Ni Desturi Ya Alikiba Kususa Miaka Yote

Ni Desturi Ya Alikiba Kususa Miaka Yote

Ni miezi sita sasa bila Alikiba kutoa wimbo mpya lakini sio jambo ngeni bali ni utamaduni wake kwa miaka nenda rudi, ni mara kadhaa amewahi kujipa mapumziko na baadaye ujio wake unakuwa wa kishindo na kuweka rekodi nyingi.

Mradi wa mwisho kutoka kwa Alikiba ni EP yake ya kwanza, Starter (2024) iliyoachiwa hapo Septemba 14 ikiwa na jumla ya nyimbo saba ambazo alishirikiana na wasanii watatu, Marioo, Nandy na Jay Melody.

Hata hivyo, EP hii haijapata mapokezi makubwa ukilinganisha na albamu yake ya tatu na ya mwisho, Only One King (2021) chini ya Ziiki Media na Kings Music iliyoshinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2021 kama Albamu Bora ya Mwaka.

Albamu hiyo ambayo kwa sehemu kubwa ilitayarishwa na Yogo Beats, ilitoka Oktoba 2021 na akakaa kimya hadi Septemba 2022 alipotoa nyimbo mbili, 'Asali' na 'Tile' ikiwa ni miezi nane ya ukimya, hivyo sasa hatupaswi kushangaa kwani anaishi utamaduni wake.

Na mwaka 2023 akaufungua akitoa wimbo wake 'Mahaba' hapo Februari, huu ulikuwa ujio wa kimya kimya ila baadaye akaonyesha kishindo chake wimbo huo ukishinda tuzo ya TMA 2023 kama Wimbo Bora wa Bongofleva na hadi sasa video yake ikiwa ya pili kwa Alikiba kutazamwa zaidi YouTube.

Ikumbukwe Alikiba, mshindi wa MTV EMAs 2016, aliwahi kukaa kimya kwa miaka miwili hadi aliporejea kwa kishindo na wimbo wake, Mwana (2014) ambao ulikuwa ndio wa kwanza kwake chini ya RockStar Africa, rebo ambayo alifanya nayo kazi kwa miaka 10.

Dili la kusaini RockStar Africa chini ya Seven Mosha wakati huo, lilikuja baada ya Alikiba kufanya vizuri katika mradi wa One8 ulioachia wimbo, Hands Across The World (2010) uliojumuisha wasanii wengi wa Afrika pamoja na R. Kelly kutokea Marekani.

Basi wimbo wa Mwana (2014) ukafanya vizuri sana, video yake iliyotoka Desemba 19 ndio iliyofanya vizuri zaidi YouTube upande wa Alikiba ikiwa imetazamwa zaidi ya mara milioni 39.7 huku akifuatiwa na Mahaba (2023) iliyotazamwa mara milioni 39.2.

Alikiba ambaye ni mwanzilishi wa Kings Music Label, alikuja kukaa kimya tena kwa zaidi ya mwaka mmoja hadi aliporejea na wimbo, Seduce Me (2017), awamu hii akiwa chini ya RockStar Afrika na Sony Music Entertainment Africa.

Ni wimbo ambao Alikiba alipanga kumshirikisha Ne-Yo, mkali wa kibao, Miss Independent (2008) kutokea Marakeni ila akaachana na mpango huo baada ya kuona amefanya kolabo na wasanii wengi Afrika akiwemo Diamond Platnumz.

Basi video ya wimbo huo (Seduce Me) ikatazamwa zaidi ya mara milioni 1 ndani saa 37 na kuweka rekodi kama video iliyotazamwa sana YouTube Bongo kwa muda mfupi ikivunja rekodi ya wimbo, Salome (2016) wake Diamond uliyotazamwa mara milioni 1 kwa saa 48.

Hivyo sasa anaposikia Alikiba yupo kimya kwa miezi sita bila kutoa kazi yake binafsi, tambua kuwa ana mipango yake ambayo ipo ndani ya utamaduni wake wa miaka nenda rudi. Sio kwa bahati mbaya.

Lakini katika kipindi chake cha ukimya anatoa nafasi ya kushirikishwa na wasanii wengi, mathalani amesikika kwenye nyimbo za wanamuziki wenzake kama Marioo, Sober (2024), Rayvanny, Naoa (2024), Dully Sykes, Zai (2024), Darassa, BreakDown (2025) n.k.

Hata hivyo, huko katika kolabo nako ana utamaduni fulani, mfano aliwahi kukaa miaka 10 bila kumshirikisha msanii yeyote wa kike katika wimbo wake, tangu alipotoa kolabo yake na Lady Jaydee, Single Boy (2012).

Baada ya miaka hiyo 10 akaja kumshirikisha Sabaha Salum katika wimbo wake, Yalaiti (2023) lakini kwa upande wa pili yeye alikuwa akishirikishwa na wasanii wa kike, miongoni mwao ni Nandy (Nibakishie), Maua Sama (Niteke Remix), Maud Elka (Songi Songi Remix) n.k.

Ikumbukwe Alikiba akiwa na miaka zaidi ya 20 katika muziki, ameshinda tuzo za kimataifa ikiwemo All Africa Music Awards (AFRIMA) 2017 kama Wimbo Bora wa Kushirikiana Afrika (Aje) ft. M.I (Mr. Incredible) na MTV EMAs 2016 kama Msanii Bora Afrika.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags