Mwigizaji Fredy azikwa makaburi ya Kinondoni mastaa wenzie wamlilia

Mwigizaji Fredy azikwa makaburi ya Kinondoni mastaa wenzie wamlilia

Mwili wa mwigizaji wa Bongo Movie Fredy Kiluswa aliyefariki dunia Novemba 16, 2024 wakati akipatiwa matibabu kwenye Hospital ya Rufaa Mloganzila umezikwa leo Novemba 19, 2024 katika Makaburi ya Kinondoni.

Fredy ambaye amefariki dunia kwa maradhi ya moyo, enzi za uhai wake aliigiza tamthilia mbalimbali ikiwemo 'Mizani ya Mapenzi', Lawama na nyinginezo ameonekana kuacha pengo kwenye kiwanda cha burudani.

Akizungumza na Mwananchi mwigizaji wa tamthilia ya Jua Kali na Mkufunzi wa Taasisi ya Sanaa Bagamoyo Beatrice Taisamo 'Mama Luka' amesema kipindi anasoma Fredy alikuwa mwanafunzi bora na mcheshi.

“Mimi hatujaanza kufahamiana kwenye tasnia huku, Fredy ni mwanafunzi wangu mimi ni mkufunzi pale TASUBA. Kwa mara ya kwanza tulikutana pale kama mwanafunzi wangu na tukaja kukutana tena kwenye tasnia na nakumbuka tulifanya kazi wote kwenye tamthilia ya ‘Single Mama’ japo hatukukutana kuigiza kwa pamoja lakini hiyo ndio kazi ambayo tumeigiza wote.

“Kwa kweli alikuwa mwanafunzi mwenye kujituma sana, alikuwa anajitihada kwa sababu alikuwa na ndoto zake na unajua unapokuwa na ndoto inabidi uipambanie toka mapema kwasababu yeye alikuwa anajua anataka kufanya nini na kuwa nani tangu chuoni alikuwa mtu wa jitihada sana na pia alikuwa anachangamkia fursa” amesema Mama Luka.

Amesema tasnia imepata pigo kubwa kwani marehemu ni kati ya waigizaji waliokuwa wakifanya vizuri.

Kwa upande wake mwigizaji Isarito Mwakalindile ‘Luka Jua Kali’ amesema alikutana na marehemu kwa mara ya kwanza kwenye Shindano la TMT.

“Nakumbuka mara ya kwanza naonana naye ilikuwa 2014 kwenye mashindano ya TMT unajua kwenye lile shindano tuliingia watu wengi ambao wengine hatupo nao sasa hivi sio kama wamefariki hapana, wengine walishaolewa/kuoa na wakaendelea na maisha yao lakini yeye toka 2014 bado anapambana kwa hiyo ni kijana mwenzangu ambaye alikuwa ana hasira ya kuendelea kupambana bila kuchoka.

“Ni pigo kubwa kwa sababu ndio kizazi kipya kwenye tasnia ya filamu, sisi vijana ndio ambao watu wengi wanatuangalia kwamba tunaweza tukaibeba hii game na kuisimamisha ukiangalia Fredy alikuwa mwigizaji mzuri kwa hiyo kumpoteza tunaweza kusema ni kama umepoteza wanajeshi 1000 ni pengo kubwa ambalo kuzibika itakuwa kipengele,” amesema Luka.

Naye Habib Seif aliyekuwa akiigiza naye kwenye tamthilia ya Mizani ya Mapenzi amesema kikubwa alichojifunza kutoka kwenye maisha ya Fredy ni upendo.

"Nilikuwa najua kuwa anaumwa kwa sababu nafanya naye kazi nilikuwa namuona hali yake alivyokuwa anaipambania, hivi karibuni tulikuwa tunawasiliana twende tukafanye photoshoot kwa sababu miili yetu kama inalingana. Fredy ukiwa nae kazini ni zaidi ya mwigizaji anakuwa kama mwalimu kwa hiyo anaweza kukusaidia ukarudi kwenye hali ya kazi. Alikuwa hata akiona jambo anataka kufanya anataka wote mpate,"amesema

Aidha mwigizaji Mulky Salum ‘Femi’ amesema kiwanda cha filamu kimepata pigo kubwa kwani tayari kimepoteza nguli watatu akiwemo Mzee Pembe, Tesa wa Huba na sasa Fredy.

“Ni pigo kubwa sana kiwanda cha filamu kinapitia kwa sababu siyo tu kwa Grace na Fredy hapo nyuma tulimpoteza Pembe kwa hiyo hata hatujatimiza miezi miwili tumepoteza watu watatu kwa wakati mmoja tunapoteza watu wetu wa muhimu sana.

“Tunapoteza nguvu kazi kubwa kwa sababu ukifikiria umtafute kijana mwenye cast ya Fredy huwezi kuipata kirahisi yani utaipata lakini utapambania sana, ukisema utafute cast ya Grace Mapunda wamama wako wengi lakini Grace atabaki kuwa Grace ukitaka umtafute Pembe huwezi, kila mmoja anakuwa na nafasi yake kwenye kiwanda hiki cha filamu, kwetu sisi tunapata mapengo mengi sana na hatujui jinsi gani ya kuziba,” amesema Femi.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post