishana ujuzi na wadau wenzao waliofika ili kujenga maarifa yenye tija katika kuboresha utendaji wa utoaji wa huduma zao kwa jamii ya taifa la Tanzania






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags