Visa na mikasa ni sehemu ya maisha ya binadamu bila kujali afanya shughuli gani. Kawaida visa hivyo na matukio huacha kumbukumbu katika jamii. Ikiwa mwaka 2024 unaelekea kuisha wadau wa burudani na wasanii walikumbana na visa mbalimbali vilivyoacha alama na funzo kwao.
Zuchu kutupiwa vitu jukwaani
Upendo na chuki za mashabiki kwa wasanii ni moja kati ya vitu vilivyogusa maisha ya kazi za wasanii nchini kwa mwaka 2024. Hili lilijionesha katika muendelezo wa mashabiki kumrushia vitu mwanamuziki Zuchu wakati akiwa anatumbuiza jukwaani.
Septemba 29, 2024, wakati akitumbuiza kwenye tamasha la Wasafi Festival Mkoani Mbeya, Zuchu alionesha kukerwa na baadhi ya mashabiki waliomrushia vitu wakati akitumbuiza na kupeleke aondoke jukwaani kabla ya kumaliza utumbuizaji.
Hata hivyo siyo tukio la kwanza kwa msanii huyo kurushiwa vitu akiwa jukwaani liliwahi kutokea pia mwaka 2023 aliporushiwa chupa na mashabiki akiwa Ruvuma anatumbuiza.
Muendelezo wa matukio hayo unaonesha tabia hiyo inaendelea kuota mizizi na kuwaacha baadhi ya mashabiki katika kumbukumbu mbaya ya kazi kwenye baadhi ya mikoa.
Marioo kususia Tuzo ya TMA kwa Barnaba
Katika hali isiyo ya kawaida Mei 21,2024 uliibuka mvutano kwenye mtandao wa Instagram uliomuhusisha wanamuziki Elias Barnabas, ‘Barnaba’ na Omary Ally,‘Marioo’, kuhusu Tuzo za Muziki Tanzania.
Mvutano huo ulianza baada ya Marioo kulalamikia albamu yake ya “The Kid You Know” kutoshinda tuzo na badala yake ikashinda “Love Sounds Different” ya Barnaba kama Albamu Bora Mwaka 2022, ambayo tuzo yake ilitoka 2023.
“Nawauliza waandaaji, kwa nini mnatoa tuzo kama hazitendi haki? Mnaombaje ushauri kwa wanaoshindania? that was not fair at all. Inasikitisha na inakatisha tamaa. This time around jipangeni.
“Albam ya #Tkyk ilikuwa ina hits kubwa, yaani sio ngoma kali tu, hits kubwa zaidi ya 4, lakini cha kushangaza imeshinda albamu ambayo ina hit song moja, sijui mbili na sio kubwa na hit yenyewe niliandika mimi kwenye hiyo albamu”. Aliandika Marioo kwenye ukurasa wake wa Instagram na kupelekea Barnaba kumsusia tuzo hiyo.
Katika kulijibu hilo Barnaba aliandika, "Nimeamua kwenda kubadilisha tuzo hii leo, ku print na nimekuwekea jina lako! nadhani unastahili so popote ulipo nitakuletea au uniambie wapi wakuletee mdogo wangu,”
Utakumbuka kuwa katika tuzo za TMA zilizotolewa mwaka huu 2024 zikihusisha tuzo za 2023 Marioo aliibuka kidedea kama msanii Bora wa Kiume.
Kiki za wasanii mzigo
Kutokana na kuwepo kwa imani kuwa kiki husaidia kuuza kazi za Wasanii. Kwa mwaka 2024 jambo hilo limeonekana kuendelea hadi kupelekea baadhi ya wasanii kupoteza uaminifu kutoka kwa mashabiki wao.
Kati ya matukio hayo ni yale ya wanamuziki Zuchu na Diamond kutangaza kuachana kisha baadaye kuonesha wakiwa pamoja na mapenzi yao yakiendelea.
Mwigizaji Hemed PHD na Lulu Diva kutokana na kazi ya tamthilia wanayocheza pamoja wawili hao walijikuta wakiingia kwenye kiki kwa lengo la kuzungumziwa zaidi, ili kazi yao hiyo itazamwe zaidi
Ruhusa kubadili tuzo kwa jina la mwingine
Mkurugenzi wa Ukuzaji na Maendeleo ya Sanaa ‘Basata’, Edward Buganga akizungumza na Mwananchi kuhusu Barnaba kuibadilisha jina tuzo alisema utolewaji wa tuzo huzingatia taratibu na kufuata vigezo.
“Hayo ni maoni ya watu, maoni na utaratibu ni vitu viwili tofauti, lakini inapotokea tuzo kuna taratibu zinafuatwa za kuwatunuku watu, kuna vigezo maalumu lazima vinafuatwa kimoja baada ya kingine
“Yanapotokea malalamiko kuna utaratibu wa kufanyia kazi, mlalamikaji na mlalamikiwa, tuna wataalamu wa kutosha wa kushughulikia suala hilo, kuna timu ya wanasheria, likifika tutashughulika nalo. Lengo letu ni kufanya kazi vizuri na wasanii wote wana haki sawa na Basata ni nyumbani kwao,” anasema.
Nini kifanyike 2025 wasanii watumbuize kwa amani
Kutokana na matukio ya aina ambayo yamemkuta Zuchu, mara kwa mara. Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Idara ya Sanaa na Ubunifu, Dk Abu Munir, ameiambia Mwananchi msanii anapaswa kujitambua kuwa yeye ni kioo cha jamii na kazi yake kubwa ni kuburudisha na kuelimisha.
Amesema msanii anapaswa kujitathimini anakusudia au anataka kupeleka ujumbe gani kwa hadhira yake na hii inaanzia kwenye mavazi yake, cheza yake pamoja na lugha atakayoitumia.
“Mfano huwezi kwenda kwenye hafla ya waheshimiwa ukafanya mambo ya ajabu, au kipindi hiki cha kuelekea vuguvugu la uchaguzi ukaenda kwa mashabiki zako kusifia chama fulani, ni lazma ujue unafanya kitu gani, kwa nani na kwa wakati gani,”anaeleza Mhadhiri huyo.
Kuhusu namna msanii anavyoweza kukabiliana na vurugu zitakazotokea dhidi yake, Dk Munir anasema ukiona maudhui unayopeleka kwa mashabiki wanayakataa, unatakiwa kubadilika haraka.
Naye Kaimu Mkurugenzi Muziki wa Baraza la Sanaa la Taifa(Basata), Kevin Stanslaus, amesema ni vyema wasanii kufuata mwongozo wa maadili ya sanaa ambao unaeleza kila kitu yakiwemo mambo watakayokumbana nayo kwenye majukwaa na namna ya kuyadhibiti.
“Mashabiki wanapaswa kutambua kuwa kunapofanyika maonyesho au matamasha, wasanii wamejiandaa kwa muda mrefu, wametumia gharama kufika eneo husika kuburudisha na wakati mwingine unakuta wametokea mbali hivyo wakifanyiwa ndivyo sivyo baadhi wanashindwa kuzuia hasira zao,”anasema
Leave a Reply