Marioo kachagua kusimama na Paula katika vita zote

Marioo kachagua kusimama na Paula katika vita zote

Na Peter Akaro

Mapema wiki hii ugomvi kati ya Abigail Chams na Paula iliibuka tena, baada ya ukimya wa muda, kitendo cha Marioo kuingilia kati na kumtetea binti huyo wa P-Funk Majani na Kajala Masanja ni ishara kachagua kusimama naye katika vita zote.

Tetesi za uhusiano wa Marioo na Paula zilianzia Aprili 2023, baada ya mrembo huyo kuachana na Rayvanny, tangu wakati huo wamekuwa pamoja, ukiwa ni uhusiano wa kwanza wa Marioo kuuweka hadharani tangu kuhusishwa na Mimi Mars.

Hata hivyo, uhusiano huu ulikuja kutibua ukaribu wa kikazi kati ya Marioo na Abigail Chams, ambaye walishirikiana katika wimbo wao, Nani? (2023).

Ugomvi ulizuka baada ya sauti ya Abigail Chams kuondolewa katika wimbo wa Marioo, Love Song (2023), ambao alishirikishwa hapo awali na nafasi yake kuchukuliwa na Alikiba, huku Marioo akimtuhumu Abigail kuvujisha wimbo huo mtandaoni.

Ugomvi huo ukanunuliwa kwa bei rahisi na mashabiki mtandaoni ambao walidai Paula ndiye alishinikiza sauti ya Abigail kuondolewa, ndipo vita vya warembo hao vikachukua nafasi na wakawa hawachaguliani maneno.

Akizungumza Instagram wakati akijibu maswali ya mashabiki wake, Abigail alisema hamchukii Paula kwa sababu ni mwanamke mwenzake ila hapendi kumzungumzia mtu ambaye hajulikani anafanya kazi gani!

“Nimejibu hili swali kwa sababu nimewaahidi nitajibu yote ila sioni umuhimu kuongelea watu ambao hata hatujui kazi zao ni nini, ila tu kuvuma kwa sababu ya kuwa na uhusiano na wanaume,” alisema Abigail Chams, kauli ambayo imeibua tena ugomvi.

Marioo, ambaye inasemekana anatarajia mtoto na Paula hivi karibuni alieleza kushangazwa na kauli ya Abigail kwa kusema licha ya mpenzi wake kutulia, bado watu wanatafuta kiki kupitia yeye.

Hata hivyo, Marioo sio kwamba anamtetea Paula kwenye ugomvi tu, bali anampa na nafasi katika kazi zake za muziki ili kuonyesha ni kiasi gani anampenda na anataka kuikuza chapa yake.

Tangu Marioo ametoka kimuziki na wimbo wake, Dar Kugumu (2018), Paula ndiye mrembo pekee ambaye ametokea katika video nyingi za nyimbo zake ambazo ni Lonely (2023), Tomorrow (2023) na Sing (2023).

Ila kuna madai kuwa Marioo alifanya hivyo kwa shinikizo la Paula ili kumrusha roho Rayvanny, ambaye amefanya video nyingi na mpenzi wake, Fahyma ambazo ni; Kwetu (2016), Natafuta Kiki (2016), Siri (2017), Forever (2023), Habibi (2023) na Mwambieni (2023).

Uhusiano wa Rayvanny na Paula ulifika tamati kwa vita vikali vya maneno, usaliti ulitajwa kuliangamiza penzi lao, hadi wanaachana tayari Paula alikuwa ametokea katika video ya wimbo mmoja wa Rayvanny, Wanaweweseka (2021).

Licha ya Marioo kushirikiana na Rayvanny katika nyimbo mbili, Te Quiero (2022) na Anisamehe (2022) ila sasa ukaribu wao umepungua sana, ingawa walikanusha madai kuwa wana ugomvi, ila inavyoonekana kwa nje Marioo kachagua kusimama na Paula.

Utakumbuka kabla ya Marioo kuwa na Paula, alihusishwa kuwa na uhusiano na Mimi Mars kwa muda, ingawa wote walikanusha jambo hilo kwa madai ukaribu wao ni wa kikazi, huku wakishirikiana katika nyimbo mbili, Una (2019) na La La (2022) ambazo zilifanya vizuri.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post

Latest Tags