Ukimfunika kukaba, atakufunika kwenye kufunga. Ukimfunika kwa chenga, atakutesa kwa mishuti. Akiwepo uwanjani anakupa meza na maji ya kunawa. Anakuwekea chakula na kitanda anakupatia.
Namuongelea fundi wa mpira kutoka visiwani. Hajatokea kama yeye kabla na baada ya mapinduzi ya Zanzibar.
Feisal Salim 'Feitoto Zanzibar Fainest'. Huyu ndiyo mfalme mzawa wa kiduara katikati ya dimba.
Simba wanamtaka kwa udi na mavumba yote. Yanga wanamuhitaji kwa hali na mali zao zote. Ni kama kumpenda demu ambaye hajui kama unampenda. Ama kumsifia demu ambaye hata yeye anajijua ni mzuri.
Simba na Yanga wanahaha. Kila timu inamtaka. Kila kocha anataka kufanya kazi na Fei. Wananchi wanamuhusudu kuliko anavyowapenda. Mashabiki wa Simba wanampenda kuliko nyota wao waliopo.
Lakini yeye ukimtazama hana habari kabisa. Anachofanya ni kuwapa Azam kile alichopewa na Mungu. Kipaji cha soka. Watu wanadata naye. Nguvu ya miguu yake ni ya pekee kuliko upekee wenyewe.
Hawawezi kusema ila wenzake hiki kitu kinawaumiza. Katikati ya magwiji kama Aziz Ki, Chama, Pacome, Aucho hata Ngoma. Lundo la viungo wa ndani na nje. Feitoto anasimama nao katika mstari mmoja.
Ogopa sana. Heshimu. Hakuna zaidi ya miguu na akili yake. Kuchezea kile kitufe kinachotakiwa kuchezwa. Hapa ukweli ulio wazi kuna bato la wazi na la siri. Kati ya Fei peke yake na viungo wa Simba na Yanga.
Ukiwa nje ya hizi timu huwezi "kubato' na walio ndani yake. 'Kozi' soka letu limekaa vyumbani mwao. Lakini Fei kaendelea kung'aa nje ya hizi timu. Na yupo kwenye kilele bila kutumia nguvu. Anawakalisha kila msimu.
Alichonacho Fei kwenye miguu yake. Angekuwa nacho mchezaji wa kigeni, nchi ingesimama. Bongo tuna hulka ya kupenda wageni kama majuha. Na ndipo Fei anafanya tuamini soka ni burudani na lichezwe kiburudani.
Mtazame Fei akiwa dimbani. Utajua Fei ni zaidi ya mashuti ya magoli. Miguu yake inaufanya mpira uwe sehemu ya sterehe kama sterehe zingine. Anastahili kuwa MVP msimu huu? Yes... Why not?
Kwa leo tubaki na Fei, 'neksi taimu' turuke na Mzize. Hawa ni migodi inayozagaa Daslama mjini kibwege tu. Nipe Fei nipe Mzize nikupe figo. Hawa ni pesa ya waziwazi kabisa.

Leave a Reply