Nilipofanywa Mshenga, mshkaji akafungishwa ndoa mbele ya jeneza

Nilipofanywa Mshenga, mshkaji akafungishwa ndoa mbele ya jeneza

Nakumbuka ilikuwa ni mwaka 1994 wakati huo nilikuwa nafanya kazi katika kampuni ya ujenzi ya Wajapani kama fundi Mchundo ndipo mkasa huu uliponitokea nikiwa na Rafiki yangu aliyenipokea kazini wakati huo.

Huyu bwana anaitwa Kiswabi, alikuwa ni fundi kama mimi na kwa kuwa nilimkuta kazini, yeye ndiye aliyenifundisha Maisha ya hapo kazini ya namna ya kufanya kazi kwa desturi ya Wajapan na pia namna ya kuhusiana na watu hapo kazini.

Ukweli ni kwamba alinisaidia sana kunifanya nizoee mazingira haraka na kwa wepesi.

Huyu Rafiki yangu Kiswabi alikuwa anaishi na mwanamke ambaye alimtorosha huko kwao Kisiju wakati akifanya kazi kwenye mradi mwingine wa kujenga barabara na aliishi na mwanamke huyo kwa miaka minne na kujaaliwa kupata Watoto wawili bila kwenda ukweni ili kukamilisha taratibu za posa na kulipa mahari.

Sasa ukatokea msiba wa baba mkwe wake hivyo ikamlazimu yeye na familia yake ya mke na Watoto waende Kisiju kuhudhuria Mazishi.

Kwa kuwa nilikuwa likizo aliniomba nimsindikize na kutokana na urafiki wetu nikakubali kumsindikiza Rafiki yangu huyu tuliyeshibana.

Tuliondoka siku inayofuata ambayo nakumbuka ilikuwa ni Ijumaa na ndiyo ilikuwa ni siku ya mazishi. Tuliwahi magari ya alfajiri sana ili tuwahi kufika Kisiju kumzika baba mkwe.

Tulifika majira ya saa nne asubuhi tukapokewa kwa bashasha hasa ukichukulia kwamba ni miaka minne hawajawahi kumuona binti yao na Watoto wao walioambatana nao kwenye msiba.

Tuliarifiwa kwamba mazishi yatafanyika baada ya swala ya Ijumaa kwa kuwa yule mzee alikuwa ni miongoni mwa wana zuoni walioshika dini pale Kisiju, msiba wake ulijaa masheikh na waalimu kutoka eneo lote la Kisiju, Mkuranga, Ikwiriri mpaka Somanga.

Ulikuwa ni msiba uliokutanisha magwiji wabobezi wa dini ya Kiislamu na muda wote kulikuwa na visomo na dua za kumuombea marehemu.

Baada ya swala ya Ijumaa na masheikh kufika kuuandaa mwili wa marehemu, jeneza lilitolewa nje kwa ajili ya kuswaliwa na kwenda kuzika kabla ya swala ya Alasiri.

Lakini wakati tukiwa tumekaa pale nje kukawa na kikao cha ndugu wakiwa wamejikusanya pembeni akiwemo mke wa Rafiki yangu Kiswabi.

Baada ya kile kikao ambacho kilikuwa kifupi, Mimi na rafiki yangu tuliitwa na tulipojumuika kwenye Kile kikao Mjomba wa mke wake ambaye ndiye Sheikh wa Pale Kisiju na aliyeonekana kuwa msemaji wa ile familia. 

Alimwambia Rafiki yangu Kiswabi kwamba Kuna suala limejadiliwa na wanafamilia la yeye kumtorosha binti yao na kwenda kuishi naye mjini kwa miaka minne bila kufuata utaratibu na Marehemu aliasha wosia kwamba siku akifariki, iwapo binti yake atakuja kumzika akiwa na mwenzake basi asizikwe mpaka wafungishwe ndoa kwa sababu hayuko tayari kwenda motoni kwa kumruhusu binti yake kuzini.

Yule Mjomba aliongea kwa mamlaka na msisitizo huku akiwa ametukazia macho.

Rafiki yangu Kiswabi kwa hali ya taharuki akajitetea kwamba hajajiandaa na hakuja na ndugu yake yeyote na kuahidi kufanyia kazi suala hilo baada ya mazishi akijipanga…

Kauli hiyo iliamsha hasira za wale Masheikh na ndugu wa Marehemu wakiwemo Watoto wake wa Kiume…

‘Sikiliza Kijana usituchezee’, alisema mjomba na msemaji wa familia, ‘Kwanza unalo kosa la kisheria kumtorosha binti yetu ambaye ndiyo kwanza alimaliza sekondari na tulikuwa na mpango wa kumuendeleza kielimu na swala hili liko Polisi na ukituchezea ujue Mkwe wa Marehemu yuko hapa na ni Kamishna wa Polisi atakuweka ndani sasa hivi usituone sisi ni Majunun tutakucharaza Henzirani hapa hapa hadharani…’

Alihamaki mjomba.

Kwa wasiwasi jamaa yangu baada ya kutishiwa Polisi alikubali kufungishwa ndoa na mjomba akamwambia mahari anayotaka mkewe ni kununuliwa Masahafu tu basi na taratibu nyingine atakuja kuzimalizia baadaye. Haikuchukua muda Masahafu ililetwa jamaa yangu akailipia na ikapokelewa na kupelekewa bibi harusi ambaye alikuwa amefichwa ndani.

Haraka haraka tukaambiwa twende ndani tukajiandae na mimi nikapewa cheo cha kuwa mpambe wa bwana harusi kimshitukizo. Sikubisha kabisa maana niliona kwamba wale Wazee walikuwa hawataki Masikhara.

Tuliazimwa Kanzu na kuvaa na bibi harusi aliandaliwa huko chumbani na baada ya taratibu za Walii ambaye alikuwa ni kaka wa mke wa jamaa kupata ridhaa ya bibi harusi, Mjomba aliitisha chetezo na ubani na tukakalishwa mbele ya jeneza la Marehemu baba mkwe na jamaa yangu Kiswabi akafungishwa ndoa pale pale.

Baada ya ndoa ikawa ni muda wa kula, likapitishwa Pilau na ikawa jamaa kaokoa gharama kwa kufungishwa ndoa na wageni kula pilau la msiba.

Tulipomaliza kula ndipo maiti akaswaliwa na tukaenda kuzika.

Tuliporudi jamaa akaingizwa ndani rasmi kumuona mkewe kama taratibu za kiislamu zinavyotaka na shughuli ikawa imeisha.

Nilirudi Dar peke yangu na kumuacha jamaa yangu akila fungate na mkewe huko Kisiju.

Hili ni fundisho kwa vijana wanaokwapua mabinti wa watu na kuishi nao kinyumba bila ya kufunga ndoa.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Mzee Mtambuzi

A freelance Journalist and also teaching self-empowerment, positive thinking as a means of creating the life you desire including spirituality. He is writing in Mwananchi Scoop every Wednesday Visa na Mikasa.


Latest Post

Latest Tags