NANI KASEMA KUSOTEA AJIRA, FANI NDIO USOMI

NANI KASEMA KUSOTEA AJIRA, FANI NDIO USOMI

Hivi karibuni kumetokea na hamasa kubwa ya vijana kufanya biashara kama njia moja wapo ya kujiongezea kipato.

Hii inaelezwa kuwa uwenda ni kutokana na upungufu wa ajira na changamoto katika kupata kazi zinazoweza kukidhi mahitaji ya taaluma na maisha kwa ujumla ya vijana hao.

Hata hivyo licha ya takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kubainisha kuwa ukosefu wa ajira umeendelea kushuka kutoka asilimia 10.3 mwaka 2014 hadi asilimia 9.7 mwaka 2018, bado kuna vijana wengi hasa wahitimu wa vyuo vikuu wanatafuta ajira ili kuweza kujiingizia kipato.

Wimbi la vijana hao hujikuta wakifanya kazi ambazo hawajasomea, ambapo wengi wao ijiingiza katika ufanyaji wa biashara mbalimbali ili kupata fedha.

Beng’i Issa ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), anafunguka na kueleza umuhimu wa kijana kujiajili na kufanya kazi ambazo hajasomea hasa biashara mbalimbali.

Amesema vijana wanapaswa kutambua kuwa maendeleo ya nchi hii yanawategemea wao hivyo wanatakiwa kuwa wafanyabiashara wazuri wakaoweza kutengeneza ajira kwa watu wengine.

“Kama kila kijana atafikiria kuwa lazima aajiliwe, hatuwezi kusonga mbele hata kidogo, wapo vijana wanauwezo wa kufanya vitu vikubwa vikaonekana huku wengine wanaweza kutengeneza kitu ambacho kitaisadia jamii nyingine.

 

“Kwahiyo vijana wajitathmini na watambue kuwa uwezo waliokuwa nao ni mkubwa hivyo wazione fursa katika kufanya biashara ili kujipatia kipato na kujenga maisha yao ya sasa na baadae,” amesema

Kuhusu mitaji

Licha ya mama Issa kuwataka vijana kufanya biashara pia amefafanua kuhusu suala la mitaji ambalo amesema naliona kama linasumbua kundi hilo.

Amesema vijana wengi wamekuwa na msukumo wa kuanzisha biashara ila wazo linalowajia vichwani mwao siku zote ni mtaji wa rasilimali fedha na si nia ya kufanya jambo.

“Mimi leo nawaambia kuwa mtaji sio kila kitu, tunapaswa kuweka akili yetu kwenye nia ya kufanya jambo na tukifanya hivyo tutafanya tu biashara hata kwa fedha kidogo uliyokuwa nayo,” amesema

Amesema kama kuna kijana anasubiri mpaka apate mtaji ndipo aanze kufanya biashara basi anaweza kuchelewa sana au kutofanya  kabisa shughuli hiyo.

“Maana kila utakaposema fedha hizi zinatosha kuanza kisha unaingiwa na hofu na kukosa nia ya kufanya jambo hilo, utajikuta unatumia fedha zote au sehemu ya fedha hizo katika shughuli nyingine.

 

“Ndio maana tunasema kuwa mtaji unaweza usikusaidie kama ujaweka nia ya kufanya jambo, utapewa hata milioni 300 kama una nia utazitumia na zitaisha zote bila kufanya chochote,” amesema

Vilevile amesema katika ufanyaji wa biashara, matokeo huwa mawili kupata faida au hasara, hivyo amewataka vijana kutambua kuwa yote hayo hutegemea mikakati ya mfanyabiashara mwenyewe, bidii, akili au maarifa.

Hata hivyo amesema hasara huweza kutokea wakati wowote hivyo cha muhimu ni kijana kutokata tamaa ili kuepuka kuwa tegemezi kwa familia yake na kutaka kuacha kisingizio cha mitaji na kukosa watu wa kuwadhamini ili kuajiriwa kwa haraka.

Kuhusu vijana wanaowawezesha kiuchumi

Amesema vijana wanaowezeshwa kiuchumi ni wengi na kama nchi wanakadiria kuwa kuna vijana Milioni 16 ambao ni kuanzia miaka 18 hadi 35.

Hata hivyo amesema kuna programu mbalimbali ya kuwawezesha vijana hao ikiwamo kuwapatia mikopo inayotolewa na halmashauri ambazo kwa mwaka mmoja zimekuwa zikitenga Bilioni 20 kwa ajili ya kuwakopesha.

“Vijana pia wamekuwa wakifikiwa na mikopo inayotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi na Ajira, zipo program ya kuwawezesha vijana katika ujuzi,” amesema

Hata hivyo amesema kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita jumla ya watanzania Milioni 15 yamefikiwa na kuwezeshwa katika shughuli za uwezeshaji.

 

“Mambo haya yamefanyika sio na baraza peke yake bali ni kwa kushirikiana na Sekta binafsi, umma na asasi za kiraia, tumefanikiwa kuwawezesha watu mitaji inayotolewa na mifuko ya Serikali ambayo imewafikia watu zaidi ya Milioni tano katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

“Kuna benki ambazo zimeanzisha bidhaa za vikundi ambazo zimekuwa zikitoa mikopo ya fedha kwa vikundi mbalimbali vya vijana na kinamama na kufanya uwekaji wa akiba,” amesema

Anasema pia wamefanikiwa kutoa elimu ya ujasiriamali hasa kwa vijana, kuwajengea ujuzi ambao utawafanya kuja kuwa imara kiuchumi, kutambua namna ya kutunza fedha na kuweka akiba.

Pia Serikali imefanikiwa kutengeneza sheria nyingi ambazo ni rafiki katika kumuwezesha mtanzania kufanya biashara na kuwekeza hapa nchini.

Vilevile anasisitiza kuwa katika shughuli za uzalishaji mali wanawake ni wengi kuliko wanaume na wao wamekuwa wakiwawezesha kwa kuwapatia mitaji huku zaidi ya asilimia 70 ya fedha za mikopo ya halmashauli uwenda kwao.

“Tumekuwa tukilihamasisha kundi hili kufanya kazi kwa kushirikiana na tumezamilia wanawake waongezeke katika makampuni yanayofanya kazi na Serikali,” amesema.

Changamoto zinazowakumba

Hata hivyo amesema moja ya changamoto wanayokubana nayo kutamani kumfikia kila mtanzania lakini uwezo wa kufanya hivyo bado kwao umekuwa ni mdogo.

 

“Watanzania wengi hasa vijana wana hamu ya maendeleo lakini wanakosa fursa, hivyo malengo yetu ya baadae ni kupeleka huduma kwa watanzania na kwa sasa tayari tumeanzisha programu ambayo itaongeza viwanda vidogo vidogo na vikubwa hapa nchini,” amesema.

Amesema wanataka kuanzisha vituo vya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi katika kila mikoa na wilaya ili kuhakikisha huduma za uwezeshaji zinakuwa karibu na wananchi.

“Tutashirikiana na mikoa na wadau mbalimbali kuhakikisha vituo hivyo vinaongezeka na wananchi wakienda huko watapatiwa mikopo itakayowawezesha kujikwamua, watapatiwa hata mafunzo ya kuongeza thamani ya mazao yao’.

Aidha amesema moja ya mafanikio waliyoyapata ni kuwepo kwa sheria za bima, huduma ndogo ndogo za fedha, madini, mafuta na gesi ambazo zimewarahisishia watanzania kuweza kushiriki kikamilifu katika biashara zote zinazoendeshwa kwenye sekta hizo.

“Sheria hizi pia zimewaradhimisha wawekezaji wowote wale wanaokuja kuwekeza kutoa ajira kwa wazawa,” amesema

Aidha amesema wanakadiria kuwa jumla ya watu 50,000 wameajiriwa katika miradi mbalimbali ya Serikali kitu ambacho ni kikubwa na wanaona mabadiriko makubwa katika maeneo hayo.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags