Rekodi 10 za Rayvanny kwenye muziki

Rekodi 10 za Rayvanny kwenye muziki

Kwa sasa Rayvanny ni miongoni mwa wasanii waliofanikiwa sana katika Bongofleva akiwa ametoa albamu moja, EP nne na kushinda tuzo za ndani na kimataifa kitu kinachompa heshima kubwa mbele ya mashabiki wake.

Safari yake ya muziki ilianzia pale Tip Top Connection kisha WCB Wasafi na sasa katika himaya yake, Next Level Music (NLM), bila kuchoka, bado anaendelea na kazi ya kutoa burudani ya uhakika huku akiweka rekodi nyingi katika muziki. Fahamu zaidi.

1. Rayvanny ni msanii wa kwanza kutoka Afrika kutumbuiza katika tuzo za MTV Europe Music Awards (MTV EMAs), mwaka 2021 alipopanda katika jukwaa hilo akiwa na Maluma wa Colombia waliyeshirikiana katika wimbo, Mama Tetema (2021).

Utakumbuka Diamond Platnumz ni msanii wa kwanza Afrika kushinda tuzo mbili za MTV EMAs katika vipengele viwili kwa wakati mmoja ambapo alifanya hivyo mwaka 2015 huko Milan, Italia.

Hata hivyo, katika tuzo za MTV EMAs 2024 zilizofanyika huko Manchester, Uingereza, Tyla kutokea Afrika Kusini alishinda vipengele vitatu, na hivyo kuandika rekodi nyingine kama mwanamuziki Afrika aliyebeba tuzo hizo nyingi kwa mara moja.

2. Rayvanny ni msanii wa kwanza Afrika Mashariki kusikilizwa (streams) zaidi ya mara milioni 100 katika mtandao wa Boomplay Music, huku Marioo akiandika rekodi kama hiyo ila bila kuwa na albamu wala Extended Playlist (EP).



3. Ni msanii wa kwanza Tanzania kushika namba moja chati za Billboard Mexico Airplay kupitia wimbo, Mama Tetema (2021), ikiwa ni mara ya pili kuingia chati hizo baada ya hapo awali kutamba Billboard Top Triller Global Chart akiwa na Dj Cuppy wa Nigeria.

4. Rayvanny ni wa kwanza aliyetoka kimuziki chini ya WCB Wasafi aliyeweza kutoa EP nyingi ambazo hadi sasa zinafikia nne, Flowers (2020), New Chui (2021), Flowers II (2022) na Unplugged Session (2022).

5. Rayvanny msanii wa kwanza Bongo ambaye amefanya video nyingi na mpenzi wake, Fahyma, wawili hao wamefanya pamoja video sita ambazo ni Kwetu (2016), Natafuta Kiki (2016), Siri (2017), Forever (2023), Habibi (2023) na Mwambieni (2023). 

Katika eneo hili anafungana na Marioo ambaye amemtumia mpenzi wake Paula katika video za nyimbo zake kama kama Lonely (2023), Tomorrow (2023), Sing (2023), Hakuna Matata (2024, Unachekesha (2024) na Tete (2025).

6. Rayvanny ni msanii wa kwanza aliyetolewa na WCB Wasafi kushinda tuzo nyingi za kimataifa. Vanny Boy ameshinda tuzo kama BET (Marekani) 2017, Zikomo (Zambia) 2022, Afrimma (Marekani) 2022, EAEA (Kenya) 2022, DIAFA (Dubai) 2022 n.k.

7. Ni msanii wa kwanza Afrika Mashariki kwa albamu yake, Sound From Africa (2021) kufikisha kusikilizwa (streams) zaidi ya mara milioni 100 ndani ya wiki moja, huku ikiwa albamu pekee Bongo iliyotoka na idadi kubwa ya nyimbo mwaka huo ambazo ni 23.

8. Rayvanny ni msanii wa pili Afrika Mashariki kutazamwa YouTube zaidi ya mara bilioni 1 akiwa ametanguliwa na Diamond, kisha Harmonize. Na hadi sasa hawa ndio wasanii pekee ukanda huo kupata namba hizo, huku Zuchu akitarajiwa kuja kuwa wa nne.

Utakumbuka Diamond ambaye alifikisha ‘views’ bilioni mnamo Juni 2020 hadi sasa ana jumla ya bilioni 2.5 na kushika nafasi ya pili katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara akiwa ametanguliwa na Burna Boy kutokea Nigeria mwenye bilioni 2.7.

9. Ni msanii wa kwanza Tanzania kushinda tuzo za BET zilizoanza kutolewa Juni 19, 2001 nchini Marekani, Rayvanny alishinda mwaka 2017 akiwa ni msanii wa pili Afrika Mashariki baada ya Eddy Kenzo wa Uganda aliyeshinda 2015. 

10. Rayvanny ni msanii wa kwanza kufungua lebo yake, Next Level Music (NLM) akiwa bado chini ya WCB Wasafi, wakati Harmonize na Rich Mavoko walifungua zao, Konde Music Worldwide na Billionea Kid baada ya kuondoka WCB Wasafi.

Hata hiyo, hawa wote kwa sasa lebo zao hazisimamii wasanii wowote wale zaidi ya kazi zao wenyewe, huku aliyekuwa bosi wao, Diamond chini ya WCB Wasafi akiwa na Zuchu na D Voice aliyetambulishwa kupitia albamu yake, Swahili Kid (2023).






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags