Mambo ya kuzingatia katika uvaaji wa suti

Mambo ya kuzingatia katika uvaaji wa suti

Alooooh!!! Its Friday kama kawaida watu wangu karibu sana kwenye ukurasa wa fashion bila shaka umekua mfuatiliaji mzuri sana ukiwa unachukua madini kadha wa kadha kuhakikisha kwenye suala la muonekano na mavazi unakua bomba kabisa.

Wiki hii kwenye kipengele hiki tutaangazia mambo ya kuzingatia katika uvaaji wa suti bwana ili uwe na muonekano mzuri kwenye vazi hili unatakiwa uwe vipi? Karibu tujifunze kwa pamoja.

Suti ni vazi la heshima sana linalopendwa kuvaliwa na watu wa rika mbalimbali katika shughuli tofauti tofauti katika jamii.

Vazi linamfanya mtu kuonekana maridadi sana lakini mtu anapokosea kulivaa humfanya kupoteza muonekano wa vazi hilo na kumfanya kuwa kituko.

Baadhi ya makosa ambayo baadhi ya watu huyafanya ni uchaguzi usiosahihi wa rangi ya suti, uvaaji usio sahihi wa tai, saa, viatu pamoja na uvaaji wa suti kubwa au ndogo kuliko mwili, pamoja na uvaaji wa 'accessories' nyingi wakati umevaa suti.

Hilo linaungwa mkono na Haidari Khamisi Fundi anayejishughulisha na ushonaji wa nguo za kike na kiume katika jiji la Dar es Salaam ambaye anaeleza kuwa suti ni vazi rasmi hivyo halipendezi kuvaliwa na urembo mwingi.

"Kuna baadhi ya watu unakuta amevaa suti na pete nyingi mkononi au cheni nyingi shingoni au anavaa culture katika mikono, uvaaji huu unaondoa ile dhana ya heshima ya vazi la suti, mtu anaweza kuvaa saa, pete moja au mbili na miwani inatosha," alisema.

Pia alisema mtu anapovaa suti ili aweze kupata muonekano unaovutia ni vyema kuvaa suti inayoendana na mwili wake

"Suti ikiwa kubwa au ndogo kuliko mwili wako pamoja na kukuharibia muonekano lakini taswira itakayojengeka kwa baadhi ya watu wanaokutazama ni kuwa umeazima, hivyo suala la vipimo ni muhimu kulizingatia," aliongeza.

Vilevile aligusia suala la uvaaji wa tai na kueleza kuwa ni muhimu kukadiria urefu sahihi na mlingano wa tai na koti.

Alisema tai inafanya muonekano wa mtu aliyevaa tai kuvutia zaidi endapo haitakuwa fupi sana wala ndefu sana.

"Tai inatakiwa isiwe ndefu mpaka kuvuka mkanda, inaweza kuwa juu kidogo ya mkanda au kukaribia juu ya mkanda,"alisema.

Nae fundi wa nguo za kike na kiume, Abdul Kilumbi alielezea kuwa mambo mengine muhimu ambayo hufanya muonekano wa mtu aliyevaa suti kuvutia zaidi ni pamoja na kuchagua tai ambayo rangi yake imekolea kuliko shati, rangi ya mkanda inapendeza zaidi ikifanana na ile ya viatu pamoja na kuzingatia ulingano wa upana wa tai na upana wa kola za koti. 

Kilumbi alisema, "Pia ili kuonekana classic na unayejua mitindo, ni vyema unaposimama kukumbuka kufunga kifungo cha koti na kukifungua pale unapohitaji kukaa, vilevile ni vizuri kuhakikisha huweki vitu vingi visivyokuwa na ulazima katika mifuko ya suruali au koti pale unapovaa suti."

Kwa mujibu wa tovuti ya editsuit, wameanisha mambo mbalimbali ya kuzingatia unapotaka kununua au kushona suti ikiwemo mahali na aina ya shughuli unayotaka kwenda ikiwa umevaa suti hiyo, rangi, majira, material zilizotumika kutengeneza kitambaa cha suti hiyo, mitindo iliyopo kwa wakati huo pamoja, kuzingatia muonekano wako na mengine mengi. 

Naaam ama kwa hakika tutakua tumefahamiana vizuri kabisaaa kupitia dondoo hii fupi ya fashion,n wewe tu mdau ni fursa kwako kuchambua na kuongeza manjonjo yako tukutane wakati ujao. bye bye!

 


Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Saphinia Suleiman

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, career, skills development and technology.


Latest Post