Mikopo Halmashauri inavyowasaidia vijana kujiajiri

Mikopo Halmashauri inavyowasaidia vijana kujiajiri

Vijana wenzangu mambo vipi….najua baadhi yenu hasa wale mliopo vyuoni mnapenda sana kufanya biashara ila ukosefu wa  fedha imekuwa ni changamoto kwenu.

Hata hivyo mtambue kuwa katika harakati za kuhakikisha kwamba vijana wanapata ajira sio tu kwa kuajiriwa lakini kwa pia kwa kujiajiri kupitia ubunifu wa biashara mbalimbali, Serikali kupitia halmashauri zake zote nchini zimekuwa zikitoa mikopo kwa makundi matatu ikiwamo la vijana.

Mikopo hiyo imekuwa ikitolewa ili iweze kuwasaidia vijana kuanzisha biashara na kuondokana na dhana ya kuajiriwa pindi tu unapomaliza masoko yako.

Ripoti ya soko la ajira kwa vijana iliyotolewa Novemba 20, 2017 na Shirika la Kazi Duniani (ILO) ilionyesha kuwa zaidi ya vijana milioni 70.9 ambao ni sawa asilimia 13.1 ya vijana wote duniani wanakosa ajira.

Shirika hilo lilisema kuwa hali hiyo ingeendelea kuzorota kwa mwaka 2018 ambapo walitegemea vijana milioni 71.1 sawa na asilimia 13.1 ya vijana hawatakuwa na ajira.

Ripoti hiyo ambayo ilikuwa ni ya kwanza tangu mwaka 2015 iliongelea ugumu wa upatikanaji wa ajira kwa vijana waliomaliza masomo na pia mabadiliko ya ajira kwa vijana yanayoelekea katika mfumo wa teknolojia.

Hata hivyo takwimu za ILO za hivi sasa zinaonyesha kwamba vijana milioni 59 hawana ajira kote duniani na wengine milioni 136 wanaishi katika umasikini na hivyo kufanya tatizo la ajira kwa vijana kuwa ni shinikizo kubwa kwa dunia.

Kutokana na takwimu hizi nataka kukupa mchongo wewe kijana hasa wa Manispaa ya Ilala kwamba kuna mikopo inatolewa na halimashauri hiyo hivyo unapaswa kuichangamkia.

Sapiencia Masaga ni Ofisa Vijana Manispaa ya Ilala, anasema zaidi ya Sh. Bilioni nne zimetolewa kwa mwaka 2019/2020 kwa ajili ya kuvikopesha vikundi vya vijana 352 vilivyopo katika halmashauri hiyo.

Masaga anasema wametoa mikopo hiyo ili kuviwezesha vikundi hivyo kujikwamua kiuchumi na kuendeleza biashara zao mbalimbali walizozianzisha.

“Tangu mwaka 2014 kundi la vijana limekuwa likiongezeka katika kupatiwa mikopo ya halmashauri yetu na hii ni kutokana na wengi wao kupata elimu juu ya umuhimu wa fedha hizo katika kujikwamua kiuchumi.

"Kupitia Idara ya Maendeleo ya jamii ya manispaa yetu tumeweza kuwahamamisha vijana kukopa fedha hizi, ukiangalia takwimu za mwaka 2014 tulikuwa na vikundi vya vijana nane  vilivyokopa lakini  mwaka 2019/2020 tumepata vikundi hivyo 352,  idadi ambayo imekuwa ikiongezeka kila mwaka," anasema

Anasema kwa takwimu hizo ni wazi kuwa upo mwamko wa vijana wa kuchangamkia fursa hiyo ya mikopo inayotolewa na Manispaa ya Ilala.

“Kundi hili la vijana ni kati ya makundi matatu yanayonufaika na mikopo hii tunayoitoa, wapo wengine wanaonufaika ambapo ni  wanawake na watu wenye ulemavu,” anasema.

Vijana kushindwa kurejesha mikopo

Hata hivyo anasema pamoja na mwamko huo bado kuna changamoto ya baadhi ya vijana kushindwa kurejesha mikopo hiyo kwa wakati hivyo kukwamisha wengine kupata fedha.

“Tumeona moja ya sababu inayowafanya vijana kushindwa kurejesha mikopo, ni vikundi vyao vingi vinavyoanzishwa zimekuwa havina kiasi chochote cha kuanzisha biashara kwahiyo mkopo huo wanaopewa ndio uutumia kama mtaji wa kuanza biashara.

“Kwa staili hiyo unaona kabisa kuna uwezekano wa biashara hiyo kufa, kwa sababu tunapowapa mtaji ndipo wanaanza hivyo kukosa uzoefu wa biashara,” anasema

Vilevile anasema vijana wengi wana mihemuko ambayo uwafanya wakisha kopa fedha ufanya mambo yao mengine tofauti na biashara. Mwisho wa siku ushindwa kurejesha fedha hizo,” anasema

Hata hivyo anasema manispaa hiyo imekuwa ikivifatilia vikundi vya vijana vilivyoshindwa kurejesha mikopo na kuwapatia mbinu tofauti tofauti za kufanya marejesho.

Aidha anasema ipo dhana kwamba mikopo hiyo inatotolewa ni ya bure jambo ambalo amesisistiza kuwa si kweli bali watu wanapaswa kuirejesha ili kutoa fursa na wengine kukopa.

Naye Mratibu wa dawati la mikopo kutoka manispaa hiyo, Lucy Byabatu anasema ili vijana waweze kupata mikopo licha ya kutimiza masharti wanapaswa kuwa na nia ya kuziitaji fedha hizo kwa lengo la kufanya biashara zitakazoinua maisha yao.

Kwa upande wake Mratibu wa Miradi kutoka Shirika lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na masuala ya kijamii (CAFLO), Emmanuel Ngazi amesema kuwa chini ya ufadhili wa Shirika la Foundation for Civili Society (FCS) wamefanikiwa kuanzisha majukwaa ya vijana katika halmashauri hiyo ya Ilala.

Ngazi anasema shirika hilo liliamua kuanzisha majukwaa hayo maalum ya vijana kwa lengo la kutoa elimu ya ujasiliamali na namna hasa ya kufanya biashara ili waweza kujiajiri.

Anasema majukwaa hayo pia yana lengo la kuwawezesha vijana kuzitambua haki zao, kuzilinda na kuzitetea pamoja na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kimaendeleo.

Ngazi anasema katika kuendeleza harakati za kutekeleza dhamira na hatimaye kuweza kufikia dira, CAFLO imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali katika jamii hususani miradi inayohamasisha maendeleo ya vijana.

Hata hivyo anasema vijana wa majukwaa hayo wanaendelea kujengewa uwezo juu ya kuimarisha na kuendeleza majukwaa yao pamoja na kushiriki katika kutekeleza shughuli za kukuza uchumi na kuleta maendeleo.

“Shirika letu limejifunza kuwa vijana wengi wakielimishwa na kupewa fursa mbalimbali za kimaendeleo wana uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko chanya katika maisha yao, familia na jamii kwa ujumla.

“Kutokana na hilo wadau mbalimbali wanatakiwa kujitokeza kwa ajili ya kuwajengea uwezo vijana hususani walio kwenye majukwaa ili waweze kupanua wigo zaidi ya kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa viwanda hapa nchini,” anasema

Hata hivyo anasema kasi ya mikopo inayotolewa kwa makundi ya vijana hasa waliopo katika manispaa hiyo ni kidogo ndio maana wamekutana ili kutengeneza mikakati ya kuhakikisha vijana wote wananufaika.

Ofisa Maendeleo ya Jamii kata ya Kipawa, Tecla Ngambila anasema vijana wengi waliopo katika kata hiyo ni waoga wa kuthubutu kufanya mambo ya kimaendeleo hivyo anaamini kuwa kupitia mradi ya CAFLO itawasaidia na kuwaondolea dhana hiyo.

"Kipawa ni miongini mwa kata zilizoingizwa katika mradi wa CAFLO tunaamini kupitia majukwaa ya vijana wengi wataamka na kuanza kujituma kufanyakazi na kuwa wabunifu, " anasema Ngambila.

Joseph Kinsi Mtaalamu wa Masuala ya Vyakula kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), anasema vijana awapaswi kuwa bendera fuata upepo hivyo ni muhimu kujua wanataka kufanya nini katika maisha yao.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags