Wananchi wa Afrika Kusini wamezua gumzo mitandaoni baada ya kumkataa Chidimma Adetshina kushiriki ‘Miss Afrika Kusini’ kwa kudai kuwa mrembo huyo ni raia wa Nigeria.
Mjadala huo ambao ulizua gumzo katika mitandao ya kijamii ulidai kuwa mrembo huyo sio raia wa Afrika Kusini, hivyo basi hawapo tayari kuwakilishwa na raia wa kigeni katika shindano hilo.
Kutokana na gumzo hilo waandaaji wa mashindano ya ‘Miss South Africa’ walilitolea ufafanuzi suala hilo na kuweka wazi kuwa Chidima ni raia wa nchi hiyo na alizaliwa Soweto na kukulia Cape Town hivyo anayo haki ya kushiriki mashindano hayo.
Naye Waziri wa utamaduni wa Afrika Kusini, Gayto McKenzie aliwataka wanaohusika na mashindano hayo kutoa ukweli unaozua taharuki katika taifa hilo.
“Hatuwezi kabisa kuwa na Wanigeria katika shindano letu la #MissSA nataka kupata ukweli wote kabla ya kutoa maoni lakini tayari inanipa hisia za ajabu.”
Hata hivyo, mrembo huyo bado hajaenguliwa katika shindano hilo hali inayoleta hisia tofauti kwa raia wa nchi hiyo kuwa huenda akaibuka mshindi kwenye fainali ya #MissSA zinazotarajia kufanyika Agosti 10, 2024.
Awali maisha ya Chidima yanaeleza kuwa alizaliwa na kukulia katika kitongoji cha Soweto, Gauteng huku baba yake akiwa ni Mnigeria na mama akitambulika kama raia wa Afrika Kusini, maelezo haya yanamfanya mrembo huyo kuwa na uraia wa nchi mbili.
Leave a Reply