Mambo muhimu kwa Mwanafunzi wa Elimu ya juu

Mambo muhimu kwa Mwanafunzi wa Elimu ya juu

 

Habari vijana wa Tanzania hasa wanafunzi wa elimu ya juu kokote mlipo duniani.

Nina furaha kubwa kupata fursa hii kuandika ujumbe huu kwenu. Hii ni kuhusu elimu ya juu na maisha halisi. Kama niwashaurivyo ninyi, nami pia najishauri!

Jambo ambalo ni muhimu sana tukalijua na tukatambua ni kwamba  elimu ni msingi wa maisha. 

Tuelewe kuwa lengo kubwa la sisi kuwa wanafunzi wa fani mbalimbali ni kutengeneza msingi ili tuweze kujenga maisha yetu. Kwa msemo huu, ni maana kwamba elimu ni nyenzo mojawapo ya kutupa mwanga wa kufika sehemu. 

Kwa kusema hivyo ninamaanisha kwamba elimu si kila kitu, bali ni nyenzo tu! Inawezekana ukasoma mambo yanayohusu uhandisi wa majengo lakini ukajikuta umekuwa meneja wa mgahawa. 

Au unaweza ukasomea fani ya mambo ya biashara ila ukajikuta ukaingia jeshi ukipiga kwata kila siku! Hayo yote yanawezekana na ukajiuliza kwanini ulisomea uhandisi lakini upo kwenye umeneja. 

Hapo ndipo inabidi utambue kwamba elimu uliyoisoma ni nyenzo tu na itabidi ujue jinsi ya kuitumia ili ifanikishe ujenzi wa nyumba nzima. Kumbuka kuwa msingi mbaya katika maisha kutaiporomosha nyumba unayoijenga.

Japo mfumo wa elimu yetu si rafiki sanaaa ambao unaweza kuturuhusu sisi kufanya mambo mengine kama vile ya kutuingizia kipato, ukweli ni kwamba bado hautufungi kujifunza vitu zaidi ya fani tunazosoma au kuwa sehemu ya wafanyakazi wasio rasmi. 

Kwa kusema hili, nataka kukufahamisha mambo unayopaswa kufanya ni pamoja  kuhudhuria matamasha ya kukujenga na kukufurahisha; fanya bidii katika kutengeneza mifumo saidizi ambayo itakufanya hata mara baada ya kumaliza chuo utapata nafasi ya kujiendeleza au kupata sehemu ya kujishikiza mahala popote.

Pia huna budi kufanya biashara halali isiyovunja sheria za nchi na hiyo utafanikiwa kama utaweka juhudi na bidii katika kila fursa utakayoipata. 

Pili, unapaswa kuwa mtu unayependa kuhudhuria katika midahalo ya kimaendeleo, kiuchumi, ukuaji wa teknolojia na sayansi kwani midahalo hii itakupa mwanga kuhusu ni nini kinachotokea duniani katika uhalisia wenyewe. 

Kwani ni kweli kuwa elimu na mitaala na vitabu tunavyovisoma wengi haitupi hali na picha halisi ya ukuaji wa dunia yetu katika mambo yote. Hivyo, "Jishughulishe, ukibweteka mwisho wa siku utarudisha mpira kwa golikipa."

Katika elimu, usiendekeze starehe zaidi. Kuwa na kipimo sahihi katika kila unachokifanya (iwe katika masomo au starehe). Maisha yako yanategemeana kwa namna moja ama nyingine. 

Ukizidisha upande mmoja unaua upande mwingine. Jiandae, jikabili na jitunze katika mambo yote. Huwezi ukazidisha kitu kimoja na kukisahau kingine kwa maana kila kitu kina nafasi yake. Jua jinsi ya kuikabili starehe yako unayoihusudu sana ili kufanya kila kitu kiwe katika mlinganyo stahiki ambao hautakufanya upoteze malengo yako!

Kundi ulilokuwa nalo chuoni, kwa asilimia kubwa linakusahilisha wewe kwa maisha yako hata baada ya chuo. Hivyo hakikisha unakuwa na kundi ambalo linakujenga, linakupa motisha ya kwenda mbele, linakuonya na kukusikiliza. 

Itaendelea wiki ijayo….






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags