Rihanna, Harmonize Na Fally Ipupa Walivyotoboa Kibishi

Rihanna, Harmonize Na Fally Ipupa Walivyotoboa Kibishi

Moja ya tukio ambalo limeibua maoni mengi katika mitandao ya kijamii wikiendii iliyopita ni kuhusiana na maneno ya mmoja wa mtayarishaji wa muziki na jaji katika mashindano ya kusaka vipaji vya kuimba BSS, Joachim Marunda 'Master Jay' kumshambulia msanii Alikiba akidai kuwa msanii huyo hajui kuimba live.

Mbali na kusema hivyo, lakini pia ameeleza kuwa ni mbana pua jambo ambalo lilipelekea baadhi ya mashabiki kumshambulia kwa maneno huku akirekebisha kauli yake hiyo kupitia mahojiano yake na Mwananchi akieleza kuwa ubanaji pua siyo tusi ni neno lililoanza kutumiwa na wasanii wa Hip-hop tangu mwaka 2000.

Aidha kwa upande wa Alikiba, naye hakulikalia kimya suala hilo ambapo aliamua kumjibu msanii huyo na kumtaka aache kumfuatilia na kuongelea watu vibaya. King sio msanii wa kwanza duniani kuambiwa hivyo, wapo mastaa ambao wana majina makubwa na wameshawahi kukutana na madongo hayo lakini waliinuka na kuwa bora zaidi.

Fally Ipupa (DR Congo)
Wakati alipokuwa akiondoka kwenye Kundi la Quartier Latin linaloongozwa na Koffi Olomide mwaka 2006, kuanza kazi yake ya muziki kama msanii wa kujitegemea msanii huyo alipokea maoni ya kukatisha tamaa ya kuwa hatokuwa bora kama alivyokuwa katika kundi hilo huku wakikosoa uimbaji wake na kudai kuwa alikuwa akibebwa.
Licha ya kukutana na maoni hayo, lakini kwasasa amekuwa msanii bora ambaye anafanya vizuri kupitia muziki wa Soukous huku akinyakuwa tuzo mbalimbali zikiwemo AFRIMMA, Trace Awards & Festival, EAEA na nyinginezo.

Jennifer Lopez (Marekani)
Mbali na Fally naye mwanamuziki J.Lo amewahi kukosolewa kuhusiana na uimbaji wake, wengi wakidai kuwa msanii huyo hajui kuimba na madai kwamba hutegemea teknolojia kama 'autotune' na playback wakati wa maonyesho ya moja kwa moja.

Lakini pia amewahi kutumia sauti za waimbaji wengine kwenye baadhi ya nyimbo zake kupitia wimbo wa ‘Play’, ambapo sauti ya mwimbaji Christina Milian inasikika zaidi kuliko sauti ya J.Lo, jambo lililozua mjadala mkubwa, licha ya ukosoaji huo, Lopez ameendelea kuwa na mafanikio makubwa katika muziki na filamu akiwa na albamu nyingi sokoni.

Rihanna (Barbados)
Ukiachana na Alikiba kukumbana na changamoto hiyo ya kuambiwa hajui kuimba na kubana pua lakini pia naye msanii kutoka katika Visiwa vya Barbados Rihanna aliwahi kupokea maoni kuhusiana na yeye kutojua kuimba huku wakida kuwa sauti yake haikuwa na nguvu wala ushawishi masikioni mwa watu.

Aidha amewahi kuthibitisha kwamba licha ya ukosoaji wa awali, ana sauti ya kipekee na anaweza kufanikiwa bila kujali vikwazo alivyokutana navyo mwanzoni. Kwa sasa Riri ameendelea kuandika historia kupitia Albamu yake ya mwaka 2016 iitwayo ‘ANTI’ ambayo imeendelea kukimbiza kwa wiki 460 ndani ya chati za billboard 200.

Harmonize
Msanii mwingine ambaye aliwahi kukutana na changamoto hiyo lakini alisimama imara ni Harmonize ‘Konde Boy’ ambapo wakati wa masimango hayo aliwahi kuambiwa kuwa anaiga mtindo wa uimbaji wa aliyekuwa bosi wake Diamond Platnumz.

Hata hivyo, Harmonize alijidhatiti na akaendelea kufanya kazi kwa bidii, akitoa albamu na nyimbo zilizopata umaarufu mkubwa. Ameshinda tuzo nyingi na kujiimarisha kama msanii mwenye mafanikio makubwa Afrika.

Wasanii wengine ambao waliwahi kupata maoni ya kuwa hawajui kuimba ni pamoja na Britney Spears, Wizkid, Davido, T-Pain, Cardi B na wengineo wengi.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags