Mfahamu aliyebuni emoji

Mfahamu aliyebuni emoji

Matumizi ya emoji katika mawasiliano yamekua yakifanyika kila kukicha. Utumiaji wa emoji hizo kawaida ni njia ya kuwasilisha hisia katika mawasiliani. Jiulize tangu siku ianze umetumia emoji mara ngapi hadi saa?

Wakati unaendelea kujiuliza na kujijibu mfahamu Shigetaka Kurita mtaalamu kutoka Japan ambaye anajulikana kama mwasisi wa emojis ishara za kidijitali zinazotumika katika mawasiliano ya kila siku kwenye simu za mkononi, programu za ujumbe, na mitandao ya kijamii.

Mwanzilishi huyu wa emoji alizaliwa mwaka 1965. Alienda shule ya sanaa na alijikita katika uandishi na mbinu za kubuni picha. Alipomaliza masomo yake, alijiunga na kampuni ya mawasiliano ya simu ya 'NTT DoCoMo' mwaka 1997, ambapo alifanya kazi kama mbunifu na mtaalamu wa teknolojia ya mawasiliano nchini Japan.

NTT DoCoMo ilikuwa ikijitahidi kuleta mapinduzi katika mawasiliano ya simu za mkononi kwa kipindi hicho, na mwaka 1999 walizindua huduma ya 'i-mode', ambayo ilikuwa ni huduma ya intaneti kupitia simu za mkononi. Kurita alipewa jukumu la kubuni kipengele kipya cha huduma hii kinachoweza kuongeza shauku na urahisi wa mawasiliano kwa wateja.

Katika juhudi za kuboresha mawasiliano ya simu, Kurita aliona kuwa njia za kawaida za kuwasiliana kupitia maandishi peke yake zilikuwa na changamoto, hasa katika kuonyesha hisia na hali za kihemko. Aliamua kubuni alama za picha ambazo zingesaidia watu kueleza mawazo yao, hisia, na hali mbalimbali kwa njia ya haraka na yenye kuvutia. Hapa ndipo akabuni 'emoji'.

Emoji hizi zilikuwa zikiwakilisha hali mbalimbali za kihisia, vitu, wanyama, hali ya hewa, na mambo ya kila siku, kama vile moyo (❤️), uso wa furaha (😊), na mikono ya kushukuru (🙏).

Bunifu zake hazikwenda bure kwani emoji kwa sasa zimekuwa maarufu ulimwenguni kote kwa sababu zinatoa njia rahisi na ya haraka ya kuwasiliana, hasa wakati wa kutuma ujumbe wa maandishi. Kwani binadamu wanaelewa picha kwa urahisi kuliko maandishi, na hivyo emoji zimekuwa sehemu muhimu ya mawasiliano ya kisasa, zikisaidia kutoa muktadha wa kihisia kwa ujumbe na kuifanya mawasiliano kuwa ya kuvutia zaidi.

Hivyo basi emoji zimekuwa sehemu muhimu ya utamaduni wa mitandao na kidijitali, zikitumika katika mitandao ya kijamii kama Twitter, Facebook, WhatsApp, na Instagram, pamoja na programu zingine za ujumbe. Shigetaka Kurita anaendelea kutambulika kama mwanzilishi wa emoji.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags