Mwanariadha aliyechomwa moto na mpenzi wake, afariki dunia

Mwanariadha aliyechomwa moto na mpenzi wake, afariki dunia

Mwanariadha kutoka Uganda wa mbio za Marathon, Rebecca Cheptegei amefariki dunia leo hii Septemba 5, 2024 wakati akipatiwa matibabu ya majeraha aliyoyapata baada ya kumwagiwa petroli kisha kuchomwa moto na mpenzi wake.

Kwa mujibu wa tovuti ya Nation ya nchini Kenya, umauti umemkuta katika Hospitali ya Rufaa ya Moi huko Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu nchini Kenya ikiwa ni siku mbili tangu kudaiwa kuchomwa moto na mpenzi wake Dickson Marangach, huku sababu ikitajwa ugomvi uliosababishwa na mgogoro wa kiwanja pamoja na nyumba.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Dk Owen Menach ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Kliniki na Upasuaji, amesema Cheptegei, aliyelazwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU), amefariki dunia saa 11 alfajiri ya leo.

“Inasikitisha kwamba tumempoteza mgonjwa mapema leo asubuhi baada ya viungo vyake vyote kuharibika saa kumi na moja asubuhi tulipokuwa tukijitahidi kuokoa maisha yake,” Dk Menach amesema.

Mwanafamilia wa marehemu, Dk Tony Sabila amethibitishia kwa kusema: “Ni kweli tumempoteza dada yetu asubuhi ya leo ingawa madaktari walijaribu kuokoa maisha yake na mimi binafsi nilikuwepo”.

Wakati akipatiwa matibabu alikuwa na majeraha ya moto kwa asilimia 80 na aliwekwa kwenye kifaa maalumu kutokana na ukubwa wa majeraha pia alikuwa akipewa msaada wa damu, maji, dawa na kupumua kupitia mashine.

Rais wa riadha nchini Kenya, Jack Tuwei amelaani tukio hilo akisema halipaswi kutokea kwa mtu yeyote kwa sababu maisha ni ya thamani na lazima yaheshimiwe na kuongeza kuwa watu wanapaswa kuishi kwa amani.

Cheptegei enzi za uhai wake alishiriki katika mbio za Marathon za Olimpiki Paris mwezi uliopita.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags