Matumizi ya dawa za kulevya kwa wanavyuo, Changamoto na athari za kudumu

Matumizi ya dawa za kulevya kwa wanavyuo, Changamoto na athari za kudumu

Na Magreth Bavuma

Kumekua na kasi ya wimbi la vjana kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya na kutokana na takwimu za sasa si vijana wakiume tu kama ilivokua imezoeleka, vijana wakike pia wameonekana kuingia humo jambo ambalo linatishia kupotea kwa nguvu kazi kuanzia ngazi ya familia mpaka taifa. Dawa za kulevya ni mojawapo ya changamoto kubwa zinazokabili jamii ya wanavyuo katika vyuo vikuu, na matumizi ya dawa hizo yanaweza kuwa na athari mbaya sana kwa maisha yao kwa ujumla. Katika Makala hii tutaangazia athari za matumizi ya dawa za kulevya kwa wanavyuo na jinsi ya kukabiliana na changamoto hii.

Matumizi ya dawa za kulevya kwa wanavyuo yamekuwa suala linaloleta wasiwasi mkubwa katika vyuo vikuu duniani kote. Utafiti unaonyesha kuwa sababu mbalimbali zinachangia wanavyuo kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya, ikiwa ni pamoja na shinikizo la kijamii, mazingira duni, msongo wa mawazo, utamaduni wa burudani na nyingine nyingi. Kuna aina mbalimbali za dawa za kulevya ambazo zinaweza kuwa zikitumiwa kwa madhumuni ya burudani au kujaribu kubadilisha hali za akili na hizi ni pamoja na; Cocaine, Marijuana (Bangi), Heroin, Methamphetamine (Crystal Meth), Ecstasy (MDMA), LSD (Acid), Prescription Drugs (Dawa za Daktari):

Matumizi ya dawa za kulevya yanaweza kuleta athari katika afya ya mwili na akili ya wanavyuo, baadhi ya athari za kawaida ni pamoja na kuharibika kwa mfumo wa kinga, matatizo ya kupumua, kuharibika kwa ini, figo, na ubongo, na matatizo ya akili kama unyogovu, wasiwasi, na msongo wa mawazo.

Pia matumizi ya dawa za kulevya yanaweza kuathiri vibaya utendaji wa wanavyuo darasani, wanavyuo wanaojihusisha na matumizi ya dawa za kulevya wanaweza kukosa kuhudhuria masomo, kukosa kufanya kazi za nyumbani, na kushindwa kufikia malengo ya viwango vya kielimu wanayotamani.

Vilevile matumizi ya dawa za kulevya yanaweza kuharibu mahusiano ya wanavyuo na wenzao, marafiki, na familia. Dawa za kulevya mara nyingi huleta tabia za kutokujali, uongo, na hata wizi ili kupata fedha za kununulia dawa hizo.

Matumizi ya dawa za kulevya ni kinyume cha sheria katika nchi nyingi. Wanavyuo wanaojihusisha na matumizi ya dawa za kulevya wanaweza kukutana na matatizo ya kisheria ikiwa watakamatwa na kushitakiwa.

Kwa upande mwingine wanavyuo na jamii inaweza kukabiliana na matumizi ya Dawa za Kulevya kwa kufanya mambo yafuatayo.

Wanavyuo wanaweza kukabiliana na changamoto hii ya dawa za kukevya kwa kujiepusha na makundi ambayo yanakua kama kichochezi kikuu katika kuwashawishi kujiingiza kwenye mkumbo huo unao dhaniwa kuwa ndiyo sehemu ya burudani.

Lakini pia ni vizuri kama mwanachuo pale unapokua bored epuka kukaa idol bila kufanya chochote unaweza kutumia muda wako wa ziada ambao sio wa masomo kwa kucheza michezo, kusikiliza muziki kwenda ufukweni au kufanya mazoezi.

Kwa uongozi wa vyuo vikuu, unapaswa kuendeleza programu za elimu kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya. Wanavyuo wanapaswa kupewa habari sahihi kuhusu athari za dawa za kulevya ili waweze kufanya maamuzi sahihi.

Pia uongozi wa vyuo vikuu unaweza kuwezesha huduma za ushauri na usaidizi kwa wanavyuo wanaopambana na matumizi ya dawa za kulevya. Wanavyuo wanapaswa kujua wanaweza kutafuta msaada bila kuhukumiwa.

Hata wazazi wanalo jukumu muhimu katika kuelimisha watoto wao kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya na kuwaunga mkono katika kukabiliana na changamoto hizo.

Matumizi ya dawa za kulevya kwa wanavyuo ni suala linalohitaji tahadhari na jitihada za pamoja kutoka kwa vyuo, familia, na jamii kwa ujumla. Ni muhimu sana kuelewa kuwa matumizi ya dawa za kulevya ni hatari na zinaweza kusababisha athari mbaya kwa afya ya mwili na akili. Kuna hatari ya utegemezi na kushindwa kuacha matumizi, na pia hatari ya kujihusisha na vitendo vya kihalifu. Ni vyema kuepuka matumizi ya dawa za kulevya na kuchagua njia za burudani na kukabiliana na mafadhaiko ambazo ni salama na zenye afya.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post

Latest Tags