Nilichokiona kwa Daz Nundaz

Nilichokiona kwa Daz Nundaz

Ferouz bado ana 'eneji' kubwa sana. Daz Baba ana nyota kali sana. Hawa wote wanahitajiana kuliko wanavyodhani wao. Na huenda wakikaa pamoja wanaweza kuiona nchi ya ahadi tena. Watu bado wanawapenda sana.

Ferouz akishika maiki unaona kabisa mwamba bado yupo imara. Anaamsha sana na sauti ni ile ile. Na ukumbuke kubwa Ferouz ndiye mwenye maeneo mengi ya kuimba kwenye nyimbo zao.

Daz Baba akishika maiki watu wanaimba naye. Na ikafika wakati umma wa jamii ya pale Ware House Arena iliifunika hata sauti yake wakasikika mashabiki tu. Bila shaka mistari yake inawakuna wengi.

Mashabiki wa Bongo Fleva Honors, wana pesa kuliko wasanii wanaotazama. Hakuna m-Daz Nundaz aliyeenda na gari lake binafsi. Lakini mashabiki ni vigumu kujua kama yupo aliyeenda bila gari lake binafsi. Wengi wamenona.

Wote wamening'iniza funguo kiunoni. Wote wanagonga 'chiazi' na glasi zenye pombe za bei ghali. Sura zao zina nuru na wanajiamini na kuwatuza kina Daz Baba pesa. Ni kama enzi za Mapedeshee wa Twanga na Ngwasuma.

Wakati zamani wasanii wangetimba na magari yao. Mashabiki wangetimba kwa miguu na daladala huku wakishangaa ndinga za mastaa. Sasa ni kinyume chake. Waliokuwa mashabiki miaka ile sasa ndiyo mabosi kwenye taasisi kibao.

Shoo ya juzi imenipa jawabu la wimbo upi kati ya Kamanda na Barua ni pendwa zaidi kwa mashabiki. Jibu ni Barua ndiyo wimbo pendwa zaidi. Watu waliimba kila mstari kwa mstari bila kuchoka. Noma!

Daz Baba kuna ulazima wa kumsimamia kwenye eneo tengefu la misosi. Iwe ni adhabu ya kula kilazima ili aweke sawa bodi. La Rhumba apewe adhabu ya kula kwa mpangilio kama adhabu, ili aweke sawa bodi pia.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags