Vijana wengi hutapeliwa mali zao na wengine hupata wakati mgumu kwa sababu ya mali za urithi.
Leo katika tutazungumzia juu ya usimamizi wa mali za marehemu kwa misingi ya sheria.
Uzoefu unaonesha kwamba matatizo mengi hujitokeza katika familia au ukoo pale mtu anapofariki.
Matatizo hayo hutokana na utata na kutokujua taratibu za kusimamia na kugawa mali za marehemu kwa warithi husika.
Sheria ya Usimamizi wa Mirathi inatoa muongozo wa jinsi ya ukusanyaji, uangalizi, usimamizi na hatimaye ugawanywaji wa mali za marehemu kwa warithi husika.
Vilevile hadhi na imani ya marehemu wakati wa kifo chake ndiyo itakayoamua ni Sheria gani itumike katika kushughulikia na kusimamia mirathi yake kama ni Sheria ya Kiserikali, Sheria ya Kiislamu, au Sheria ya Kimila.
Ambapo muongozo huo wa usimamizi wa mirathi utazingatia endapo marehemu ameacha wosia au hajaacha wosia.
Hata hivyo kama familia ya marehemu inapaswa kusajili kifo ndani ya siku 30 katika ofisi ya vizazi na vifo, na kama marehemu amefariki pasipo kuacha wosia familia ya marehemu au koo itapaswa kufanya kikao na kumchagua msimamizi wa mirathi.
Msimamizi huyo atafungua shauri la mirathi katika mahakama husika. Baada ya kutolewa barua ya usimamizi wa mirathi, Msimamizi wa mirathi atakusanya, kusimamamia na kugawa mali za marehemu kwa warithi halali na pia kuwasilisha mahakamani hati inayoorodhesha mali na jinsi zilivyogawanywa.
Vilevile katika kulinda, kutunza na kuendeleza mali za marehemu Sheria ya Usimamizi wa Mirathi inatoa muongozo wa usimamizi huu hata kabla ya kutolewa kwa barua za usimamizi wa mirathi.
Hivyo wanafamilia wa marehemu wanapaswa kuzingatia taratibu zote zilizoainishwa kisheria ili kuweza kulinda au kutunza mali za marehemu hata baada ya kifo.
Imeandaliwa na kwa msaada wa sheria kiganjani
Leave a Reply