Mwigizaji na mchungaji Emmanuel Myamba ‘Pastor Myamba’ amepinga mitazamo ya baadhi ya watu kuwa kufanya sanaa ni dhambi.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu, Myamba amesema dhambi ipo kwenye kila fani.
“Kwenye hii dunia unaweza ukaamua kuishi kwa dhambi au kwa utakatifu, kila mahali kuna watakatifu na wenye dhambi na ndiyo maana kuna nyimbo za Bongo Fleva na gospel (za injili) lakini wote ni waimbaji.
“Mimi nimekaa kwenye kiwanda cha filamu kwa miaka karibia 20 lakini sijawahi kutenda dhambi kwa sababu ya usanii. Vitu vingine ni asili ya mtu inaonekana ulivyokuwa kwenye sinema ulikuwa mtenda dhambi, kwa hiyo sasa unadhani wote wanatenda dhambi,” anasema.
Wakati Myamba akisema hayo, kwenye uhalisia mambo ni tofauti. Mwaka 2016, mwanamuziki wa taarab, Mzee Yusuph alitangaza kuacha muziki na kumrudia Mungu lakini ilipofika 2020 alirudi tena kwenye muziki.
Naye msanii Snura Mushi, Julai 2024 alitangaza kuachana na sanaa. Si hao tu hata Suma Lee naye ameacha muziki na kumrudia Mungu.

Leave a Reply