Nyama za pua, ugonjwa unaowatesa wengi

Nyama za pua, ugonjwa unaowatesa wengi

Ugonjwa wa nyama za pua ni neno linalotumika kumaanisha nyama zilizoota katika pua ambazo zinaweza kuwa ni sehemu ya pua ambapo zimekuwa kubwa kiasi cha kuziba pua au ni nyama zisizo sehemu ya pua ila zimeota.

Kwa hiyo nyama za pua ni ugonjwa unayojumuisha kundi kubwa la aina za nyama tofauti tofauti zinazoweza kuota katika pua ambazo zina sababu tofauti tofauti na zinaathiri watu tofauti tofauti katika makundi tofauti ya umri na jinsia.

Kimsingi hizi nyama kila mtu anazo katika ukubwa tofauti tofauti lakini watoto wadogo kutokana na maumbile madogo ya pua, hizi hukua kwa haraka kuliko pua inavyoongezeka matokeo yake hizi nyama huziba mfumo wa hewa wa puani.

Mfumo wa hewa ukizibwa kutokana na nyama kuongezeka kuliko ukubwa wa pua ndo matatizo yanapoanza.

Tunaona tatizo hili kwa siku za hivi karibuni limekuwa likiwasumbua watoto wengi huku wazazi wengi wakishindwa kugundua mapema.

Akizungumza na Jarida la Afya kuhusu tatizo hilo, Daktari bingwa wa koo, pua na masikio kutoka hospitali ya Agakhan, Christopher Mwansasu anasema mara nyingi watoto huwa wanapata nyama za pua ambazo zinaitwa adenoids, ambazo huwa zipo nyuma ya pua katika njia ya hewa inayoelekea kwenye koo la pamoja la hewa na chakula(pharynx).

 

Anabainisha baadhi ya dalili za nyama za pua ni pamoja na  kuwa na mafua ya mara kwa mara, kukoroma, kupumulia mdomo wakati wa kulala ambapo huonekana kwa mtoto kuacha mdomo wazi akiwa usingizini na kustukastuka.

Pia kuhangaika kama mtu anayetafuta hewa wakati akiwa amelala, upungufu wa kusikia au kupatwa na maambukizi ya bacteria katika sikio la kati mara kwa mara, kutokupenda kula au kunyonya, kudhoofika mwili na kuzorota kwa mpangilio wa meno ya juu sehemu ya mbele.

Hata hivyo anasema historia ya ugonjwa huo katika chunguzi zilizofanywa unatokea kwa wingi kati ya watoto wa mwaka mmoja mpaka miaka mitano hadi sita, huku watoto wa miaka mitatu ndo waathirika wakubwa.

“Ni ngumu kusema kwamba tatizo hili kwa watoto limeongezeka au la kwa sababu hatuna takwimu zinazojumuisha na zilizochapishwa katika jamii yetu kufuatilia mwenendo wa huu ugonjwa. Lakini ni kweli  kwa macho ya juu juu upasuaji unaohusu watoto wenye tatizo la nyama za pua(adenoids) unaonekana kuongezeka ambazo inaweza ikawa kwa sababu kama mbili au zaidi.

“Ya kwanza ni kutokana na kuongezeka wataalam wa pua, koo na masikio Tanzania katika miaka 15 iliyopita, hii ikimaanisha uwezo wa nchi kugundua na kulitibu tatizo umeongezeka na kwa namna hiyo ufahamu wa ugonjwa katika jamii yetu unaongezeka kupitia hawa wataalam,” anaeleza Dk Mwansansu. 

 

Anaongeza sababu nyingine ni ongezeko la watu wa daraja la kati kiuchumi ambapo baadhi ya tafiti zimeonyesha ongezeko hilo la kiuchumi huwa linaambatana na mafua ya allergy ambapo nayo yamekuwa yakichangia ukuaji wa nyama za pua ambazo ni sehemu ya kinga katika miili ya watoto.

Kuhusu tiba, Dk Mwansasu imegawanyika katika makundi mawili ambapo ni mgonjwa kusubiri kwenye uangalizi wa mara kwa mara na pia kwa njia ya upasuaji.

“Ina maanisha ikifika miaka mitano kuna uwezekano mkubwa zile dalili zikapungua makali yake kwani pua za watoto hawa huwa zinaongezeka ukubwa na nyama zinasinyaa kwahiyo kuacha nafasi kubwa ya kupita hewa.

“Daktari akimfanyia uchunguzi anaweza akawa anamfuatilia kwa karibu ili aweze kuvuka umri wa miaka mitano bila madhara, akaamua kumpa dawa za kutuliza dalili za mafua au maambukizi yatokanayo na pua kuziba akitegemea mtoto pua zake kuongezeka na tatizo kuisha baada ya muda fulani.

“Tiba ya pili ni kuzipunguza nyama za pua ili kuongeza njia ya hewa kwa kutumia upasuaji.Hili ni lile kundi la watoto ambao halikidhi vigezo la tiba ya kusubiria na kufuatiliwa kwa ukaribu,” anasema Dk Mwansasu.

Anaeleza kuwa kwa Agakhan katika kliniki ya masikio, pua na koo katika watoto kumi walio chini ya miaka sita hadi mwaka mmoja, wanne wanakuwa na nyama za pua na waliobaki ni magonjwa mengine.

 

Naye Daktari bingwa wa koo, pua na masikio, kutoka Hospitali ya Dk. Ole Lengine’s Memorial, Emmanuel Ole anasema huwezi kuzungumzia nyama za pua kwa watoto bila kuzungumzia mafindofindo (vidonda vya koo).

Anasema nyama za pua na mafindonfindo ni mtandao mmoja, ambapo ni sehemu ya nyama ambazo zinahusika na mfumo wa kinga mwilini ambao hauishii kwenye nyama ya pua na koo unahusisha pia na mlolongo wa tezi ambazo ziko kwenye shingo, bandama na sehemu nyingine za utumbo.

“Ni mara chache unaweza usichanganye nyama za pua na mafindofindo kwasababu nyama za pua zinaushirikiano na nyama za koo, yaani ni mfumo mkubwa na hata upasuaji unaofanyika ni kwa nyama za pua na koo kwa wakati mmoja, kwani ukitoa nyama za pua tu, ugonjwa huo unarudi tena,” anasema.

Anasema pamoja na dalili zilizotajwa, madhara mengine ambayo anaweza kuyapata mtoto ikiwa hajafanyiwa upasuaji ni matatizo ya moyo, kifua, mifupa na figo inashindwa kuchuja maji vya kutosha.

Anabainisha kuwa ili mtoto afanyiwe upasuaji awe na umri kuanzia mwaka mmoja na uzito kuanzia kilo 10.

“Upasuaji unafanyika ndani kwa ndani kwa kuweka kifaa maalumu kooni, na baada ya upasuaji mgonjwa anashauriwa kula Ice cream, vitu vya laini, kusukutua na maji ya chumvi, kutafuna big G na asitumie vitu vya moto na pia tunasisitiza asitumie nyama kwasababu inaweza kumuumiza,” anasema kuongeza:

“Pale palipotolewa nyama za koo panabadilika na kuwa na mabaka ya rangi nyeupe hiyo ndo dalili ya mwanzo ya kupona na sio maambukizi,”

Anabainisha sababu ambayo husababisha watoto wakifanyiwa upasuaji ugonjwa kujirudia ni kutokana na upasuaji kutokufanyika kikamilifu, ambapo kuna nyama ambazo zinakuwa vimeachwa.

Hata hivyo Dk Ole anasema mpaka sasa hakuna visababisi vya moja vya ugonjwa huo ila inatakiwa kuepuka vumbi, dawa za mbu, perfume na vitu vyenye harufu kali ambazo zinamsababishia mtoto mafua.

Anasema katika hospitali hiyo kwa siku wanafanya upasuaji kwa watoto sita au saba huku wengi wakiwa chini ya miaka saba.

“Sina takwimu lakini duniani kote upasuaji huu ndo unaoongoza ukilinganisha na zingine nadhani ni kwasababu ya mabadiliko ya mazingira,” anafafanua.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags