Mambo  ya kuzingatia kwa mwanafunzi wa elimu ya juu

Mambo ya kuzingatia kwa mwanafunzi wa elimu ya juu

Inaendelea……

Kama unataka kutengeneza umoja katika kazi, kundi ulilokuwa nalo linakutafsiri mbele ya jamii ni nini hasa utakachokijenga maishani mwako. Kuna msemo wa kiingereza unaosema, "You choose your business partner at college."

Usiogope kufeli katika masomo, ogopa kuwa na hofu ya kutofikia malengo yako. Ni kweli kuwa unapokuwa chuo, moja kati ya vitu vya msingi ni kufaulu masomo. Ila ukweli ni kwamba wengi wanapofika chuo ndipo wanapoweza kujipambanua ni nini wanachotaka- yaani malengo wanayotaka kuyafikia. 

Hivyo wengi wanahofu ya kufeli katika masomo kuliko kufeli katika malengo yao. Tambua kuwa kufaulu masomo bila kuwa na malengo au kutofikia malengo yako ni sawa na kulipa nauli ya ndege kubwa halafu ukashindwa kusafiri kisa umekosa nauli ya kukutoa nyumbani mpaka uwanja wa ndege.

Yatafakari malengo yako na pia liangalie jambo unalolifanya chuoni kama kweli vinaendana na kama haviendani ni kheri ukatafuta njia mbadala ya kuyafikia malengo yako. "Usihofu katika jambo lolote, hofu ni kifo cha mtu aliyekosa maarifa."

"Fanya maamuzi sahihi, si kila jambo linawezekana kwa wakati ule ule." Maisha yako chuoni si zaidi ya miaka mitano (yamkini kuna wengine wanaosoma zaidi ya miaka hiyo). 

Hivyo tambua kuwa unapokuwa mwanafunzi wa chuo si kila jambo au wazo linalokuja katika akili yako ulipaparikie. Fanya uchambuzi yakinifu, jiridhishe, jisadikishe na upange kwa usahihi kwa kila jambo unalolifanya. 

Na pia usitende jambo kwa sababu umeambiwa na mtu fulani ulifanye. Kumbuka kuwa mwisho wa siku kila jambo unalolifanya litakurudishia majibu chanya au hasi. 

Unaweza ukapata wazo la biashara, jiulize kama ni wazo sahihi kwa wewe kulifanya. Tambua kuwa haya ni maisha yako unayoyajenga kwa ajili yako na kizazi chako. Lakini pamoja na hayo yote, usiogope kuchukua au kukamata fursa pale inapojitokeza.

Jifunze zaidi kuhusu akiba, tafuta vyanzo vya mapato. Hata ukifanikiwa kuweka kiasi kidogo cha pesa, kitakusaidia katika siku ambazo una uhitaji zaidi ya leo. Wengi wa wanafunzi wa chuo ni wafujaji wazuri zaidi ya kuwa wawekezaji.

Simaanishi kuwa hautakiwi kuwa na matumizi mengi, kuwa na matumizi yenye tija na kiasi kidogo utakachoweza kukiweka akiba, weka katika 'Fixed Deposit' na kitaweza kukusaidia pale utakapohitaji zaidi. 

Kwa maana mkopo ulio nao leo, kesho unaweza usiwepo; msaada wa kiuchumi unaoufaidi leo kesho utaisha, je utafanya nini iwapo ulitumia vyote na hukujua kuwekeza. Kuwa mjasiriamali wa pesa zako, zitengenezee namna ambayo zitakuheshimu na hazitakufanya uwe na mihemko katika kuzitumia.

"Cheti kizuri sio kufanikiwa katika maisha." Sikuvunji moyo unayetafuta kuwa mwanafunzi bora au kuwa na cheti cha 'first class' au 'highest GPA’, bali ni kukujulisha kuwa 'utashi katika mafunzo ya vitendo ni jambo ambalo uchumi wa karne ya ishirini na moja inahitaji.' Jitahidi ujue soko lako linahitaji nini na sio kuwa na matokeo mazuri katika maandishi ila ubovu katika vitendo. 

Iwapo itatokea hivyo, ni wazi kuwa unaishusha hadhi yako, hadhi ya elimu yako na hadhi ya mahali kote ulipopitia. Ofisi za siku hizi, ziwe za Uhasibu au Uhandisi, sio za kujizungusha kwenye kiti cha ofisi, bali ni za vitendo na kulielewa soko linalokuzunguka.

 

mwisho






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags