Muonekano unavyowabeba wasanii

Muonekano unavyowabeba wasanii

Leo kwenye Burudani tunaangalia wasanii na mionekano yao. Wapo baadhi ya watu wamekuwa wakijiuliza kwani kuna ulazima wa msanii kuvaa nguo za ajabu, mabwanga, nguo za kuchanika, kunyoa mitindo mbalimbali, na hata kubadili rangi nywele zao? Sasa basi kupitia segment hii ya Burudani majibu yote tumekuletea.

Kwa kawaida ukimtazama msanii kama vile Burna Boy na Asake kutoka nchini Nigeria hakika watakushagaza kwa mionekano yao hasa kimavazi, ukija kwa msanii kutoka nchini Marekani Kanye West ndiyo kabisaa unyama ni mwingi, lakini kibongo bongo nako hatuko nyuma mkali Simba la Masimba Dangote naye si haba, bila ya kumsahau Jux.

Pengine baadhi ya watu ambao wapo nje ya game inakuwa ngumu kuelewa mtindo wa maisha ya wasanii lakini kwa hakika wao huamini muonekano ni muhimu kwenye biashara zao.

Kwani azungumziwapo msanii basi inaguswa sanaa moja kwa moja, na katika sanaa hiyo ubunifu ni muhimu ili kazi ziweze kuvutia, hivyo basi wapo baadhi ya mashabiki wanaovutiwa na wasanii fulani kutokana na namna wanavyojiweka kwenye uvaaji na hata maisha yao kwa ujumla.

Kuhusiana na mionekano ya wasanii Mwananchi Scoop imekuletea majibu kamili kutoka kwa wadau mbalimbai wa muziki, wakitolea majibu kuhusiana swali lililouliza je ni lazima msanii kuwa na muonekano wa kipelee tofauti na watu wengine?

Huyu hapa Peter Minja mdau wa muziki ametolea majibu swali hilo amesema,
“Msanii ni lazima awe tofauti na watu wengine kimavazi, muonekano na maisha kwa ujumla kwa sababu akiwa kawaida hatakuwa na kitu cha ziada cha kufanya mtu aweze kumfuatilia, ukitazama mtu mpaka unaitwa msanii basi tayari kuna vitu unaweza kuvibadilisha na kuwa kwenye muundo wa sanaa na vikavutia watu wengine.”Anasema Peter

Hakuisha hapo na kuamua kutolea mfano maisha ya baadhi ya wasanii kwenye mavazi na picha wanazopiga kwa kudai kuwa wanafanya hivyo kwa ajili ya watu ili waweze kuwavutia huku akimtolea mfano mavazi ya msanii Diamond na kudai kuwa endapo atavaa suruali za vitambaa na viatu mchongoko basi atakosa mvuto.

Kwa wasanii wenye kipato cha chini mdau huyu wa muziki amewazungumzia nao na kusema. “Tunajua wapo wasanii wenye hali ya chini ila kwenye kujitafuta lazima waoneshe maisha ya namna fulani anayoishi kama msanii ili waweze kuvutia, mavazi wanayotakiwa kuvaa yawe na mvuto kwa jamii yawakilishe sanaa”. Anasema Peter

Hata hivyo Mwananchi Scoop haikuishia hapo moja kwa moja tukazungumza na msanii chipukizi kwenye muziki wa Bongo Fleva Xouh ambaye kwa upande wake amesema kuwa msanii lazima uweze kuwa tofauti, awaze kupata pesa kwa ajili ya kununua nguo kwani msanii anatakiwa akipita sehemu watu wote wajue kweli msanii amepita.




Mbali na msanii huyu mdau mwingine wa muziki John Lupembe ametoa mtazamo wake juu ya wasanii na mionekano yao.

“Sahihi kuwa na muonekano tofauti ili kuweza kutofautishwa, lakini linapokuja kwenye suala la maisha ni wewe uamuzi wako binafsi muda mwingine unakuta msanii hana kipato cha kuishi maisha ya kitajiri ili kukwepa mashabiki kufahamu kuwa hana kipato

Msanii anatakiwa kuwa na muonekano tofauti lakini hakikisha utofauti wako usikupelekee kushindwa kuishi maisha yako ya kawaida, na utofauti si tu mavazi hadi kwenye kusaidia jamii, kuwasilisha mawazo na kuwasiliana”. Anasema John

Safari ya Scoop ikaendelea na kupata maoni ya wadau juu ya muonekano, awamu hii ikamvuta Derick Joseph anasema kuwa utofauti wa msanii unamsaidia ku-promote ngoma zake na kutosahaulika kama ilivyokuwa wa Jux alikuwa hatoi ngoma lakini watu hawakum sahau kutokana na muonekano wake.

Derick akaenda mbali zaidi na kusema kuwa wasanii kuwa tofauti pia inawasaidia ku- set trend anasema.

Justin Bieber wakati anatoa albamu yake ya ‘changes’ mwaka 2020, alirudisha trend ya kuvaa mabwanga , nguo kubwa na Bongo Diamond alivyofanya ‘Jeje’ alivaa suruali kubwa na viatu vikubwa watu wakavifatilia na kuanza kuvivaa.




Zamani watu walikuwa wanabana suruali lakini siku hizi hata mtu akivaa bwanga bado anaonekana yupo kwenye fashion kwa sababu wasanii wana-set trend yaani wanaachana na vitu ambavyo watu wanafanya na kuanzisha vipya ili watu waige.” Anasema Derick
Kutokana na maswali ambayo wengi walikuwa wakijiuliza juu ya mionekano ya wasanii, kupitia wadau hawa mbalimbali waliofanya mahojianoa na Mwananchi Scoop naimani mtakuwa mmepata kitu na mmeelewa kwa nini wasanii wengi wanapenda kuwa na mionekano tofauti.

Tukutane tena Ijumaa ijayo ndani ya magazine yetu ya Mwananchi Scoop kama bado haujatu-follow hakikisha unafanya hivyo kwenye mitandao yetu ya kijamii kwa jina la Mwananchi Scoop. Tchaoooooo






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags